Wasiliana nasi : chademadiaspora@gmail.com -Fair and Balanced Platform- Twitter @ChademaDiaspora

Wasiliana nasi : chademadiaspora@gmail.com -Fair and Balanced Platform- Twitter @ChademaDiaspora
----------------------WE THANK AND APPRECIATE YOU FOR VISITING CHADEMA DIASPORA BLOG. AGAIN, THANK YOU!-----------------------

Saturday, March 8, 2014

Katiba mpya sasa shakani

Vurugu Bunge la Katiba zasikitisha wengi
Latawaliwa na wanasiasa watunisha misuli 

   Baadhi ya wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba, wasomi, wanasiasa na viongozi wa dini, wamesikitishwa na vurugu zinazojitokeza kwenye bunge hilo maalumu na kuhofia kupatikana kwa katiba mpya kutokana na kuyumbishwa kwa mwenyekiti wa muda na kusababisha kuliahirisha kila wakati. Wakitoa maoni yao kwa kurejea vurugu za juzi, waliwaonya wabunge wasihamishie  vurugu za bunge la kawaida kwenye baraza hilo la katiba. Kadhalika wameonya kuwa upungufu unaojitokeza sasa ni  bunge hilo kutawaliwa na wanasiasa wanaotunisha misuli  wakipenda kushindana  huku wengine wakitafuta fursa kwenye uchaguzi mkuu mwakani.

VIONGOZI WA DINI WAZUNGUMZA

      Askofu Msaidizi wa Kanisa Katoliki Jimbo la Bukoba Mhashamu Methodius Kilaini, alisema kitendo cha wanasiasa kuliteka Bunge la Katiba kunawafanya wajumbe wengine waanze kuliogopa na kuwaachia walitawale. Aliwaonya  wajumbe hao wazoefu na kazi za bunge wasihamishie vurugu za bunge la kawaida kwenye Bunge Maalumu la Katiba. Alisema “baadhi ya wabunge wanatumia muda mwingi kutaka kuonyesha kuwa ni wazoefu na  ni miamba, jambo ambalo silo lililowapeleka bungeni.” Askofu Kilaini aliwataka wakubaliane kwa hoja kwa sababu muda unakwenda na kuna mambo mengi ya msingi hayajadiliwi. Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhad Mussa Sakum, alisema kinachoendelea bungeni kinasikitisha na kuleta na aibu. “Kikawaida Mungu alivyotuumba binadamu kuwaridhisha watu wote ni jambo lisilowezekana, kinachotakiwa ni watu kuvumiliana katika baadhi ya mambo ili kufanikisha kile tunachokifanya,” alisema Sheikh Sakum. Aliongezea kuwa: “Tunawaomba viongozi hao wavumiliane na waangalie maslahi ya nchi zaidi.” Pia aliwaomba viongozi wa dini mbalimbali  kuliombea bunge hilo limalizike kwa amani na salama kwani bila Mwenyezi Mungu hawataweza kutimiza lengo.

WANASIASA



        Mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba,  Profesa Mwesiga Baregu, alisema  hata kama kuna kanuni lazima kuwa na ratiba maalum ambayo itaonyesha jambo fulani linatakiwa kumalizika kwa muda gani na  kuwa na ratiba ya utendaji na kumaliza kazi. Aliwataka wajue kuwa muda lazima utawaliwe na nidhamu ili kufikia muafaka wa suala linalojadiliwa. Akizungumzia vurugu hizo, Mjumbe wa Bunge hilo ambaye pia na Mbunge wa Jimbo la Kawe, Halima Mdee, alisema ameshangazwa na uamuzi wa Mwenyekiti wa Muda wa bunge hilo, Pandu Ameir Kificho, kuahirisha kikao kutokana na makosa ya sekretariati ya bunge hilo. Alisema ni wiki ya tatu tangu  bunge hilo kuanza lakini hadi sasa  linajadili rasimu ya kanuni za kuongoza bunge hilo na hakuna jitihada za haraka za kumaliza na kuanza kazi mahususi iliyowapeleka Dodoma.

     "Tunalipwa fedha nyingi na Watanzania ili tuwafanyie kazi, matokeo yake mambo yanayoendelea hayaridhishi,  imefikia mahali watu wameacha kufuatilia mchakato wa katiba mpya," alisema. Alisema hali hiyo inawakatisha tamaa wananchi na kuona wajumbe hao wanatumia visivyo fedha zao na kushindwa kufikia lengo mahususi la kuwa na katiba bora itakayotibu matatizo ya msingi waliyonayo. Mjumbe mwingine James Mapalala, alisema palipo na mkusanyiko wa watu wengi hata kama ni watu wazima watageuka kuwa watoto. Alisema ni vyema kukawa na maafikiano ili kutengeneza katiba bora inayokidhi mahitaji ya matatizo ya Watanzania.

WASOMI WANENA



     Mhadhiri wa Sayansi za Siasa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Dk. Ally Bashiru, alisema bunge hilo la katiba limetawaliwa na wanasiasa ambao wanapenda kushindana  wengine wakitafuta jinsi ya kushinda uchaguzi mwakani. Alisema kasoro zinazojitokeza bungeni zipo ndani ya mchakato wa sheria na haiwezekani kupatikana katiba bora kwa sababu ya mchakato mbovu. “Tunayoyashuhudia ni matokeo ya kushindwa kuwa na mchakato bora wa ushirikishaji wananchi na tutaendelea kushuhudia mambo ambayo hatukuyategemea … kushikana mashati katika mchakato huo mbovu,” alionya “Haiwezekani kupata katiba bora kwa hali hii.” Aidha, alisema wananchi ndiyo wenye mamlaka ya kuwachagua wawakilishi wa kuingia kwenye bunge hilo kwa kuwapigia kura lakini si kwa  njia iliyotumiwa kuteua wawakilishi.

      Mhadhiri mwingine wa Sayansi za Siasa wa UDSM, Dk. Benson Bana, alisema CCM imechangia kwa asilimia kubwa kutokea vurugu bungeni kwani tayari wamekwenda na misimamo yao bila kuelewa wapo kwa maslahi ya wananchi na siyo chama. “Hilo ni bunge la wananchi si la CCM jambo hilo linaweza kuathiri bunge kwa asilimia kubwa kutokana na misimamo yao  jinsi walivyozungumzia muundo wa serikali tatu,” alisema Dk. Bana. Aliionya CCM isionyeshe ukomavu wao katika kuvuruga  mchakato wa katiba mpya kwa kuwa na misimamo yao isiyo na msingi.


 Swedi M. , Shayo B., & Kitomari S.,   Dar/Dodoma

No comments: