MM Mwanakijiji |
Kwa mara
nyingine tena Waziri Mkuu Pinda ametoa kauli ambayo inatafsirika kuwa ni
kuhalalisha vyombo vya usalama kuvunja haki za msingi za wananchi kwa kuwapiga
na hata kuwaua. Kauli hiyo iliyotolewa leo Bungeni inatukumbusha sisi wengine
kauli yake nyingine aliyoitoa wakati mauaji ya Albino yamepamba moto pale
alipoonekana kuhalalisha wananchi kuchukua hatua mikononi. Inawezekana watu
wengi wameshasahau kauli ile. Akizungumza Bungeni Waziri Mkuu Pinda akionesha
kuchoshwa na mauaji ya Albino alisema hivi “Mkimuona mtu akamkata mwingine
shingo naye muueni kwani sasa viongozi wote tumechoka... no more, I can't
tolerate anymore (imetosha, siwezi kuvumilia tena” na hakuishia hapo bali
aliagiza Umoja wa Vijana wa Chama chake kutekeleza agizo hilo kwa kuwaambia
“Umoja wa vijana wa CCM mna jeshi zuri ambalo naamini mkiamua mnaweza
kutokomeza mauaji ya wazee wetu pmoja na ndugu zetu maalbno na kazi hiyo
nawaagiza muanze leo msisubri auawe mwingine tena”
Kitu ambacho
Pinda hajakielewa na inaonekana hana uwezo wa kukielewa ni kuwa hakuna binadamu
anayependa kutendewa kama vile si binadamu. Hakuna mwanadamu ambaye anaweza
kuendelea kukubali kudharauliwa, kupuuzwa, kunyanyaswa na kuteswa kwa vile tu
wale wanaofanya hivyo wanaamini wanauwezo wa kufanya hivyo. Kauli ya Pinda ni
ushahidi wa yeye na wale walioshangilia kutokujua historia.
Nimesoma
baadhi ya michango ya watu ambao wanaunga mkono kauli ya kipuuzi kama hii
wakiamini wanafanya hivyo wakiwakilisha jambo jema. Historia inao watu kama hao
na ni wengi wameenda na kusahauliwa katika giza la historia wakiamini walikuwa
wanatetea ‘uzalengo’ au ‘utaifa’. Ni vizuri kumkumbusha Pinda na mashabiki wake
kuwa binadamu ana kikomo cha kunyanyaswa, kupuuzwa na kudharauliwa anapofika
kwenye kikomo hicho (prespice) mwanadamu atachukua hatua tu!
Uasi wa
Watumwa wa Meli ya Amistad 1839
Meli ya
Kihispania ya La Amistad ilibeba kundi la watumwa kutoka Afrika ya Magharibi
(Sierra Leone) na walikuwa wanaenda kuuzwa tena (kama bidhaa) kwenye mojawapo
ya nchi za Amerika. Watumwa wale walijitambua kuwa wao ni binadamu na kuwa
waliishi kama watu huru kabla ya kukamatwa na kuuzwa utumwani. Hawakuwa wanajua
mambo mengi ya watekaji wao lakini walijua kitu kimoja - minyororo waliyofungwa
ilikuwa ni minyororo siyo tu ya kufunga mifupa yao bali pia kufunga fikra zao.
Julai 2,
1839 (miaka 174 iliyopita) Wakiwa njiani kuelekea kwenye soko hilo la watumwa
(Cuba) watumwa wale walikula njama wao wenyewe na kuasi na kuwapiga
wafanyabiashara wa utumwa na kuwalazimisha wawarudishe Afrika. Lakini kiujanja
manahodha badala ya kuipeleka meli Afrika wakati wa usiku wakawa wanailekeza
Kaskazini na lakini ikakamatwa na majeshi ya Marekani na kulazimishwa kutia
nanga Long Island, New York.
Kutoka Long
Island kesi moja kali sana ya haki za binadamu ilifanyika ambayo bado
imeoneshwa katika filamu ya Amistad (1997) ya Steven Spielberg. Swali kubwa
lilikuwa je watumwa wale walipoamua kutumia nguvu na hata kuua watekaji wao
wakidai uhuru wao walifanya uhalifu? Na je kuwa kwao Waafrika kuliwafanya
wasiwe binadamu wenye haki?
Kesi
ilinguruma na hoja zilibishaniwa lakini mwisho wa siku Mahakama zote
zilizosikiliza kesi hii zilikubaliana kuwa Watumwa wale walikuwa ni watu huru
walipokamatwa na hivyo walikuwa na haki ya kupigania uhuru wao kwa namna yoyote
ile na hivyo uasi wao ulikuwa halali! Mahakama ikaruhusu Waafrika wale
kufanyiwa mipango ya kurudishwa kwao na fidia walipwe. Waafrika wale
hawakuhitaji kupewa elimu ya uraia kujua kuwa walikuwa wanadhulumiwa na wala
hawakuhitaji chama cha siasa kuwaongoza kukataa dhulma! Hawa
hawakuwa peke yao katika historia.
Uasi wa
Meermin wa Madagascar 1766
Japo uasi wa
Amistad unajulikana sana (labda kwa sahabu unahusisha Marekani) lakini uasi
mwingine wa Waafrika waliokataa kuchukuliwa watumwa ulifanyika miaka 73 nyuma
katika bahari ya Hindi. Meli ya Meermin ilikuwa nimojawapo ya meli za Waholanzi
zilizobeba watumwa na ilikuwa imebeba watu wa Malagasy ambao walikuwa waende
kuwa vibarua kwenye mashamba ya kampuni ya Dutch East India Company huko kwenye
jimbo la Cape Africa ya Kusini. Watumwa wale wakaamua kuasi na wakafanya uasi
mkubwa kwelikweli; waliua nusu ya wazungu waliokuwemo mle na kuagiza meli
igeuze njia kuwarudisha Madagascar. Kama ilivyokuwa kwa Amistad manahodha
wakatumia ulaghai na kuielekeza meli Afrika y a Kusini ambako ilitia nanga na
watumwa wale waliohadaiwa wakajikuta wanaangukia mikononi mwa watesi wao.
Maofisa wa
meli walishtakiwa na watumwa waliachiliwa isipokuwa viongozi wa uasi huo ambao
walijikuta wakitumikishwa katika Kisiwa cha Robben - ambapo miaka karibu mia
mbili baadaye mpigania haki za weusi Nelson Mandela naye alifungwa. Watumwa
hawa nao ambao kwa kiasi kikubwa historia imewasahau walijitambua kuwa wao ni
nani na hawakujali waliowakamata walikuwa ni kina nani au wana nguvu gani;
walitambua utu wao na walikuwa tayari kuupigania. Hawakuhitaji elimu ya uraia,
hawakuhitaji viongozi wenye elimu kubwa walichohitaji ni kujitambua kuwa ni
binadamu na hawakuwa tayari kuburuzwa, kudharauliwa, au kuteswa. Hawa nao
hawakuwa peke yao.
Uasi wa
Majimaji 1905
Miaka 139
baada ya uasi wa Wamalagasy kule Afrika ya Kusini na miaka 66 baada ya uasi wa
Amistad kule Uingereza Waafrika bado walijitambua utu wao na bado hawakutaka
kunyanyaswa, kudharauliwa, na kuteswa na watawala wao. Wananchi wa makabila
mbalimbali katika Tanganyika walijikusanya pamoja kuukataa utawala wa Mdachi
(Mjerumani). Kilichowafanya kuukataa utawala huu haikuwa kukataa rangi ya
Wadachi! Walikuwa wanakataa utawala wa mdachi juu yao.
Katika
kufanya hivyo waliamua kuasi; walinyanyaswa sana na waliteswa sana na
kudharauliwa katika nchi yao na walipofikia kikomo walisema inatosha na
wakaanza kujibu mashambulizi. Watawala waliwaita waasi, watawala walisema ni
wachochezi na wanaleta vurugu katika koloni lililokuwa limetulia na lenye
‘amani’. Watawala wakasema wamechoshwa na wakaja na sera ya kuwashambulia
mababu zetu; na kweli wengi walikufa mikononi mwa Wadachi! Nani atasahau
yaliyomkuta Chifu Mkwawa, au kina Mpambalioto na Nduna Songea?
Kuanzia
Umatumbi hadi Umatengo, Mahenge hadi Nachingwea, toka ghala za silaha za
Ifakara hadi ngome za Iringa; mto Rufiji hadi Mto Luwegu wazee wetu wakiwa
hawana zaidi cha kupoteza isipokuwa utu wao. Walisimama na kupigana na watu
waliowazidi kwa kila namna. Na kweli walishindwa, damu ilimwagika na watawala
waliamini kuwa wameweza. Lakini historia haikuwahurumia watawala wale kwani
miaka si chini ya kumi tu walijikuta wanapoteza koloni lao la thamani zaidi kwa
wababe wengine. Historia ina tabia mbaya sana ya kujirudia rudia, hasa
ukiidharau.
Hivi kuna
watu wanaamini wazee wetu walihitaji elimu ya uraia ili kujitambua? Hivi
walihitaji kusoma sana kujielewa kuwa utu wao ulikuwa unadharauliwa? Kwamba
wanahitaji wazungu waje kuwapa elimu ya kujitambua? Hivi kweli inahitaji usomi
kujijua unadhulumiwa, unadharauliwa, na kuwa unatawaliwa isivyo haki?
Kwa
kuhalalisha uhalifu wa vyombo vya dola Pinda amewapa wananchi haki ya
kujitetea! Alichokisema
Pinda ni kitu ambacho hakina jina jingine isipokuwa amehalalisha uhalifu
kufanywa na vyombo vya dola. Kama nilivyosema wakati ametoa ile kauli yake ya
kuhalalisha uhalifu mwingine dhidi ya watuhumiwa Pinda anastahili kujiuzulu
yeye mwenyewe ili kumpisha mtu mwingine mwenye hekima na uwezo wa kuongozza
wakati kuna pressure. Alichokifanya kwa upande mmoja ni kutoa kibali kwa Polisi
kuwapiga wananchi kwa sababu yoyote ile kwa kisingizio cha kuleta amani na
utulivu! Lakini amefanya kitu kingine; amewapa wananchi haki ya kujitetea
wakishambuliwa na Rais pasi ya haki.
Haki ya
Kujitetea ni Haki ya Msingi ya Mwanadamu
Mojawapo ya
haki ambazo labda hatujazizungumza sana na hazieleweeki ni haki ya kujitetea
(the right of self defence). Haki hii haijaleweka au haieleweki kwa wengi kwani
inachanganywa na kuonekana ni uhalifu. Mwanadamu anayo haki ya kulinda nafsi
yake na mali yake kutoka kwenye dhulma yoyote ile. Mara kwa mara haki hii
tunaitumia kwa njia za sheria - kama kwenda mahakamani au kumkamata mwizi.
Lakini inakuwaje kama jambazi amevamia familia yako na kuitishia maisha na wewe
una silaha? Je unaweza kutumia silaha kuitetea familia yako? Jibu ni ndiyo!
Hiyo ni haki yako na ukifanya hivyo kwa kujitetea maisha yako na ya familia
yako ni vigumu kwa mahakama kukuta una hatia isipokuwa kama inaonekana kwa
mfano, umeweza kumweka jambazi chini ya ulinzi na kumnyang’anya silaha halafu
kwa kisasi ukaamua kumuua! Hapo huwezi tena kujitetea ‘self-defense”.
Lakini
inakuwaje kama wanaokushambulia ni maafisa wa vyombo vya usalama? Je maafisa wa
vyombo vya usalama wakifuata agizo la Pinda wakakukufuza na kuanza kukupiga
bila kujaribu kukukamata au kukuletea mashtaka au si kwa ajili ya kukuweka
chini ya ulinzi unatakiwa kufanya nini? Je, polisi au wana usalama wanaweza
kuja nyumbani kwako na kukushambulia kwa vile wanakushuku wewe ni mkorofii kama
walivyofanya Mtwara je wewe nyumbani kwako una haki ya kujitetea?
Baadhi ya
watu ambao nimewasoma toka jana wanaamini kuwa serikali inaweza kupiga wananchi
wake na wananchi hawapaswi kujitetea! Kuna watu ambao ukiwasoma wanaamini
kabisa kuwa polisi na vyombo vya usalama vina haki na uwezo wa kuja na
kukuambia “bong’oa” na wewe unatakiwa ubong’oe kwa sababu unatakiwa ‘kutii
sheria bila shurti’! Wapo kabisa ambao wanaamini kabisa kuwa Mkuu wa Polisi
fulani anaweza kuja na nyota na mwenge wake na kukuambua “panua” na wewe
unatakiwa upanue tu kwa sababu yeye kasema! Kwamba wanaamini wananchi
hawatakiwi kuwabishia polisi, hawatakiwi kuwauliza na kwa hakika hawatakiwi
kuwapinga! Je hili ni kweli? Je ni kweli polisi wana nguvu hiyo katika maisha
ya watu wetu kiasi kwamba watu wetu wanatakiwa watii bila shurti!? Yaani, watii
lolote, popote, kwa lolote na vyovyote kwa vile wameamriwa hivyo?
Mifano
niliyotoa hapo juu inatupa jibu. Mwanadamu siyo mnyama ambaye anaweza kusukumwa
sukumwa au kunyanyaswa na watu wenye nguvu na madaraka. Mwanadamu ameumbwa na
dhamira na utu wake. Wapo wanadamu kati yetu ambao hawajali kunyanyaswa
alimradi wanaachwa na “amani”. Wapo kati yetu ambao utu wao kwao ni chakula cha
leo tu na ukiwapa chakula cha leo tu basi unaweza kuwafanyia lolote, popote, na
kwa lolote! Naam, wapo kati yetu ambao hawawezi kuhoji serikali yao, hawawezi
kuipinga, na kamwe hawatothubutu kulalamika kwa sababu wanaogopa au kuhofia
kuonekana siyo watiifu. Hawa wakiambiwa ‘inama’ wanainama, ‘inuka’, ‘lala’
wanalala na wakiambiwa ‘lia’ wanalia kama wameona mzimu! Hawa hawana namna ya
kuwasaidia kwani kila jamii inayo watu kama hao; watu ambao wanaabudu kwenye
altare ya watawala wa zama zao!
Wapo kati
yetu wanaojitambua
Lakini wapo
kati yetu ambao wanajitambua. Wanajitambua kama watumwa wa Amistad au wazee wa
Majimaji na kujiona kuwa na wao ni binadamu wenye kutaka kutambuliwa na
kuthaminiwa utu wao kama walivyofanya wale wa Malagasi. Wapo kati yetu ambao
wameamua kukataa watawala wa sasa, kuwapinga na kuwabishia; wamekataa kuendelea
kufukiza uvumba mbele zao. Watawala hawawapendi hawa na maneno ya Pinda
kimsingi yanawalenga hawa. Hawa hawatokubali kunyanyaswa na kudharauliwa na kwa
vile Pinda amewapa kibali vyombo vya dola kuwapiga wananchi basi wananchi nao
watakuwa wamejipa haki ya kujitetea dhidi ya polisi.
Hili si
jambo geni na mara nyingi ndio mwanzo wa machafuko makubwa ya nchi. Polisi
wanapoanza kutekeleza amri kama za Pinda wananchi nao wanaanza kutenda kwa
kujitetea na wanatangaza uadui na polisi na matokeo yake ni kuwa polisi
watakaojifanya ndio wa kwanza kupiga wananchi bila sababu watajikuta
wanarushiwa mawe na wao kuanza kupigwa. HIli likikitokea mimi sitoshangaa kwa
sababu Mwanadamu ana haki ya kujitetea. Huu mtindo wa polisi kwenda kwenye
nyumba za watu na kuanza kuwapa kipigo kutageuka kwani wananchi nao wataanza
kutetea nyumba zao na familia zao.
Pinda asije
kudhani kuwa serikali inaweza ikashindana na wanananchi wake. Ni kweli inaweza kuwa
na silaha nyingi na mbinu nyingi lakini wananchi wakiamua kujibizana na polisi
serikali itashindwa na itaanguka yenyewe. Ndiyo historia ilivyo. Pinda afute
kauli yake au aiweke vizuri. Akiiacha hivyo ilivyo kuwa polisi waanza kuwapiga
tu wananchi kwa sababu ati wao kina Pinda wamechoka ajue kabisa kuwa amewapa na
kibali wananchi haki ya kujitetea watakapoanza kupigwa.
Kwani nao
wananchi wamechoka vile vile!
Niandikie:
Mwanakijiji@jamiiforums.com
1 comment:
Kaka...I am reading this late at night and my eyes are getting big as I skim your long and detailed account. For now, I will say to you simply, yes. Kweli kabisa.
Will take the time to respond to you properly when I am rested. Bless you for reminding people of that history and those realities. Asante.
Post a Comment