Pamoja na Bunge Maalumu la Katiba kupitisha kanuni zote 87 za uendeshaji wake, bado kuna sintofahamu miongoni mwa wananchi kuhusu nini kilikubaliwa katika utaratibu wa upigaji wa kura. Mkanganyiko huo unatokana na wingu zito lililokuwa limetanda kwa takribani wiki tatu, huku wajumbe wakivutana juu ya aina ya kura itakayotumika katika kupitisha vifungu vya Rasimu ya Katiba. Mvutano huo unatokana na wajumbe wa CCM kutaka kura ya wazi na wale wa makundi mengine kutaka kura ya siri. Kanuni zilizoibua mvutano mkubwa na kutishia kuvunjika kwa Bunge Maalumu la Katiba, ni ya 37 na 38 ambazo wajumbe wa Kamati ya Kanuni, walikuwa wamependekeza utaratibu wa kupiga kura ya siri katika kupitisha uamuzi.
Mapendekezo hayo yalikabiliwa na upinzani mkubwa kutoka kwa wajumbe walioshikiliwa msimamo wa kura ya wazi wakati vyama vya upinzani na makundi mengine, wakitaka kura ya siri. Mkazi mmoja wa mjini Moshi, Patricia Temu, alimpigia simu mwandishi wa gazeti hili juzi akihoji kuwa Bunge limepitisha utaratibu gani kati ya kura ya siri ama ya wazi kwa sababu maelezo yaliyotolewa yamewachanganya watu. Mbali na Temu, mkazi mwingine wa Morogoro, Benard Senyael alisema yuko katikati ya ubishani na watu wengine. Alisema wananchi wengi wanaamini kuwa utaratibu uliopita ni wa kura ya wazi. “Hapa nilipo nina watu wengi wamenizunguka wanabishana wanasema Bunge limepitisha utaratibu wa kura ya wazi kwani nini hasa kilipitishwa,” alihoji.
Ingawa alielezwa kuwa hakuna utaratibu uliotangazwa, Senyale alisema suala hilo linachanganya. “Sasa hiyo ndio nini. Wanapitishaje kanuni inayoishia kusema utaratibu utakuwa ni wa kura, ilipaswa kanuni iseme ni kura ipi ya wazi ama ya siri. Hapa naona wamechemsha.” Suala la mfumo wa kura limepangwa kuamuliwa wakati wajumbe watakapoanza kupigia kura vifungu vya Katiba.
Mjema D./ Mwananchi
No comments:
Post a Comment