Wasiliana nasi : chademadiaspora@gmail.com -Fair and Balanced Platform- Twitter @ChademaDiaspora

Wasiliana nasi : chademadiaspora@gmail.com -Fair and Balanced Platform- Twitter @ChademaDiaspora
----------------------WE THANK AND APPRECIATE YOU FOR VISITING CHADEMA DIASPORA BLOG. AGAIN, THANK YOU!-----------------------

Friday, June 21, 2013

Mbowe, Lema ngangari

WATOKA MAFICHONI, WAGOMA KUTOA USHAHIDI POLISI


     MWENYEKITI wa Taifa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo, (CHADEMA), Freeman Mbowe na Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema wamejisalimisha polisi huku wakigoma kutoa ushahidi wa polisi kuhusika na mlipuko wa bomu uliotokea katika mkutano wa kufunga kampeni za udiwani Juni 15, mwaka huu. Mbowe na Lema waliokuwa mafichoni kwa siku mbili, walijisalimisha polisi jana saa nne asubuhi, walikochukuliwa maelezo kisha kupatiwa dhamana iliyowawezesha kushiriki mazishi ya kada mwenzao Judith Mushi aliyeuawa kwa bomu. Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kufanya mahojiano yaliyodumu kwa saa tatu, Mbowe alisema walipinga kufanya kusanyiko lisilo halali Juni 18, mwaka huu kwa madai kuwa mkutano huo uliovunjwa na polisi ulikuwa halali.

      Aliongeza kuwa licha ya polisi kwa kutumia mabomu ya machozi na maji ya kuwasha kuuvuruga mkutano huo, ukweli unabaki palepale ulikuwa halali kwani CHADEMA walikuwa na ruhusa na baraka za jeshi hilo. Mbowe alisisitiza CHADEMA wana ushahidi wa polisi kurusha bomu la gurumeti na risasi za moto kwenye picha za kawaida na za video na wako tayari kuutoa mbele ya tume huru ya majaji ya kimahakama endapo Rais Jakaya Kikwete ataridhia kuiunda na si vinginevyo. Wakiwa wameambatana na mawakili watatu wa chama hicho, Albert Msando, James Millya na Lemmy Bartholomew, Mbowe ambaye pia ni kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni alisema kuwa hawawezi kutoa ushahidi huo kwa polisi ambao ni watuhumiwa wa mauaji hayo ya mwanamke mmoja na watoto watatu.

       Alisema kumekuwa na mauaji mengi ambayo vyombo vya dola vimekuwa vikihusishwa huku kukiwa na ushahidi wa wazi pasipo wahusika kuchukuliwa hatua ya kisheria. Hata hivyo kauli hiyo ya Mbowe ilipingwa vikali na Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Liberatus Sabas na Kamishna wa mafunzo wa jeshi hilo, Paul Chagonja ambao walidai kuwa aliyowaeleza Mbowe ni tofauti na aliyowaeleza waandishi wa habari. Chagonja alisema kutokana na utofauti wa kauli za kiongozi huyo, Jeshi la Polisi linawasiliana na makachero wao ili kujua hatua zaidi za kuchukua dhidi ya viongozi hao.

     Alisema kuwa wakati wakihojiwa na polisi, viongozi hao walisema kuwa hawana ushahidi kwani na wao wanapata taarifa kutoka kwa wanachama wao juu ya tukio hilo. “Kimsingi mimi nashangazwa sana na Mbowe na wenzake, wanashindwa kuwa wakweli, huku wanasema hivi kule wanasema vile, tunawasiliana na wenzetu tujue cha kufanya,” alisema Chagonja.

Maziko ya kiongozi wa CHADEMA

          Viunga mbalimbali vya Arusha jana viligubikwa na simanzi, huzuni na vilio, wakati maelfu ya waombolezaji walipojitokeza kushiriki mazishi ya Katibu wa CHADEMA, Kata ya Sokoni One, Judith Mushi, aliyefariki dunia katika mlipuko wa bomu uliotokea Juni 15 wakati wa kuhitimisha mkutano wa kampeni za udiwani. Umati wa watu ulijitokeza katika hospitali ya rufaa ya mkoa ya Mount Meru, ulikokuwa umehifadhiwa mwili huo ambapo ulitolewa hospitalini hapo saa sita mchana na kupelekwa katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) katika eneo la Sokoni One kwa ajili ya ibada na kuuaga. Askari kanzu na wale waliovaa sare walitanda kila kona wakati msafara huo ukielekea kanisani na baadae makaburini, huku baadhi ya wananchi wakisitisha shughuli zao ikiwamo kufunga maduka ili kushiriki msiba huo.

Mchungaji aionya polisi

       Akisoma ibada kwa ajili ya marehemu, Mchungaji wa Kanisa la KKKT, Jimbo Mla Kaskazini, Isac Kisiria, alivilaumu vyombo vya dola kutumia nguvu kubwa kila wakati pasipo kutanguliza busara. Mchungaji Kisiria alisema kamwe uovu hauwezi kushinda haki na anasikitika kuona Tanzania ya sasa watu wanauawa mchana kweupe huku kukikosekana juhudi za kukomesha uovu huo. Alisema kifo cha Judith si mapenzi ya Mwenyezi Mungu bali kimelazimishwa na watu kwa tamaa za kidunia, huku akiwataka wananchi kutumia vifo hivyo kutafuta amani ya kweli na kuepuka vurugu zitakazosababisha mauaji zaidi. “Pamoja na yote yaliyotokea, nawasihi msiogope, tambueni damu hii haijamwagika bure, ni mbegu ya amani iliyopandwa,” alisema Mchungaji Kisiria.

       Alisema kumekuwa na matukio mbalimbali ya utekaji, utesaji na uuaji huku vyombo vya dola vikiwa havichukui hatua zinazostahili na badala yake huishia kusema wamejipanga kukabiliana na uhalifu. Mchungaji Kisiria alivitaka vyombo vya dola kuacha kutumia mabomu kwani hata wakiua watu, wajue wengine watajitokeza kuendeleza hatua iliyofikiwa na marehemu.
“Ukimsukuma kobe si kwamba umemkomoa bali ujue umemuongezea mwendo,” alisema.

Mbowe azidi kuvibana vyombo vya dola

      Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa, Mbowe akitoa salamu za chama chake katika msiba huo, alisema vyombo vya dola haviwezi kukwepa tukio hilo la kigaidi na kueleza kuwa lililenga kuwamaliza viongozi wa CHADEMA. Alisema kutokana na mkakati huo kushindwa, Jeshi la Polisi limeamua kuwabambikia kesi zisizokuwa na msingi wowote wafuasi na wanachama wa CHADEMA kwa ajili ya kupoteza malengo. Alisisitiza kuwa licha ya Tanzania kuwa nchi iliyoridhia kulinda haki za watoto na wanawake, katika shambulio hilo ndio wamekuwa wahanga wakubwa pasipo kulindwa na serikali. Alisema hata hatua ya viongozi wa kitaifa kukimbilia jijini Arusha na kutoa matamko ya kumtafuta mrusha bomu kwa ahadi ya kutoa sh milioni 100 si ya kiungwana kwa kuwa wameshindwa kuwasaidia majeruhi au ndugu wa marehemu katika suala zima la maziko.

Source: Macha G. (June 2013).Mbowe, Lema ngangari. Arusha. Retrieved from Tanzania Daima

No comments: