CCM yamwandalia chopa kujibu mapigo ya M4C Pamoja Daima
USHINDANI wa
kisiasa kati ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(CHADEMA) umefikia hatua mpya baada ya CCM kuibuka na mkakati wa kumtumia
Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe, kupambana na CHADEMA waziwazi.
Katika mkakati huo
CCM imepanga kukodisha helikopta ya kumpeleka Zitto katika mikoa minne kwa
gharama ya sh milioni 50 mara tu baada ya CHADEMA kuhitimisha Operesheni yao ya
M4C Pamoja Daima.
Kwa mujibu wa
taarifa kutoka vyanzo vilivyo karibu na Zitto na CCM, yeye na chama hicho sasa
wana adui mmoja – CHADEMA; na wameamua kujibu mapigo baada ya kuridhika kwamba
kwa vyovyote Zitto amekwisha kupoteza uanachama wake katika CHADEMA.
Nia yao ni kumtumia
Zitto kuleta mpasuko katika CHADEMA, na kufunika mjadala wa mgogoro wa CCM,
kero za wananchi na mchakato wa Katiba mpya.
Zitto ambaye
alivuliwa nyadhifa zake zote ndani ya CHADEMA – Naibu Katibu Mkuu Bara, Mjumbe
wa Kamati Kuu, Mjumbe wa Baraza Kuu na Naibu Kiongozi wa Kambi Rasmi ya
Upinzani Bungeni – anatarajia kutumia helikopta yenye uwezo wa kubeba watu
wanne, ambayo inadaiwa kukodishwa na wapinzani wa CHADEMA.
Kwa mujibu wa
habari hizo, lengo la ziara ya Zitto ni kujibu mapigo ya CHADEMA, hasa katika
maeneo ambayo baadhi ya makada na viongozi wa chama hicho wamepita na
kuzungumzia hatima yake kisiasa, hasa walipojibu maswali ya wananchi kuhusu
sakata lake kuvuliwa uongozi kwa tuhuma za usaliti, na hatimaye Zitto kwenda
mahakamani kuzuia chama kujadili uanachama wake.
Katika kesi ya
msingi, Zitto aliyewahi kuwa maarufu akiwa kiongozi wa CHADEMA, anaomba
arudishiwe nyadhifa zake zote, na apatiwe nakala za uamuzi wa Kamati Kuu (CC)
ili aweze kukata rufaa Baraza Kuu.
Taarifa zinasema
tayari chama kimempatia nyaraka hizo, lakini kwa mujibu wa Katiba ya CHADEMA,
Zitto amekwisha kujiondoa kwenye chama hicho kwa kupeleka shauri mahakamani.
Taarifa za Zitto
kuanza ziara mikoani zilianza kusikika mwishoni mwa wiki iliyopita.
Mikoa iliyotajwa ni
Kilimanjaro, Arusha, Tanga, Morogoro na Dar es Salaam, ingawa maandalizi
yanaendelea na kuna uwezekano wa kubadili baadhi ya mikoa kulingana na mkakati
wao.
Kwa hadhi yake ya
sasa, CHADEMA imeshasema haitahusika na mikutano yake, na wanachama wake
hawatajihusisha nayo. Uratibu wa mikutano yake unafanywa na viongozi waandamizi
wa CCM.
Baadhi yao
walizungumza na gazeti hili kwa kujitapa kwamba hii ndiyo njia ya kuimaliza
CHADEMA, lakini hawakutaka kutajwa majina gazetini.
Iwapo Zitto
atakubali ufadhili huo wa CCM na kuendelea na mikutano yake, ni wazi atakuwa
amekamilisha ushahidi wa kinachodaiwa na chama chake kwamba amekuwa akikisaliti
kwa masilahi ya CCM.
Hata hivyo, baadhi
ya viongozi wa CCM walipoombwa maelezo juu ya urafiki wao na Zitto kiasi cha
kumkosanisha na chama kilichomlea kisiasa, CHADEMA, walisema kwamba urafiki
uliopo si wa Zitto na CCM, bali Zitto na Rais Jakaya Kikwete.
Gazeti hili
linafahamu kwamba wakati fulani mwaka juzi Zitto alipobanwa na wabunge wenzake
kuhusu tabia zake za kuwasaliti kwa Rais Kikwete, alisisitiza kuwa Rais Kikwete
ni rafiki yake binafsi, kwa hiyo wamwelewe.
Vilevile, wapo
wanaohoji nia ya ziara hii wakati kwa muda mrefu amekuwa akikwepa kuambatana na
viongozi wenzake katika ziara na operesheni nyingi za kichama.
Wanasema kwa kuwa
operesheni ya sasa ya CHADEMA imepewa jina la M4C Pamoja Daima, kitendo cha CCM
kuandaa ziara ya Zitto na kumkodishia helikopta, ni uthibitisho kuwa Zitto
hayuko pamoja na CHADEMA tena.
Wameongeza pia kuwa
kama hilo litafanyika, litakuwa limemwingiza Zitto katika orodha ya makada
kadhaa wa upinzani waliotumikia CCM baada ya kufukuzwa au kunyimwa fursa za
uongozi katika CHADEMA, kama Tambwe Hiza, Dk. Aman Walid Kabourou na Dk.
