Wakati Bunge Maalum
la Katiba likikutana kwa takribani nusu saa tu jana huku wajumbe wakiendelea
kulipwa mamilioni ya fedha za kodi za wananchi, baadhi ya wajumbe wamelalamika na kupinga hali ya kuendelea kuahirisha vikao kwa kuwa hatua hiyo
inasababisha matumizi makubwa ya fedha za umma na muda.
Bunge hilo limekuwa
likiahirishwa tangu kuanza Jumanne iliyopita kwa ajili ya kutoa nafasi kwa
wajumbe kuzisoma kanuni pamoja na Kamati ya Kanuni kukamilisha kazi ya
kuzichambua na kuwasilisha mbele ya wajumbe hao kwa ajili ya kuzijadili na
kuzipitisha, kabla ya kuanza kujadili Rasimu ya Katiba.
Wajumbe hao walitoa
madai hayo jana baada ya kikao hicho kufanyika kwa nusu saa na kuhairishwa
wakidai kuwa huko ni kupoteza muda na rasilimali za Watanzania bila
sababu ya msingi.
Jana wajumbe takribani 629 waliokwisharipoti waliingia
katika kikao kilichodumu kwa nusu saa kuanzia saa 3:00 asuhuhi hadi saa 3:30 na
kuahirishwa. Kutokana na kila mjumbe kulipwa posho ya kikao ya Sh. 220,000 kwa
siku, jana kwa dakika 30 zilitumika takribani Sh. 128,920,000 zilitumika
kuwalipa wajumbe hao.
Baada ya Mwenyekiti wa muda wa Bunge hilo, Ameir Pandu
Kificho, kutoa taarifa ya kuahirishwa kwa kikao hicho, Ezekia Oluoch kutoka
Vyama vya Wafanyakazi, alishauri siku mbili ambazo kamati itakuwa inaendelea na
kazi
ya kuchambua kanuni, wajumbe waendelee na kazi ya kuijadili Rasimu ya Kanuni na
maoni yapelekwe kwenye Kamati.
Akizungumza na waandishi wa habari nje ya
ukumbi bunge, Oluoch alisema
anashangazwa na uamuzi huo kwa kuwa unapoteza
rasilimali na muda kwa kuwa tangu bunge hilo lianze Februari 18 mwaka huu
hakuna jambo la msingi lililofanyika.
“Tungeambiwa hivi wala tusingewahi
asubuhi, sasa tunaambiwa hadi Jumatano, siku zote hizi mbili tunafanya nini
hapa Dodoma, ni matumizi
mabaya ya muda na rasilimali za Watanzania ambao ndiyo
wanatulipa tunavyokuwa hapa,” alisisitiza.
Profesa Sospeter Muhongo alisema
anashangaa kazi hiyo kushindwa kukamilika kwa siku hizo wakati walikuwa na
mwongozo wa Rasimu ya Kanuni.
“Tusipokuwa waangalifu kuzingatia muda hii kazi
haitaisha, kwa hiyo tukubaliane kwamba muda uliopangwa ukimalizika hakuna muda
wa nyongeza kwa maelezo kwamba hawajamaliza, wananchi wanavyotuona tunaweza
kujifurahisa tunafanya vitu vya maana sana, lakini watu wanatushangaa, kama
kamati haiwezi unaitoa tunaendelea mbele,” alisema Profesa Muhongo ambaye pia
ni Mbunge wa Kuteuliwa na Waziri wa Nishati na Madini.
Mjumbe mwingine, James
Mbatia, alisema kanuni hizo ni ngumu na zimetengenezwa kama kanuni za kudumu za
Bunge, jambo ambalo litawafanya wajumbe wengine washindwe kuzitumia.
“Fikiria
mvuvi wa Muleba au Mwanza au mkulima ambaye hana uzoefu na mambo ya kibunge,
hizi kanuni zinavyotengenezwa ni ngumu inaonyesha zinanakiliwa na kubandikwa
wakifuata zile Kanuni za Kudumu za Bunge,” alisema na kuongeza:
“Huu ni mkutano
wa siku 70 na si bunge la kudumu. Zingepaswa ziwe kwenye karatasi mbili au tatu
kwa kuwa tupo hapa kwa tendo la Katiba ambalo ni maridhiano.”
Alisema wabunge
waliozizoea kanuni na ukumbi huo bado zinawasumbua, kwa mtu ambaye amekuja mara
ya kwanza anawekewa masharti ya uvaaji ikiwamo kuvaa suti na kwamba tatizo
kubwa lipo kwenye muundo wa Bunge lenyewe kwa kuwa wengi wa wajumbe wanatokana
na Wabunge na Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar.
Alisema Katiba si kwa
ajili ya kizazi hiki bali vizazi vya miaka 100 ijayo, na kwamba mambo yanakuwa
magumu kwa kuwa yanazungumzwa masuala ya nchi mbili kwa wakati moja.
Alisema
mkutano huo ni wa siku 70 na ni sawa na mkutano wa kawaida, hivyo huwezi
kutengeneza kanuni kama kanuni za kudumu kama mtu anayeandaa kanuni
zitakazotumika kwa miaka 20 ijayo.
“Ni kanuni ngumu sana na zinachanganya,
wanasahau kuwa Katiba ni suala la maridhiano, Bunge la Nepal lilitumia siku 90
kutengeneza Kanuni.
Ukishakosea kwenye kanuni ndiyo basi, hizi zilitengenezwa
na sekretarieti ambazo siyo wajumbe wa Bunge, zinapaswa kutokana nawajumbe
wenyewe iwe ya kurasa mbili au tatu,” alisema.
Alisema kwa mwendo huo haoni
dalili za Bunge hilo kuanza wiki hii wala ijayo na kwamba Watanzania wasikubali
kuondoshwa kwenye hoja ya msingi na kupelekwa kwenye suala la posho.
Aidha,
alikosoa kanuni hizo na kudai kuwa zimetengenezwa kwa hofu ya watawala na
kwamba kuweka kanuni ya kumtoa nje mjumbe kwa siku kumi kwa Bunge la siku 70 ni
ajenda isiyo na lengo jema.
Ally Kessy, ambaye pia ni Mbunge wa Nkasi
Kaskazini (CCM), alisema kuahirishwa kwa vikao vya bunge tangu wiki iliyopita
kwa madai kwamba wajumbe wanahitaji muda wa kutosha kusoma Rasimu hiyo ni
kupoteza bure fedha za wananchi.
Mbunge wa Jimbo la Kasulu Mjini, Moses
Machali (NCCR-Mageuzi), alisema haoni sababu ya bunge hilo kuahirisha vikao kwa
hoja ya kutoa muda wa kutosha kwa wabunge kusoma vya Rasimu ya Kanuni.
“Haina
sababu, busara inakosekana, Mwenyekiti wa Muda alikwishaunda kamati ya wajumbe
20 ya kumshauri, kwa nini sasa hali hii inaendelea kuwa hivi?” alihoji.
Alisema
kwa upande wake ameisoma Rasimu hiyo kwa siku mbili tu na kuielewa, hivyo haoni
kwa nini wajumbe wahitaji siku nyingi kuisoma na kuielewa.
Naye Mjumbe kutoka
kundi la Vyama vya Wavuvi Zanzibar, Issa Ameir Suleiman, alisema: “Sisi tunaona
hawatundei haki, lengo letu lilikuwa kuja na kufanya kazi moja kwa moja, lakini
sasa tunaingia wiki ya pili bado hatujaanza kujadili Rasimu ya Katiba.”
Halima
Mdee ambaye pia ni Mbunge wa Kawe (Chadema), alisema maadalizi mabovu ya bunge
hilo ndicho kilichosababisha mambo mengi kwenda kinyume cha matarajio yao.
Alisema
kutokana na kazi kubwa na umuhimu wa kupitia kanuni na kuzichambua kwa kina
kukosa maandalizi ndiyo sababu ya bunge hilo kushindwa kufanya kazi yake kwa
wakati.
“Maandalizi ya kuchambua Rasimu ya Kanuni ni kazi kubwa na ilitakiwa
kanuni zipitiwe mapema na kuchambuliwa kwa kina, lakini kutokana na kutokuwapo
kwa maandalizi ya kutosha ndiko kunakozalisha ucheleweshwaji na utendaji kazi
wa ovyo.
“Mimi siitetei kamati ambayo ilitakiwa kupitia kanuni, lakini
kimsingi kanuni ni muhimu sana kuingia katika mjadala wa Katiba na kama kanuni
itakuwa mbovu, ni wazi kuwa katiba nayo itakuwa mbovu na kanuni ikiwa nzuri ni
wazi kuwa Katiba itakuwa nzuri kwa maana kanuni ndizo zinatoa mwongozo wa
mjadala wa Katiba,” alisema.
“Nina shaka kama kweli makundi ambayo
yamekuja katika bunge yamekuja kwa ajili ya kuboresha Rasimu ya pili ya Katiba
au wamekuja kwa ajili ya kupinga maoni ya Watanzania zaidi ya milioni 45 ambao
walitoa maoni yao,” alisema na kuongeza:
“Kanuni zimekuja na vipengele
mbalimbali ambavyo vinatoa nguvu nyingi kwa Bunge kuliko Sheria kwa maana ya
kutaka kuondoa maneno au mapendekezo ya Rasimu ya pili na kuweka mapendekezo
mapya, jambo ambalo litakuwa ni kutowatendea haki Watanzania.”
Kitomari S., Ngunge J., & Massano J.:Dodoma/Ippmedia-Nipashe
No comments:
Post a Comment