Wasiliana nasi : chademadiaspora@gmail.com -Fair and Balanced Platform- Twitter @ChademaDiaspora

Wasiliana nasi : chademadiaspora@gmail.com -Fair and Balanced Platform- Twitter @ChademaDiaspora
----------------------WE THANK AND APPRECIATE YOU FOR VISITING CHADEMA DIASPORA BLOG. AGAIN, THANK YOU!-----------------------

Friday, January 31, 2014

Malecela amvaa Edward Lowassa


  Ni mbio za urais 2015
  Amtuhumu kumwaga fedha

Makamu Mwenyekiti mstaafu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Samuel Malecela, akiwaonyesha waandishi wa habari (hawapo pichani) moja ya fulana iliyoandikwa Friends of Edward Lowassa (Marafiki wa Edward Lowassa) alizodai kuwa zimesambazwa nchi nzima. Malecela alifanya hivyo wakati akizungumza na waandishi wa habari nyumbani kwake mjini Dodoma jana.

Vita ya kusaka urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) inazidi kuchukua sura mpya kila uchao na safari hii Makamu Mwenyekiti mstaafu wa chama hicho Bara, John Malecela, ameibuka na kuelekeza mashambulizi yake dhidi ya Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, kwa kumtuhumu kuwa anausaka urais kwa kutumia fedha. Mbali na kumtaja Lowassa wazi, pia ameishambulia sekretarieti ya chama hicho kwa kile alichosema inakaa kimya bila kukemea harakati za watu wanaousaka urais kupitia CCM kinyume cha misingi na katiba ya chama. Akizungumza na waandishi wa habari nyumbani kwake mjini Dodoma jana, Malecela ambaye pia ni Waziri Mkuu na Makamu wa Rais mstaafu, alisema kuwa ingawa sekretarieti ya chama hicho inajua muda wa kuanza mbio za urais bado haujafika, imekaa kimya bila kutoa karipio lolote.


Mbali ya kumtaja Lowassa ambaye pia ni Mbunge wa Monduli, akisema kuwa ni miongoni mwa  wanachama walioanza harakati hizo na kwamba amekuwa akikivuruga chama, alisema ana ushahidi wa harakati zake. “Hapa najiuliza kuwa ile misingi imara ya uongozi ndani ya chama chetu iko wapi? Mpaka tumuachie mtoto (Katibu wa kitengo cha Uhamasishaji na Chipukizi wa UVCCM, Paul Makonda) ndiye akemee haya? Je, hapa chama kiko wapi?” alihoji Malecela. Alisema kuwa anamuunga mkono Makonda kwa kitendo chake cha ujasiri cha kumkemea Lowassa bila woga kutokana na anavyokivuruga chama kwa lengo la kutaka urais. “Naomba niseme kuwa bila kuwa na karipio au tamko la chama, hawa wanaotumia pesa zao hadharani kwa lengo la kutafuta umaarufu na ushawishi kwa vijana ili kupata madaraka wanaharibu misingi yetu bora ya uongozi iliyowekwa na waasisi wetu ndani ya chama,” alisema Malecela na kuongeza: “Kinachonisikitisha zaidi ni kuona juhudi za uongozi wa sasa wa chama ngazi ya juu ikiwa ni pamoja na sekretarieti inayoongozwa na Katibu Mkuu, Abdulrahman Kinana na Katibu Mwenezi, Nape Nnauye, za kutetea chama hiki zinatiwa mchanga,” alisema.

Alisema vijana ndiyo wamekuwa wakijenga na kuimarisha chama kwa kukemea na kueleza misingi ya uongozi bora. “Je, chama hakioni haya mpaka vijana ndio waone?” alihoji Malecela.Malecela aliishauri sekretarieti ya chama hicho kuchukua hatua mara moja kwani Makonda asingesema hayo yote kama hana ushahidi wa aliyoyasema. “Na tunapozidi kuchelewa suala hili linazidi kuleta mgawanyiko...vijana na wanachama wa CCM wamekuwa na hamu kwa muda mrefu ya kutaka kujua msimamo wa chama chao bila mafanikio na ndiyo sababu ya baadhi ya wengine kupoteza mwelekeo,” alisema. Alisema wao walikijenga chama kwa tabu sana na kwamba hakuna mwanachama aliyediriki kutumia fedha zake kutafuta madaraka. “Nidhamu, busara na uchungu wa rasilimali za taifa hili kwa maslahi ya wananchi ndiyo vilituongoza kufuata misingi na maadili ya uongozi ndani ya chama na serikalini, ndiyo maana tunaumia sana kuona chama sasa kinataka kutekwa na wenye fedha kutafuta madaraka,” alisema.