Masumbuko Lamwai.
Alipotafutwa
athibitishe kuhusu ziara hii na kama ni kweli inafadhiliwa na CCM, Zitto
hakuweza kupatikana.
Mbowe kuwania tena
uenyekiti
Katika hatua
nyingine, Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman
Mbowe, amesema kuwa kamwe hatakiacha chama hicho katika uchanga wa harakati za
kulikomboa taifa kama kiongozi wake wa juu.
Akihutubia katika
mikutano ya Operesheni M4C Pamoja Daima katika sehemu mbalimbali mkoani
Morogoro jana, mwenyekiti huyo alisisitiza kuwa, bado atagombea nafasi ya
uenyekiti kwa lengo la kuendeleza harakati za ukombozi wa pili wa taifa hili.
Bila kutaja jina,
Mbowe alionya kuwa wenye fikra za kuachiwa chama hicho kikiwa katikati ya
ukombozi huo hawatapata nafasi, kwa sababu hawana nia thabiti ya kukiendeleza,
bali wana nia ya kukibomoa kwa kutumiwa na wapinzani wa CHADEMA.
“Makamanda,
kumbukeni kuwa chama hiki na sisi viongozi wake tumepita katika majaribu
makubwa na hata kukoswakoswa kuuawa. Mimi nimekoswakoswa kuuawa kwa bomu huko
Arusha, lakini pia kuna watu wamepoteza maisha, wamefungwa jela, wengine wamekuwa
vilema, halafu watu wengine wanatusaliti kwa kupewa visenti ili wakivuruge
chama na wanataka tuwape chama. Huu ni uendawazimu,” alisema.
Mwenyekiti huyo
alisema CCM imekuwa ikifanya jitihada za kuihujumu CHADEMA kwa mbinu
mbalimbali, zikiwemo za kupandikiza migogoro, jambo ambalo limeshindwa
kufanikiwa kwani Mungu ameweka mkono wake ili kisisambaratike.
“Harakati hizi
tunazofanya za kuwakomboa Watanzania mjue tunahatarisha maisha yetu,
tumejaribiwa kushawishiwa ndani na nje ya Bunge ili tuwe kondoo, tumekataa. CCM
wamekuja na mbinu za kupandikiza migogoro wameshindwa na sasa wanaomba nife
wakifikiri nikifa na CHADEMA itakufa. Nawaambia CHADEMA haifi kwa kuwa
tumezalisha makamanda wengi, watakiendeleza,” aliongeza Mbowe.
Akielezea kwa mara
ya kwanza kwa undani zaidi kuhusu mauaji ya Arusha, mwenyekiti huyo alisema
wana ushahidi wa kutosha kwamba polisi walihusika na mauaji hayo na kuongeza
kuwa waliohusika ni polisi wa kutoka mkoani Morogoro.
“Kwa mara ya kwanza
niliseme hili, mauaji ya Arusha yaliyofanyika kwa kurusha bomu katika mkutano
wa kampeni za CHADEMA, yalifanywa na polisi ambao walitoka mkoani Morogoro.
Ndiyo maana tunaendelea kumwambia Rais Jakaya Kikwete aunde tume ya kimahakama
ili kupata ukweli wa jambo hili,” alisema.
Kuhusu Katiba
Akizungumzia
msimamo wa CHADEMA kuhusu muungano, Mbowe alisema chama hicho kinaunga mkono
maoni yaliyokusanywa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba inayoongozwa na Jaji
Joseph Warioba, ya serikali tatu.
Alisema hata tafiti
mbalimbali zilizofanyika, zikiwemo za wanasheria na wachumi zinaonyesha kuwa
Muungano utaimalika zaidi chini ya muundo wa serikali tatu.
“Nawaonya Wana CCM
wasijaribu kuingilia mjadala wa Bunge la Katiba na kama wanataka nchi
ichimbike, basi walazimishe serikali mbili,” alisema Mbowe.
“Zipo tetesi za CCM
kutaka kupitisha hoja zao kwa nguvu kutokana na idadi yao ndani ya wabunge
zaidi ya 600, wakiwemo 356 wa Bunge la Tanzania Bara, 84 kutoka Zanzibar na 201
kutoka makundi mbalimbali watakaokwenda kwenye bunge hilo. Wasidanganyike
kwamba wanaweza kutumia wingi wao kubadilisha maoni ya Watanzania kuhusu
serikali tatu,” alisisitiza Mbowe.
Halima Mdee
anguruma
Naye Mbunge wa
Kawe, Halima Mdee, ambaye yuko katika msafara wa mwenyekiti huyo, alisema
vijana wengi wanaochipukia katika siasa kupitia chama hicho, wamelelewa na
Mbowe, ambao leo wamekuwa chachu ya mabadiliko nchini.
“Ukweli ni kwamba
kamanda huyu wa anga (Mbowe), ndiye ametulea vijana wengi nikiwemo mimi, tena
wengine hatukuwa na ujasiri tulionao sasa, asiwadanganye mtu, hasa sisi vijana
kwamba tuliingia CHADEMA na umaarufu, hawapo hao, tumelelewa na huyo kamanda,”
alisisitiza huku akipigiwa makofi.
Tanznia Daima