Wasiliana nasi : chademadiaspora@gmail.com -Fair and Balanced Platform- Twitter @ChademaDiaspora

Wasiliana nasi : chademadiaspora@gmail.com -Fair and Balanced Platform- Twitter @ChademaDiaspora
----------------------WE THANK AND APPRECIATE YOU FOR VISITING CHADEMA DIASPORA BLOG. AGAIN, THANK YOU!-----------------------

Friday, June 21, 2013

PINDA KAWAPA WANANCHI HAKI YA KUJITETEA DHIDI YA POLISI

MM Mwanakijiji

        Kwa mara nyingine tena Waziri Mkuu Pinda ametoa kauli ambayo inatafsirika kuwa ni kuhalalisha vyombo vya usalama kuvunja haki za msingi za wananchi kwa kuwapiga na hata kuwaua. Kauli hiyo iliyotolewa leo Bungeni inatukumbusha sisi wengine kauli yake nyingine aliyoitoa wakati mauaji ya Albino yamepamba moto pale alipoonekana kuhalalisha wananchi kuchukua hatua mikononi. Inawezekana watu wengi wameshasahau kauli ile. Akizungumza Bungeni Waziri Mkuu Pinda akionesha kuchoshwa na mauaji ya Albino alisema hivi “Mkimuona mtu akamkata mwingine shingo naye muueni kwani sasa viongozi wote tumechoka... no more, I can't tolerate anymore (imetosha, siwezi kuvumilia tena” na hakuishia hapo bali aliagiza Umoja wa Vijana wa Chama chake kutekeleza agizo hilo kwa kuwaambia “Umoja wa vijana wa CCM mna jeshi zuri ambalo naamini mkiamua mnaweza kutokomeza mauaji ya wazee wetu pmoja na ndugu zetu maalbno na kazi hiyo nawaagiza muanze leo msisubri auawe mwingine tena”

       Kitu ambacho Pinda hajakielewa na inaonekana hana uwezo wa kukielewa ni kuwa hakuna binadamu anayependa kutendewa kama vile si binadamu. Hakuna mwanadamu ambaye anaweza kuendelea kukubali kudharauliwa, kupuuzwa, kunyanyaswa na kuteswa kwa vile tu wale wanaofanya hivyo wanaamini wanauwezo wa kufanya hivyo. Kauli ya Pinda ni ushahidi wa yeye na wale walioshangilia kutokujua historia.


      Nimesoma baadhi ya michango ya watu ambao wanaunga mkono kauli ya kipuuzi kama hii wakiamini wanafanya hivyo wakiwakilisha jambo jema. Historia inao watu kama hao na ni wengi wameenda na kusahauliwa katika giza la historia wakiamini walikuwa wanatetea ‘uzalengo’ au ‘utaifa’. Ni vizuri kumkumbusha Pinda na mashabiki wake kuwa binadamu ana kikomo cha kunyanyaswa, kupuuzwa na kudharauliwa anapofika kwenye kikomo hicho (prespice) mwanadamu atachukua hatua tu!

Uasi wa Watumwa wa Meli ya Amistad 1839


       Meli ya Kihispania ya La Amistad ilibeba kundi la watumwa kutoka Afrika ya Magharibi (Sierra Leone) na walikuwa wanaenda kuuzwa tena (kama bidhaa) kwenye mojawapo ya nchi za Amerika. Watumwa wale walijitambua kuwa wao ni binadamu na kuwa waliishi kama watu huru kabla ya kukamatwa na kuuzwa utumwani. Hawakuwa wanajua mambo mengi ya watekaji wao lakini walijua kitu kimoja - minyororo waliyofungwa ilikuwa ni minyororo siyo tu ya kufunga mifupa yao bali pia kufunga fikra zao.

      Julai 2, 1839 (miaka 174 iliyopita) Wakiwa njiani kuelekea kwenye soko hilo la watumwa (Cuba) watumwa wale walikula njama wao wenyewe na kuasi na kuwapiga wafanyabiashara wa utumwa na kuwalazimisha wawarudishe Afrika. Lakini kiujanja manahodha badala ya kuipeleka meli Afrika wakati wa usiku wakawa wanailekeza Kaskazini na lakini ikakamatwa na majeshi ya Marekani na kulazimishwa kutia nanga Long Island, New York.