Aliongeza: “Mpaka tunashangaa na kujiuliza hizi pesa wanazotumia wanazipata wapi? Haya madaraka wanayotaka kwa kununua ni kwa maslahi ya nani huku Watanzania wakiendelea kuwa maskini, sisi Watanzania siasa yetu isimame kwa upande wa maskini.”  Akizungumzia suala la malumbano ndani ya chama, alisema vitendo hivyo havina tija kwa chama. “Hivi karibuni baadhi ya viongozi wa chama ngazi ya juu wamejibishana kwenye vyombo vya habari, vitendo hivi havina tija kwa chama na wala havileti umoja na mshikamano ambao umedumu ndani ya chama kwa muda mrefu,” alisema Malecela bila kuwataja. “Ninaomba sekretariate ichukue hatua haraka kama alivyoomba kijana wetu Makonda na kweli kuchelewa kuchukua hatua jambo hili kumejionyesha wazi kwamba kutaleta kutoelewana ndani ya chama kusikokuwa na ulazima,” alisema Malecela.Alipoulizwa na waandishi sababu za kumtaja Lowassa peke yake, Malecela alisema hawajui wengine bali Lowassa.

Baadaye aliingia chumbani na kuchukua fulana mbili na kuwaonyesha waandishi moja ikiwa na rangi nyeusi na kahawia na nyingine rangi nyekundu na nyeupe zikiwa zimeandikwa ‘Friends of Edward Lowassa’ (marafiki wa Lowassa) na kusema kuwa fulana hizo zipo sehemu mbalimbali za nchi. Katika mkutano huo pia alisema siyo busara kutowapongeza Kinana na Nape kwa kujijenga chama na kuwaeleza wananchi juu ya misingi bora ya chama kwa kukemea viongozi wasiofaa bila kujali cheo na umaarufu wao ndani ya chama na serikali.  “Nawaomba waendelee na juhudi zao hizo nami naziunga mkono juhudi zao na kama kuna watu wanaowabeza, naomba wasijali kwani kukemea viongozi wasiofaa ni msingi wa chama chochote kilichounda serikali,” alisema Malecela. NIPASHE lilipomtafuta Lowassa kuzungumzia kauli hizo hakupatikana. Hata hivyo, mmoja wa wasaidizi wake alipoulizwa, alisema hana la kusema.

KAULI ZA MAKONDA

Jumanne wiki hii, Makonda alitoa taarifa iliyojaa maneno makali akimshambulia Lowassa na baadhi ya viongozi wa dini akiwahusisha na kampeni za uchaguzi wa urais mwakani. Bila kutaja jina la kiongozi yeyote wa dini, ila tu kurejea kwa ujumla wao kama maaskofu na masheikh, Makonda, aliwataka kwenda kwa Lowassa kama wanataka fedha za haraka. Hakusema ni fedha za nini. Makonda alisema  hawawezi kukaa kimya wakati viongozi wa CCM wakishambuliwa na watu aliosema hawana mapenzi mema na chama chao. Alisema wapo watu aliodai wanafadhiliwa na Lowassa ili kuwashambuliwa viongozi wa sekretarieti ya CCM, Kinana na Nape kwa kuwa anautaka urais mwakani. Aliwataja makada wa CCM aliodai wanaosukumwa na Lowassa kuwa ni Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Singida, Mgana Msindai na Mwenyekiti mstaafu wa CCM Dar es Salaam, John Guninita.

Makonda aliwatuhumu makada hao kuwa ni wahaini, waongo na wazandiki, na kueleza kuwa kama nia yao ni kusaka urais kwa ajili ya Lowassa, basi wajue kuwa amekosa sifa za kuteuliwa na chama hicho kuwania wadhifa huo katika uchaguzi mkuu wa mwakani. Hata hivyo, siku hiyo muda mfupi tu baada ya kauli ya Makonda, Makamu  Mwenyekiti wa UVCCM, Mboni Mhita, alisema kauli hiyo siyo msimamo wa UVCCM bali ya Makonda binafsi.

Ippmedia/Nipashe

No comments: