Uchaguzi wa 2010
Katika uchaguzi wa 2010 ambapo mgombea wa CCM marehemu Dr. William Mgimwa aliibuka kidedea ukiziangalia namba utaona zinatisha. Dr. Mgimwa alipata kura 31,421 wakati mgombea aliyemfuatia kutoka CDM Rehema Paulo Makoga alipata kura 3356. Huu ni uwiano wa karibu 1:10 ya wapiga kura; yaani kwa kila kura 10 zilizoenda kwa Mgimwa mpinzani wake alipata kura moja. Ni uwiano mpana sana hasa ukingatia mwamko uliokuwepo wakati wa kuelekea uchaguzi mkuu na zaidi mwamko uliokuwepo kwenye jimbo la karibu la Iringa mjini ambapo CDM walikuwa wanakubalika sana.
Bila ya shaka watu wengi walijiandikisha kupiga kura na wale waliojitokeza kupiga kura walikuwa ni wengi vile vile. Lakini ushindi huo mkubwa kwa Dr. Mgimwa unaweza kuelezewa kuwa ni ama wana Kalenga walimkubali yeye binafsi zaidi au walikikubali chama chake zaidi kiasi kwamba hata kama kingemsimamisha mtu mwingine basi angeendelea kushinda kwa kishindo. Hili la pili hata hivyo ni gumu kulikubali kama tutaamua kuangalia kura za mwaka 2005.
Uchaguzi wa 2005
Katika uchaguzi wa 2005 namba zinatuonesha kitu tofauti kidogo na tunaweza kusema tu kuwa hizi ndizo namba ambazo tunahitaji kuziangalia sana kwani zinaweza kabisa kuamua ni nani ataibuka kidedea katika kinyang’anyiro hicho ambacho kama vingine vya karibu tayari kimeshanyunyizia damu katika ardhi ya Kalenga.
Mwaka 2005 CCM ilishinda jimbo la Kalenga chini ya mgombea wake Stephen Galinoma aliibuka na ushindi wa kura 32,734 wakati mpinzani wake kutoka chama cha Jahazi Asilia Grace Tendega alipata kura 13, 492. Hapa inatupasa tuangalie kwa karibu mambo fulani; kwanza, ukilinganisha namba za CCM kati ya 2005 na 2010 utaona kuwa tofauti ya watu waliomchagua mgombea wa CCM ni kura 1300 hivi. Kama hili ni kweli – na namba hazisemi uongo – CCM haikuona tofauti kubwa sana kwa wagombea wake hata baada baada ya miaka mitano licha ya upinzani kusimamisha wagombea tofauti.
Je yawezekana namba hizi zikajirudia tena kwenye uchaguzi mdogo? Kwa vile hakujafanyika uandikishaji wapiga kura wapya yawezekana CCM bado ikapata karibu kidogo ya wapiga kura hawa tena – hata kama ni kufikia kama 25,000 hivi? Hili linawezekana si geni sana kwani tumeona lilijitokeza miaka kadhaa huko nyuma na mfano mzuri ni kuangalia uchaguzi mdogo wa Kiteto wa 2008 ambao ulifanyika baada ya mbunge wa jimbo hilo kufariki dunia. Japo CCM walipunguza kura zao lakini bado CDM ilijikuta na yenyewe imepunguza kura kulinganisha na ilizopata 2005. Bila ya shaka kuna mambo mengine mengi yalitokea wakati ule mambo ambayo pia tunaona yakijirudia Kalenga na sehemu nyingine – vurugu, umwagikaji damu, matumizi ya vyombo vya dola na kutumika kwa watumishi wa serikali kufanya kazi za siasa.
Kwa hiyo kama hili linaweza kuangaliwa vizuri basi kibarua cha CDM kushinda Kalenga ni kigumu zaidi kuliko watu wanavyojiaminisha au kufikiria. Mfano wa Arumeru Mashariki nao unapaswa kuangaliwa kwani tangu uchaguzi wa 2005 kulikuwa na mwamko wa kuikataa CCM huko na hatimaye kwenye uchaguzi mdogo Joshua Nassari aliweza kumbwaga Siyoi Sumari ambaye baba yake alishikilia jimbo kabla na ambaye alimwangusha Joshua kwenye uchaguzi mkuu wa 2010. Kushinda kwa Joshua Nassari ni wazi hakukutokana na kampeni tu ya wakati wa uchaguzi mdogo bali pia kulichangiwa na kufanya kwake vizuri katika uchaguzi wa 2010 ambapo ukilinganisha na kura za CCM 2005 utaona kuwa wimbi la mabadiliko liliikumba Arumeru Mashariki na bila ya shaka wakivuna upepo wa kuikataa CCM uliotokea Arusha Mjini chini ya Godbless Lema ambaye alipambana na mbingu na ardhi ya nguvu za CCM jijini hapo.
CDM inaweza kuiangusha CCM
Tukiangalia yote haya tunaweza kuona pasi ya shaka kuwa kila jimbo lina mambo yake (dynamics) ambayo yanaweza kuchangia ushindi au kushindwa kwa CDM. Kwa maoni yangu uwezekano wa CCM kuanguka Kalenga ni mkubwa kwa sababu kadhaa licha ya namba kuonekana kuwa upande wake zaidi.
1. Mgombea wa CDM anakubalika zaidi sasa kuliko aliyesimamishwa 2010 au 2005. Huyu si mwingine ila ni Bi. Grace Tendega. Ikumbukwe kuwa Tendega alisimamishwa na Jahazi Asilia 2005 na kufanya vizuri zaidi na Jahazi Asilia ilipomsimamisha mtu mwingine mwaka 2010 mtu huyu hakufanya vizuri sana kama Tendega miaka mitano nyuma. Hili linatuambia jambo moja kubwa; Bi. Tendega anakubalika sana jimboni hapo.
2. Kusimamishwa kwa mtoto wa Mgimwa ambaye hana rekodi yoyote ile ya kusimamia isipokuwa jina la baba yake yaweza kuwa ni kosa lile lile lililofanywa na CCM Arumeru Mashariki. Bila ya shaka itakuwa tofauti Chalinze ambapo mtoto wa Rais anagombea. Watu wa Kalenga kama wa Arumeru Mashariki wanaweza kuona – na siwezi kushangaa – kuwa CCM imeonesha dharau ya aina fulani hivi; kwamba badala ya kumsimamisha mtu ambaye anaweza kweli kushinda kwa tiketi ya CCM wakaona ni bora wamsimamisha mtoto aliyekuwa Mbunge wakitegemea kuwa kura zile za 2010 zitamuinua na mtoto vile vile. Kama watu wa Kalenga walivyo huru kama walivyojionesha huko nyuma uwezekano wa kukataa dharau hiyo unaweza kujitokeza Jumapili.
3. Upepo wa Mabadiliko kutoka Iringa mjini; uzuri mmoja wa majimbo yaliyo karibu na miji mikubwa ni kuwa mwamko wa kisiasa – kwa uzuri au kwa ubaya – unafika hadi pembezoni. Hili tumeliona Mwanza, tumeliona Arusha, Kigoma, Moshi n.k Je laweza kuwa kweli hata Kalenga? Napendekeza kwa msomaji kuwa kama wananchi wa Kalenga ni wafuatiliaji wa karibu wa siasa za mkoa wao bila ya shaka wanajua ni kitu gani kinapiganiwa; siyo sifa, siyo ujiko, wala siyo ajira. Kinachopiganiwa ni maisha yao na hasa hatima ya maisha yao. Wakavyochagua kuongozwa ndivyo watakavyoongozwa!
4. Harakati za kampeni isiyoonekana; mojawapo ya sababu kubwa zinazoweza kuchangia CDM kuibwaga CCM ni kampeni ambayo inaongozwa na mmojawapo wa wanasiasa machachari na naweza kumuita “Kamanda wa Vijiji” Bw. Alfonce Mawazo. Sitasema mengi hapa lakini itoshe kusema tu kuwa ni miongoni mwa wanasiasa ambao binafsi nawahusudu sana kwa mikakati, uthubutu na mitindo yao ya kuishambulia CCM kijiji kwa kijiji. CDM ikishinda Kalenga itakuwa ina deni kubwa sana kwa kijana huyu na timu anayoiongoza huko.
5. CCM imefanya kosa kumsimamisha Godfrey Mgimwa. Kosa hili wanaweza kulilipia vilivyo.
Pamoja na ukweli huo, bado kibarua cha CDM Kalenga kigumu; na ugumu wake unatokana na ukweli mwingine mmoja ambao tunautambua wazi; CCM bado ina mbinu na uzoefu wa kushinda hata sehemu ngumu kweli. CCM ikiongozwa na wanasiasa wake machachari inachohitaji kufanya huko Kalenga ni uminyaji upigaji kura; kwamba kwa namna fulani watu watakaopiga kura wawe wachache sana kulinganisha na 2010 au 2005. Kama nilivyotabiri kuelekea uchaguzi mkuu wa 2010; endapo watu wengi hawatajitokeza kupiga kura basi CCM itashinda vivyo hivyo itakavyokuwa Kalenga. Kama wapiga kura watakuwa chini ya 20,000 CCM itashinda; kukiwa na wapiga kura zaidi ya hivyo au karibu ya kuelekea 27,000 CDM itashinda kwa tofauti nzuri tu ya kura. Nasubiri kusahihishwa.
No comments:
Post a Comment