Wasiliana nasi : chademadiaspora@gmail.com -Fair and Balanced Platform- Twitter @ChademaDiaspora

Wasiliana nasi : chademadiaspora@gmail.com -Fair and Balanced Platform- Twitter @ChademaDiaspora
----------------------WE THANK AND APPRECIATE YOU FOR VISITING CHADEMA DIASPORA BLOG. AGAIN, THANK YOU!-----------------------

Saturday, March 8, 2014

Kura ya siri bado moto Bunge la Katiba


  Utaratibu wa kupata uamuzi kuhusu kupitisha Rasimu ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 2013 kwa kupiga kura ya siri, uliozua mvutano mkubwa baina makundi mawili katika Bunge Maalumu la Katiba linaloendelea mjini hapa, umekuwa wa moto kuendelea kujadiliwa katika Bunge hilo. 
Suala lingine ni kuhusu hoja itakayowasilishwa na Kamati ya Uandishi katika Bunge Maalumu la Katiba, kuamuliwa kwa kuungwa mkono kwa wingi wa idadi ya theluthi mbili ya wajumbe wote kutoka Tanzania Bara na theluthi mbili ya idadi ya wajumbe wote wa Bunge hilo kutoka Zanzibar. Hali hiyo inatokana na semina ya wajumbe wa Bunge hilo kujadili vifungu vya Rasimu ya Kanuni za Bunge Maalumu ya Mwaka 2014 vinavyopendekeza utaratibu huo, kuahirishwa jana na Mwenyekiti wa muda wa Bunge hilo, Pandu Ameir Kificho, hadi leo. Vifungu hivyo, ni kuanzia cha 31 hadi 40 vya rasimu ya kanuni hizo. Uamuzi huo ulifikiwa na Kificho, ili kutoa fursa ya kufikiwa kwanza maridhiano ya pamoja baina ya makundi hayo nje ya Bunge.

         Katika kufikia maridhiano hayo, Kificho jana aliiagiza Kamati ya Mashauriano ya Kumshauri Mwenyekiti wa Muda, kukutana kwa niaba ya wajumbe wa Bunge hilo, ili kupata maridhiano, kabla ya semina ya kujadili na kuipitisha rasimu ya kanuni hizo kuendelea bungeni. Kamati hiyo iliyoundwa na Kificho yenye wajumbe 21 wa Bunge hilo kutoka vyama vya siasa na makundi mengine ya kijamii, wakiwamo viongozi wa dini, inaongozwa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda. Mbali na Pinda, wajumbe wengine wanaounda kamati hiyo ni Kificho, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Mahusiano na Uratibu, Stephen Wassira na Balozi Seif Ali Idd na Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), Balozi Seif Ali Idd. Wengine ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Mohamed Abood Mohamed; Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Vuai Ali Vuai; Profesa Costa Mahalu na Kingunge Ngombale-Mwiru. Wamo pia Dk. Tulia Ackson, Olive Luena, Fatma Himid Sadati, James Mbatia, Profesa Ibrahim Lipumba, Freeman Mbowe, John Cheyo, Sheikh Thabit Nouman Jongo na Askofu Donald Mtetemelwa.

    Semina hiyo ilianza Jumatano, wiki iliyopita, bungeni, iliahirishwa jana na Kificho ili kuipa kamati hiyo fursa ya kukutana jana saa 9.30 alasiri. Kificho alisema wakati akiahirisha semina hiyo bungeni jana kuwa baada ya kamati hiyo kukutana, kamati za uongozi za wajumbe wa vyama vya siasa na wale 201 walioteuliwa na Rais zingekutana baadaye kati ya saa 11 na saa 12 jioni. Alisema baada ya kukutana, kamati hiyo itatoa taarifa juu ya yaliyojiri katika kikao hicho. Kificho alisema pia makundi mengine, wakiwamo wajumbe wanaotoka vyama vya siasa, nao pia watapeana taarifa. “Kimsingi tuwe na mtazamo wa pamoja ili tuifanye kazi yetu kwa wepesi,” alisema Kificho. Akaongeza, “Pamoja na mivutano (iliyopo bungeni), ni lazima tupitishe kanuni hizi ili wiki ijayo tuanze kazi yetu baada ya Rais kulizindua Bunge,” alisema Kificho. Kundi la kwanza kati ya makundi mawili yanayovutana kuhusu vifungu hivyo, linaongozwa na CCM kupitia wajumbe, ambao ni wanachama wake waliomo kwenye Bunge hilo.

      La pili, linaundwa na wajumbe kutoka vyama vya upinzani, baadhi ya wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Baraza la Wawakilishi la Zanzibar, baadhi ya mashirika yasiyokuwa ya kiserikali na taasisi za kidini. Mvutano baina ya makundi hayo mawili, umedhihirika wakati wa mjadala wa rasimu ya kanuni hizo. Katika utaratibu wa upigaji kura, vifungu hivyo vinapendekeza kuwa baada ya Mwenyekiti wa Bunge Maalumu kutoa swali la kulihoji Bunge, itapigwa kura ya siri, ambayo itaitwa “kura ya mwisho.” Vifungu hivyo vinaeleza: “Kwa madhumuni ya Kanuni hii, utaratibu utakaotumika kupata uamuzi baada ya Mwenyekiti wa Bunge Maalumu kutoa swali la kulihoji Bunge Maalumu utakuwa ni wa kura ya siri.” “Bila kuathiri masharti ya Sheria na Kanuni hizi, wakati wa kupata uamuzi Bunge Maalumu kuhusu kupitisha Rasimu ya Katiba, Bunge Maalumu litapiga kura ya siri, ambayo kwa madhumuni ya Kanuni hii, itaitwa “kura ya mwisho.”

     Kundi la kwanza la wajumbe, wengi wakiwa ni wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wajumbe wa Baraza la Wawakilishi la Zanzibar kutoka CCM, baadhi ya viongozi wa dini na makundi ya kijamii, wanataka utaratibu utakaotumiwa na Bunge Maalumu kupata uamuzi uwe wa kura za wazi. Kundi la pili, linaloongozwa na vigogo wa vyama vya upinzani, wajumbe wengi kutoka makundi ya kijamii na baadhi ya viongozi wa dini na wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wakiwamo wachache wa CCM, wanataka utaratibu utakaotumiwa uwe wa kura za siri. Kuhusu hoja itakayowasilishwa na Kamati ya Uandishi katika Bunge Maalumu la Katiba kuamuliwa kwa kuungwa mkono kwa wingi wa idadi ya theluthi mbili ya wajumbe wote kutoka Tanzania Bara na theluthi mbili ya idadi ya wajumbe wote wa Bunge hilo kutoka Zanzibar, kundi moja linaloongozwa na wajumbe kutoka CCM linaupinga, badala yake linataka iwe nusu kwa nusu pande zote. Kundi la pili, linataka utaratibu huo uendelee kama unavyopendekezwa na kanuni hizo.


Said M./ Ippmedia/Nipashe

No comments: