Katibu Mkuu
wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Willibrod Slaa, ameapa kuwa
chama chake hakitakuwa tayari kuona damu ya wakazi wa Kalenga inamwagika katika
kampeni za uchaguzi mdogo wa jimbo hilo unaoendelea, huku baadhi ya wakazi wake
wakibaki na ulemavu wa kudumu kwa lengo la kujibu mapigo ya Chama Cha Mapinduzi
(CCM).
Akizungumza katika uwanja wa Ifunda katika Jimbo la Kalenga, Dk. Slaa
alisema Chadema hakitishiki na kauli iliyotolewa na CCM inayowataka wanachama
wake kuacha unyonge na kujibu mapigo ya Chadema.
”Hatutaki na hatutakubali
Grace Tendega (mgombea ubunge wa Chadema), aende bungeni Machi 18, mwaka huu
huku nyuma akiwa ameacha vilema na baadhi ya wananchi wamefariki dunia kwa
sababu tu CCM wameambiwa waache unyonge.
Nyie Polisi wa Iringa, hii ni fursa
nyingine ambayo Mwenyezi Mungu amewaletea ili muwasaidie maskini wenzenu kupata
kiongozi anayefaa na si kupendelea,” alisema Dk. Slaa.
Alisema licha ya
ukarimu aliokuwa nao aliyekuwa Mbunge wa jimbo hilo, marehemu Dk. William
Mgimwa, kuamua kuwasomesha watoto wa wananchi wasio na uwezo, lakini fadhila
hizo haziwezi kugeuzwa fadhila ya kupeana madaraka ya kurithishana baba na
mtoto kwa kuwa jambo hilo linawadhalilisha na kuwanyima wananchi wengine fursa
ya kuongoza.
Katika hatua nyingine, Dk. Slaa alisema ajenda kuu atakayokwenda
nayo bungeni Tendega iwapo wakazi wa Kalenga watampa ridhaa ya kuwaongoza, ni
pamoja na kuihoji serikali mabilioni ya fedha za wafadhili yanayotolewa kila
mwaka na Jumuiya ya Ulaya (EU) kwa ajili ya maendeleo ya serikali za mitaa
yanakwenda wapi kama si kugeuzwa saccos ya wakubwa na watendaji wa halmashauri.
Mwenyekiti
wa Chadema, Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Dk. Steven Kimondo, alisema wananchi
wa Kalenga wanapaswa kuonyesha hasira zao kwa vitendo dhidi ya CCM kwa
kumchagua mama wa familia na anayejali wanaomzunguka kwa kuwa mpinzani wao
mkuu, Godfrey Mgimwa, anayegombea kupitia CCM, hajui matatizo ya Kalenga kwa
sababu anaishi Uingereza na ameoa Mwingereza.
“Huyu (Grace) ni wa kwenu,
lakini jamaa yetu (Godfrey Mgimwa), akikosa ubunge atarudi Uingereza, ila mama
huyu atabaki hapa hapa na familia yake. Maskini mwenzenu anayetibiwa na
nyie hospitali ambazo hazina dawa na amesoma kwa kukaa chini kama nyie katika
shule hizi hizi,” alisisitiza Dk. Kimondo.
Kwa upande wake, Tendega aliwaomba
wananchi wa Ifunda wamchague ili akajenge hoja bungeni, ni kwa nini fedha za
mfuko wa jimbo zinazotolewa na Bunge kwa ajili ya kusaidia shughuli za
maendeleo ya wananchi zinatolewa kwa upendeleo.
Alisema wananchi wenye itikadi
tofauti na CCM wanaojiunga katika vikundi wanabaguliwa.
“Hizi fedha zinatolewa
kwa wana-CCM tu na kama wakibaini kuna kikundi kina mrengo fulani na hawamuungi
mkono mbunge, wanatoswa kimya kimya na wala hawajali kama hivi ni vicoba,
saccos au vikundi vya wajasiriamali wadogo...sitakubali maana nataka kwenda
kuleta usawa huko Dodoma nawaomba sana mnipe kura ili tumalize wizi huu,”
alisema Tendega.
Mushi G. / Ippmedia-Nipashe
No comments:
Post a Comment