      Kutoka Long Island kesi moja kali sana ya haki za binadamu ilifanyika ambayo bado imeoneshwa katika filamu ya Amistad (1997) ya Steven Spielberg. Swali kubwa lilikuwa je watumwa wale walipoamua kutumia nguvu na hata kuua watekaji wao wakidai uhuru wao walifanya uhalifu? Na je kuwa kwao Waafrika kuliwafanya wasiwe binadamu wenye haki?

      Kesi ilinguruma na hoja zilibishaniwa lakini mwisho wa siku Mahakama zote zilizosikiliza kesi hii zilikubaliana kuwa Watumwa wale walikuwa ni watu huru walipokamatwa na hivyo walikuwa na haki ya kupigania uhuru wao kwa namna yoyote ile na hivyo uasi wao ulikuwa halali! Mahakama ikaruhusu Waafrika wale kufanyiwa mipango ya kurudishwa kwao na fidia walipwe. Waafrika wale hawakuhitaji kupewa elimu ya uraia kujua kuwa walikuwa wanadhulumiwa na wala hawakuhitaji chama cha siasa kuwaongoza kukataa dhulma! Hawa hawakuwa peke yao katika historia.

Uasi wa Meermin wa Madagascar 1766

      Japo uasi wa Amistad unajulikana sana (labda kwa sahabu unahusisha Marekani) lakini uasi mwingine wa Waafrika waliokataa kuchukuliwa watumwa ulifanyika miaka 73 nyuma katika bahari ya Hindi. Meli ya Meermin ilikuwa nimojawapo ya meli za Waholanzi zilizobeba watumwa na ilikuwa imebeba watu wa Malagasy ambao walikuwa waende kuwa vibarua kwenye mashamba ya kampuni ya Dutch East India Company huko kwenye jimbo la Cape Africa ya Kusini. Watumwa wale wakaamua kuasi na wakafanya uasi mkubwa kwelikweli; waliua nusu ya wazungu waliokuwemo mle na kuagiza meli igeuze njia kuwarudisha Madagascar. Kama ilivyokuwa kwa Amistad manahodha wakatumia ulaghai na kuielekeza meli Afrika y a Kusini ambako ilitia nanga na watumwa wale waliohadaiwa wakajikuta wanaangukia mikononi mwa watesi wao.

      Maofisa wa meli walishtakiwa na watumwa waliachiliwa isipokuwa viongozi wa uasi huo ambao walijikuta wakitumikishwa katika Kisiwa cha Robben - ambapo miaka karibu mia mbili baadaye mpigania haki za weusi Nelson Mandela naye alifungwa. Watumwa hawa nao ambao kwa kiasi kikubwa historia imewasahau walijitambua kuwa wao ni nani na hawakujali waliowakamata walikuwa ni kina nani au wana nguvu gani; walitambua utu wao na walikuwa tayari kuupigania. Hawakuhitaji elimu ya uraia, hawakuhitaji viongozi wenye elimu kubwa walichohitaji ni kujitambua kuwa ni binadamu na hawakuwa tayari kuburuzwa, kudharauliwa, au kuteswa. Hawa nao hawakuwa peke yao.

Uasi wa Majimaji 1905

       Miaka 139 baada ya uasi wa Wamalagasy kule Afrika ya Kusini na miaka 66 baada ya uasi wa Amistad kule Uingereza Waafrika bado walijitambua utu wao na bado hawakutaka kunyanyaswa, kudharauliwa, na kuteswa na watawala wao. Wananchi wa makabila mbalimbali katika Tanganyika walijikusanya pamoja kuukataa utawala wa Mdachi (Mjerumani). Kilichowafanya kuukataa utawala huu haikuwa kukataa rangi ya Wadachi! Walikuwa wanakataa utawala wa mdachi juu yao.

         Katika kufanya hivyo waliamua kuasi; walinyanyaswa sana na waliteswa sana na kudharauliwa katika nchi yao na walipofikia kikomo walisema inatosha na wakaanza kujibu mashambulizi. Watawala waliwaita waasi, watawala walisema ni wachochezi na wanaleta vurugu katika koloni lililokuwa limetulia na lenye ‘amani’. Watawala wakasema wamechoshwa na wakaja na sera ya kuwashambulia mababu zetu; na kweli wengi walikufa mikononi mwa Wadachi! Nani atasahau yaliyomkuta Chifu Mkwawa, au kina Mpambalioto na Nduna Songea?

     Kuanzia Umatumbi hadi Umatengo, Mahenge hadi Nachingwea, toka ghala za silaha za Ifakara hadi ngome za Iringa; mto Rufiji hadi Mto Luwegu wazee wetu wakiwa hawana zaidi cha kupoteza isipokuwa utu wao. Walisimama na kupigana na watu waliowazidi kwa kila namna. Na kweli walishindwa, damu ilimwagika na watawala waliamini kuwa wameweza. Lakini historia haikuwahurumia watawala wale kwani miaka si chini ya kumi tu walijikuta wanapoteza koloni lao la thamani zaidi kwa wababe wengine. Historia ina tabia mbaya sana ya kujirudia rudia, hasa ukiidharau.

        Hivi kuna watu wanaamini wazee wetu walihitaji elimu ya uraia ili kujitambua? Hivi walihitaji kusoma sana kujielewa kuwa utu wao ulikuwa unadharauliwa? Kwamba wanahitaji wazungu waje kuwapa elimu ya kujitambua? Hivi kweli inahitaji usomi kujijua unadhulumiwa, unadharauliwa, na kuwa unatawaliwa isivyo haki?

        Kwa kuhalalisha uhalifu wa vyombo vya dola Pinda amewapa wananchi haki ya kujitetea! Alichokisema Pinda ni kitu ambacho hakina jina jingine isipokuwa amehalalisha uhalifu kufanywa na vyombo vya dola. Kama nilivyosema wakati ametoa ile kauli yake ya kuhalalisha uhalifu mwingine dhidi ya watuhumiwa Pinda anastahili kujiuzulu yeye mwenyewe ili kumpisha mtu mwingine mwenye hekima na uwezo wa kuongozza wakati kuna pressure. Alichokifanya kwa upande mmoja ni kutoa kibali kwa Polisi kuwapiga wananchi kwa sababu yoyote ile kwa kisingizio cha kuleta amani na utulivu! Lakini amefanya kitu kingine; amewapa wananchi haki ya kujitetea wakishambuliwa na Rais pasi ya haki.

Haki ya Kujitetea ni Haki ya Msingi ya Mwanadamu

       Mojawapo ya haki ambazo labda hatujazizungumza sana na hazieleweeki ni haki ya kujitetea (the right of self defence). Haki hii haijaleweka au haieleweki kwa wengi kwani inachanganywa na kuonekana ni uhalifu. Mwanadamu anayo haki ya kulinda nafsi yake na mali yake kutoka kwenye dhulma yoyote ile. Mara kwa mara haki hii tunaitumia kwa njia za sheria - kama kwenda mahakamani au kumkamata mwizi. Lakini inakuwaje kama jambazi amevamia familia yako na kuitishia maisha na wewe una silaha? Je unaweza kutumia silaha kuitetea familia yako? Jibu ni ndiyo! Hiyo ni haki yako na ukifanya hivyo kwa kujitetea maisha yako na ya familia yako ni vigumu kwa mahakama kukuta una hatia isipokuwa kama inaonekana kwa mfano, umeweza kumweka jambazi chini ya ulinzi na kumnyang’anya silaha halafu kwa kisasi ukaamua kumuua! Hapo huwezi tena kujitetea ‘self-defense”.

      Lakini inakuwaje kama wanaokushambulia ni maafisa wa vyombo vya usalama? Je maafisa wa vyombo vya usalama wakifuata agizo la Pinda wakakukufuza na kuanza kukupiga bila kujaribu kukukamata au kukuletea mashtaka au si kwa ajili ya kukuweka chini ya ulinzi unatakiwa kufanya nini? Je, polisi au wana usalama wanaweza kuja nyumbani kwako na kukushambulia kwa vile wanakushuku wewe ni mkorofii kama walivyofanya Mtwara je wewe nyumbani kwako una haki ya kujitetea?

