Ratiba ya Bunge
Maalum la Katiba, imevurugika baada ya suala la Rasimu ya Kanuni za kuendesha
Bunge hilo kuchukua muda mrefu kukamilika na sasa haijulikani Bunge hilo
litazinduliwa lini ikiwamo kuapishwa kwa wajumbe hao.
Ratiba ya awali
iliyotolewa na Ofisi ya Bunge ilionyesha kuwa Februari 16 na 17, mwaka huu, ni
kuwasili na usajili wa wajumbe wa Bunge hilo, na mkutano kuanza Februari 18 kwa
kuanza kupata maelekezo ya ukaaji na jiografia ya ukumbi.
Pia, kusomwa kwa
tangazo la kuitisha Bunge Maalum, uchaguzi wa Mwenyekiti wa muda, kuandaa na
kupitisha Kanuni za Bunge Maalum.
Februari 19 na 20, kikao cha kazi ya kuandaa
rasimu ya kanuni za Bunge Maalum, Februari 21, kupitisha Azimio la kuridhia
kanuni za Bunge, uchaguzi wa Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti, kiapo cha Katibu
na Naibu Katibu wa Bunge.
Februari 21 ilikuwa ni kiapo kwa Mwenyekiti na
Makamu Mwenyekiti na Februari 22 kiapo cha wajumbe wa Bunge, na Februari
24 hadi 30 ufunguzi rasmi wa Bunge, uwasilishaji wa Rasimu ya Katiba kwenye
Bunge, mjadala wa kupitisha Rasimu ya Katiba kadiri kanuni zitakavyoainishwa.
Hata
hivyo, kilichofanyika hadi juzi kabla ya kuahirishwa hadi leo ni uchaguzi wa
Mwenyekiti wa muda na kuwasilishwa kwa rasimu ya kanuni na sheria ya mabadiliko
ya Katiba na wajumbe kukabidhiwa na kupewa muda wa kuzisoma huku kamati ya
kanuni ikichambua kanuni hizo na itaziwasilisha leo.
Mwenyekiti wa muda, Pandu
Ameir Kificho, alisema juzi kuwa Kamati ya Kanuni imeomba siku mbili
kukamilisha kazi na leo na kesho wajumbe watakuwa kwenye kikao kazi cha kupitia
kanuni na uchambuzi wake.
Ijumaa azimio la kuridhia kanuni za Bunge
litapitishwa katika kikao cha Bunge hilo.
Hata hivyo, haijajulikana lini
Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti, Katibu na Naibu Katibu wa kudumu
watapatikana, kuapishwa kwa wajumbe, uzinduzi wa Bunge na kuwasilishwa kwa
rasimu.
Kitomary N./ Ippmedia-Nipashe
No comments:
Post a Comment