Wizara ya Elimu na
Mafunzo ya Ufundi imetupiwa lawama kwa kuruhusu upangaji wa madaraja ya
mitihani ya kidato cha nne unaozua utata na kuwa na dalili za kuzika elimu
nchini.
Akizungumza na NIPASHE jijini Dar es Salaam jana, Katibu wa Shirikisho
la Wamiliki na Mameneja wa Shule Binafsi na Vyuo Visivyo vya Kiserikali
(Tamongso), Benjamin Nkonya, ameiambia NIPASHE kuwa upangaji wa madaraja
uliofanywa na Necta utaligharimu taifa kwa kiasi kikubwa kwani unaangamiza elimu
badala ya kuiinua.
Nkonya alisema kuwa madaraja hayo mapya yaliyotumika katika
kutangaza matokeo ya mtihani uliopita ya kidato cha nne yanaonekana kuwa na nia
ya kuuonyesha umma kuwa watahiniwa wameanza kufanya vizuri zaidi na kujenga
dhana kuwa kiwango cha elimu kinapanda kwavile imepanua wigo wa ufaulu bila
kuzingatia haja ya kuboresha maeneo muhimu kama ya uandaaji wa mitaala sahihi
na kuboresha mazingira ya utoaji wa elimu yenyewe.
Alisema kuwa wao
(Tamongso), walishapinga mara kadhaa utaratibu huo uliotumika sasa lakini
wanashangaa kuona kuwa bado serikali kupitia Baraza la Mitihani la Taifa
(Necta) ikitumia madaraja yaleyale waliyokuwa wakiyapinga kila mara.
"Kwa
mfano, sisi tulipendekeza alama za ufaulu zianzie angalau alama 35 hadi 50 kwa
daraja la nne... wanaopata chini ya hapo watafutiwe utaratibu mwingine ikiwa ni
pamoja na kuwapeleka kwenye vyuo vya ufundi. Lakini hilo halijazingatiwa na
kilichopo sasa, ni siasa tupu katika elimu ambayo mwishowe itaua elimu,"
alisema Nkonya.
Mbunge wa kuteuliwa, James Mbatia, amesema matokeo ya kidato
cha nne yaliyotangazwa hivi karibuni ni danganya toto na kama siyo serikali
kupandisha madaraja, yangekuwa mabaya kuliko ya mwaka jana kwani wengi
waliofaulu, wakifuatilia kiundani ni sawa na wamefeli.
Alisema matokeo hayo ni
kucheza na akili za Watanzania hususan walala hoi kwa kuwa katika shule za
serikali ambazo kwa sasa zimegeuziwa kisogo, hakuna mtoto wa kiongozi au
mtumishi wa umma mwenye kipato cha kati anayesoma huko.
Mbunge wa Ubungo, John
Mnyika ameitaka serikali kuboresha mazingira ya kutolea elimu ili kuinua
kiwango na siyo kwa njia hii ya kubadili madaraja kwa namna inayotia shaka
kwani huko ni kuangamiza elimu nchini.
"Serikali kwa barakoa (veil) ya
kutekeleza Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (Big Results Now) imeamua kulificha
taifa juu ya Matokeo Mabaya ya Sasa (Bad Results of Now). Hivyo, wachambuzi
wa masuala ya elimu wanapaswa kutoa takwimu za matokeo yangekuwa namna gani
iwapo viwango vya awali vya ufaulu vingetumika ili nchi ijue hali halisi kwa
manufaa ya wananchi," alisema Mnyika.
UTATA
Uchunguzi uliofanywa
na NIPASHE kupitia matokeo yaliyotangazwa mwishoni mwa wiki umebaini kuwa mbali
na wizara hiyo kushusha sana alama za ufaulu na hivyo kupunguza pia idadi ya
watahiniwa waliofeli kutoka asilimia 56.92 ambayo ni sawa na wanafunzi 210,846
mwaka 2012 hadi kufikia asilimia 42.91 (wanafunzi 151,187), bado kumekuwa na
matokeo yenye utata, hasa katika vigezo vya kuwapanga waliopata daraja sifuri
na wale waliofaulu kwa kiwango cha walau daraja la nne.
Katika baadhi ya
shule, NIPASHE imebaini kuwa matokeo hayo yamewachanganya watahiniwa kwa kiasi
kikubwa, yakionyesha kuwa baadhi yao wamefeli kwa daraja sifuri licha ya kupata
alama za jumla walizoamini kuwa zingewaweka katika kundi la waliofaulu kwa
kiwango cha daraja la nne.
Aidha, wengine wamejikuta wakichanganywa pia na
matokeo ya wenzao wanaoonekana kupata alama za jumla za chini zaidi lakini bado
wakipewa daraja la nne.
Miongoni mwa matokeo hayo ya utata yanaonekana katika
Shule ya Sekondari Wigamba iliyopo Mbeya mjini na pia katika Shule ya Sekondari
Dr. Nchimbi, hasa tofauti ya alama kati ya madaraja ya nne na sifuri. Baadhi ya
wanafunzi katika shule hizo wanaonekana kufeli vibaya kwa kupata daraja la
sifuri, licha ya jumla ya alama walizopata kuonyesha kuwa ni 42.
Kwa mujibu wa
upangaji mpya wa madaraja wa NECTA, daraja la sifuri huanzia alama 47 hadi 49
huku daraja la nne likiwa ni kwa ajili ya watahiniwa waliopata jumla ya alama
zinazoanzia 32 hadi 46.
Katika shule ya Wigamba, mtahiniwa mvulana mwenye
namba S3133/0054 anaonekana akiwa amepata daraja la sifuri licha ya kupata
alama 43. Huyu amepata D ya English na E za masomo ya Civics, Kiswahili na
Biology huku akiwa amefeli kwa kupata F katika masomo mawili ya Historia na
Hisabati.
Hata hivyo, mtahiniwa mwingine katika shule hiyo hiyo ya Wigamba,
mwenye namba S.3133/0010 amefaulu kwa kupata daraja la nne licha ya kwamba
jumla ya alama zake kuwa 44, moja zaidi ya mtahiniwa S.3133/0054 aliyepata
sifuri. Mwingine aliyepata sifuri licha ya kupata alama 42 ni mtahiniwa mwenye
namba S.3133/0092 wakati mwenzake mwenye namba S.3133/0100 akifaulu kwa kiwango
cha daraja la nne licha ya alama zake kuwa sawa na yeye ambazo ni 42.
Mifano
mingine inayoashiria utata au kutoeleweka wazi kwa mfumo mpya wa madaraja ni
pamoja na matokeo ya mtahiniwa mwenye namba S.1877/0007 wa Shule ya Sekondari
ya Dr. Nchimbi. Huyu anaonekana kufaulu kwa kupata daraja la nne licha ya kuwa
na pointi 46, akipata C ya Kiswahili na F za masomo sita ya Civics, History,
Geography, English, Chemistry, Biology na Basic Maths.
Mtahiniwa mwenye namba
S1877/0006 wa Shule ya Sekondari Dr. Nchimbi pia anaonekana kupata daraja la
nne licha ya kuwa na alama 46 wakati mwanafunzi mwingine wa shule hiyo hiyo,
mwenye namba S1877/0170 akifeli kwa kupata daraja sifuri licha ya kuwa na alama
46 kama mwenzake mwenye namba S1877/0006.
Kwa mujibu wa NECTA, madaraja
mapya yaliyotumika sasa yanaonyesha kuwa sawa na yale yaliyowahi kutangazwa na
Profesa Sifuni Mchome na kupingwa na baadhi ya wabunge ambayo ni daraja la
kwanza lililiobaki vilevile kuanzia alama za jumla 7 hadi 17, daraja la pili
likibadilika kutoka 18-21 hadi 18-24, daraja la tatu kuwa 25-31 badala ya 22-25
; daraja la nne kubadilika kutoka 26-32 na kuwa 32-46 huku daraja sifuri likiwa
47 hadi 49.
Aidha, katika utaratibu wa sasa, A huanzia 75-100; B+ ni 60-74; B
ni 50-59 wakati C ni alama kuanzia 40 hadi 49. Mgawanyo mwingine unaonyesha
kuwa D huhusisha alama kati ya 30 hadi 39, E ni 20 hadi 29 na F huhusisha
ufaulu wa alama 0-19.
Hata hivyo, ilitarajiwa kuwa kutokana na mabadiliko
hayo, wale waliopata alama za jumla kuanzia 32 hadi 46 wangekuwamo katika
orodha ya waliofaulu kwa kiwango cha daraja la nne na siyo sifuri.
NECTA YAFAFANUA
Akizungumzia kuhusu utata wa madaraja, Afisa Uhusiano
wa Necta, John Nchimbi, aliiambia NIPASHE jana kuwa ufaulu wa daraja la nne
hautegemei alama za jumla peke yake bali ni pamoja na sharti lake kuu ambalo ni
lazima kila mtahiniwa awe amepata angalau D mbili na C moja.
Aliongeza kuwa
kifungu cha 20 (6) cha Kanuni za Mitihani ndicho kinachoeleza wazi kuhusu
vigezo vya ufaulu wa daraja la nne ambavyo ni pamoja na ulazima wa kufaulu kwa
kiwango cha C au D mbili na siyo wingi wa alama.
Alieleza dhana nyingine za
madaraja hayo mapya kuwa ni pamoja na kuangalia viwango vya ufaulu, kuanzia A
hadi F ya makundi ya alama ambazo watahiniwa wamezipata; hilo likiambatana na
mabadiliko yaliyopanua wigo kutoka makundi matano yaliyozoeleka awali (A, B, C,
D NA F) hadi kufikia makundi saba ya A, B+, B, C, D, E na F.
Akitoa mfano,
Nchimbi alisema kuwa mtahiniwa mwenye alama 42 anaweza kuwamo katika kundi la
waliofeli kwa kupata daraja sifuri ikiwa atakosa sifa ya kuwa na walau C moja
au D mbili.
Aidha, alieleza mazingira yanayoweza kumfanya mtahiniwa apate daraja
la nne licha ya kuwa na jumla ya alama 46 kuwa ni pamoja na kupata C na kisha
masomo sita kati ya saba yanayohesabiwa akawa amefeli yote kwa kupata F.
Hata hivyo, haikufahamika mara moja kama wanafunzi wote waliofanya mtihani
huo walishajulishwa juu ya upangaji huo mpya wa madaraja na kufanya mazoezi
kupitia mitihani yao ya majaribio maarufu kama 'mock' na pia mitihani ya
kawaida ambayo kidato cha nne huifanya wakati wote wanapojipima kwa maandalizi
ya mtihani wa taifa.
BUNGE
Licha ya Necta kutoa ufafanuzi huo kuhusu
madaraja, NIPASHE inatambua kuwa uamuzi wa baraza hilo umekiuka mapendekezo
kadhaa ya wabunge wakati wakijadili kadhia ya matokeo mabaya ya mitihani ya
kidato cha nne mwanzoni mwa mwaka 2012.
Katika majadiliano yao, wabunge wengi
walipinga mapendekezo kadhaa ya kuwapo kwa madaraja mapya likiwamo la daraja la
tano lililotangazwa awali mbele ya waandishi wa habari na Katibu Mkuu wa Wizara
ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Mchome kabla serikali kumkana bungeni
kupitia kauli iliyotolewa na aliyekuwa Naibu Waziri, Philip Mulugo, akisema
kuwa hakuna daraja la tano na kwamba, daraja sifuri lililotangazwa kufutwa na
Mchome linabaki palepale.
Matokeo yaliyotangazwa mwishoni mwa wiki na Kaimu
Katibu wa Necta, Dk. Charles Msonde yalionyesha kuwa kwa ujumla, ufaulu
umeongezeka kwa asilimia 15.17 kulinganisha na mwaka 2012, matokeo ambayo
baadhi ya wadau wameyakosoa vikali.
Ippmedia/Nipashe
No comments:
Post a Comment