      Baadhi ya watu ambao nimewasoma toka jana wanaamini kuwa serikali inaweza kupiga wananchi wake na wananchi hawapaswi kujitetea! Kuna watu ambao ukiwasoma wanaamini kabisa kuwa polisi na vyombo vya usalama vina haki na uwezo wa kuja na kukuambia “bong’oa” na wewe unatakiwa ubong’oe kwa sababu unatakiwa ‘kutii sheria bila shurti’! Wapo kabisa ambao wanaamini kabisa kuwa Mkuu wa Polisi fulani anaweza kuja na nyota na mwenge wake na kukuambua “panua” na wewe unatakiwa upanue tu kwa sababu yeye kasema! Kwamba wanaamini wananchi hawatakiwi kuwabishia polisi, hawatakiwi kuwauliza na kwa hakika hawatakiwi kuwapinga! Je hili ni kweli? Je ni kweli polisi wana nguvu hiyo katika maisha ya watu wetu kiasi kwamba watu wetu wanatakiwa watii bila shurti!? Yaani, watii lolote, popote, kwa lolote na vyovyote kwa vile wameamriwa hivyo?

      Mifano niliyotoa hapo juu inatupa jibu. Mwanadamu siyo mnyama ambaye anaweza kusukumwa sukumwa au kunyanyaswa na watu wenye nguvu na madaraka. Mwanadamu ameumbwa na dhamira na utu wake. Wapo wanadamu kati yetu ambao hawajali kunyanyaswa alimradi wanaachwa na “amani”. Wapo kati yetu ambao utu wao kwao ni chakula cha leo tu na ukiwapa chakula cha leo tu basi unaweza kuwafanyia lolote, popote, na kwa lolote! Naam, wapo kati yetu ambao hawawezi kuhoji serikali yao, hawawezi kuipinga, na kamwe hawatothubutu kulalamika kwa sababu wanaogopa au kuhofia kuonekana siyo watiifu. Hawa wakiambiwa ‘inama’ wanainama, ‘inuka’, ‘lala’ wanalala na wakiambiwa ‘lia’ wanalia kama wameona mzimu! Hawa hawana namna ya kuwasaidia kwani kila jamii inayo watu kama hao; watu ambao wanaabudu kwenye altare ya watawala wa zama zao!

Wapo kati yetu wanaojitambua 

        Lakini wapo kati yetu ambao wanajitambua. Wanajitambua kama watumwa wa Amistad au wazee wa Majimaji na kujiona kuwa na wao ni binadamu wenye kutaka kutambuliwa na kuthaminiwa utu wao kama walivyofanya wale wa Malagasi. Wapo kati yetu ambao wameamua kukataa watawala wa sasa, kuwapinga na kuwabishia; wamekataa kuendelea kufukiza uvumba mbele zao. Watawala hawawapendi hawa na maneno ya Pinda kimsingi yanawalenga hawa. Hawa hawatokubali kunyanyaswa na kudharauliwa na kwa vile Pinda amewapa kibali vyombo vya dola kuwapiga wananchi basi wananchi nao watakuwa wamejipa haki ya kujitetea dhidi ya polisi.

        Hili si jambo geni na mara nyingi ndio mwanzo wa machafuko makubwa ya nchi. Polisi wanapoanza kutekeleza amri kama za Pinda wananchi nao wanaanza kutenda kwa kujitetea na wanatangaza uadui na polisi na matokeo yake ni kuwa polisi watakaojifanya ndio wa kwanza kupiga wananchi bila sababu watajikuta wanarushiwa mawe na wao kuanza kupigwa. HIli likikitokea mimi sitoshangaa kwa sababu Mwanadamu ana haki ya kujitetea. Huu mtindo wa polisi kwenda kwenye nyumba za watu na kuanza kuwapa kipigo kutageuka kwani wananchi nao wataanza kutetea nyumba zao na familia zao.

       Pinda asije kudhani kuwa serikali inaweza ikashindana na wanananchi wake. Ni kweli inaweza kuwa na silaha nyingi na mbinu nyingi lakini wananchi wakiamua kujibizana na polisi serikali itashindwa na itaanguka yenyewe. Ndiyo historia ilivyo. Pinda afute kauli yake au aiweke vizuri. Akiiacha hivyo ilivyo kuwa polisi waanza kuwapiga tu wananchi kwa sababu ati wao kina Pinda wamechoka ajue kabisa kuwa amewapa na kibali wananchi haki ya kujitetea watakapoanza kupigwa.

Kwani nao wananchi wamechoka vile vile!

Niandikie: Mwanakijiji@jamiiforums.com

1 comment:

Diane said...

Kaka...I am reading this late at night and my eyes are getting big as I skim your long and detailed account. For now, I will say to you simply, yes. Kweli kabisa.
Will take the time to respond to you properly when I am rested. Bless you for reminding people of that history and those realities. Asante.