NI
MAKOSA NA HATARI KUACHA KAMATI KUU YA CHAMA KUWAHOJI NA KUWAPIMA MAWAZIRI
Na.
M. M. Mwanakijiji
Kuna
jambo la hatari limetokea nchini jambo ambalo tumelikubali na kuona kuwa ni
halali. Jambo hili litakuwa na matokeo na yawezekana tayari limekuwa na matokeo
katika utendaji kazi wa serikali pale ambapo wanasiasa wanapoamua kuamua hatima
ya watendaji wa serikali na hata kuingilia kati utendaji wa serikali katika
mfumo ambao haupo katika Katiba na Sheria zetu.
Tatizo
hili ni kubwa sana na inashangaza siyo wanasiasa wetu (wa chama tawala au
upinzani) na wala siyo wasomi wetu (wa Katiba na wengine) ambao wamesimama
kulionesha tatizo hili na hatari yake katika kutengeneza mfumo mzuri wa utawala
wa sheria katika nchi ya kidemokrasia. Ni vizuri nifafanue jambo hili ili
wasomaji wangu waelewe kuwa kukubali Kamati Kuu ya chama cha siasa kuingilia
wajibu wa Rais ambao ni wa kwake peke yake (presidential prerogative) ni jambo
la kupinga, kukejeli na kulikataa kwa lugha kali inayowezekana. Kwanini?
1. Wakati Rais anateua Mawaziri Hakuomba Maoni toka Kamati Kuu
ya Chama chake
Katika
ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeweka uteuzi wa mawaziri kama miongoni mwa
yale majukumu ya kipekee ya Rais (presidential prerogatives) ambayo hawezi
kuingiliwa na mtu yeyote katika kutekeleza. Majukumu mengine ya aina hii ni
kama kusamehe wafungwa, kufuta adhabu ya kifo na kutangaza vita.
Ibara
ya 55 ya Katiba inasema kuwa Rais anaweza kuwateua Mawaziri na Manaibu Waziri
kwa idadi yoyote ile baada ya kushauriana na Waziri Mkuu. Katiba haisemi kuwa
Rais anapaswa kufuata ushauri huo wa Waziri Mkuu ndio maana katika Ibara ya 58
inasemwa “Mawaziri na Naibu Mawaziri watashika madaraka yao kwa ridhaa ya Rais,
na watalipwa mshahara, posho na malipo mengineyo kwa mujibu wa sheria
iliyotungwa na Bunge.”
Hii
ina maana moja tu; Mawaziri hawafanyi kazi na hawawajibiki kwa namna yoyote
mbele ya Kamati Kuu ya Chama chao. Wanawajibika mbele ya Rais peke yake. Kitu
kinachotupa sababu ya pili.
2. Rais peke yake ndiyo anawajibu wa kuhoji utendaji kazi wa
mawaziri na manaibu waziri wake
Hili
ni jambo linalotokana na hilo hapo juu. Kama Mawaziri wanateuliwa na Rais na
kama wanafanya kazi kwa ridhaa yake (at his pleasure) basi ni yeye peke
anayeweza kuhojiwa juu ya utendaji wao. Kuwaita Wateule wa Rais “mizigo” ni
kumuita mteuaji “mbeba mizigo”. Huwezi kuwasema walioteuliwa tena ukawananga
vilivyo na wakati huo huo ukawa unaheshimu aliyewateua!
Kama
walioteuliwa wanaboronga, na aliyewateua hawawajibishi hadi watu walalamike au
hafuatilii utendaji wao kwa karibu kiasi kwamba wanaonekana kuwa mizigo kwa
chama chake basi mwenye kubeba wajibu huo ni yeye mteuaji. Wamarekani wanamsemo
kuwa “the bucks stops with the president” kwa maana ya kwamba mambo yote mwisho
wake mwenye kuwajibika ni Rais. Hivyo, Kamati Kuu ya chama haiwezi kufanya kazi
ya Rais, haipaswi kufanya kazi ya Rais na ni makosa kuiacha idhanie kuwa
inaweza kumsaidia Rais kusimamia Mawaziri! Kitu ambacho kinatupa sababu ya tatu
ya kwanini jambo hili ni la hatari na la kukatiliwa vikali.
3. Katiba ya CCM haitoi mamlaka kwa Kamati Kuu ya CCM
kuwasimamia Mawaziri wa serikali
Ibara
ya 109 ya Katiba ya CCM imeweka bayana kazi na majukumu ya Kamati Kuu ya
Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM. Kazi zake zote ni za kisiasa na zinahusiana na
utendaji kazi wa chama na si wa serikali. Hii ina maana Kamati Kuu ya CCM haina
madaraka yoyote ya kuwaita, kuwahoji au kuwapa maelekezo ya kiutendaji wateule
wa rais wa ngazi yoyote ile; siyo mawaziri, siyo manaibu, wala siyo wakuu wa
mikoa! Madaraka hayo haina na haijapewa na hivyo kimsingi ni kuingilia kazi za
vyombo vingine. Hili linatupa jambo la nne.
4.
Ibara ya 63 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano imetoa nafasi kwa mawaziri wa
serikali kuulizwa juu ya wizara zao na utendaji wao wa kazi. Kifungu kidogo cha
3(a) cha Ibara hiyo kinasema kuwa Bunge laweza “kumuuliza Waziri yeyote swali
lolote kuhusu mambo ya Umma katika
Jamhuri
ya Muungano ambayo yako katika wajibu wake;” Hili linajibu swali jepesi tu;
sasa kama Kamati Kuu ya chama haiwezi kuwauliza mawaziri nani basi ukimuondoa
Rais anayeweza kuwauliza maswali na kuwawajibisha mawaziri? Jibu liko katika
Ibara hiyo na ibara nyingine ambayo imelipa Bunge uwezo wa kupiga ya kutokuwa
na imani na serikali (ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu).
Kama
kuna kiongozi au mwanachama yeyote ndani ya CCM ambaye hafurahii utendaji kazi
wa waziri yeyote njia pekee na rahisi ya kumfuatilia waziri au kuwafuatilia
mawaziri hao ni kupitia wabunge wa chama hicho Bungeni. Hili ni muhimu hasa
ukizingatia ukweli kuwa CCM ina wabunge wengi zaidi kiasi cha kwamba hawahitaji
kura za upinzani kupitisha jambo lolote Bungeni (wana wingi wa theluthi zaidi
ya mbili). Hivyo, kama kuna waziri mzigo njia na mahali pekee pa mawaziri hao
kuhojiwa na kuwajibishwa ni Bungeni na hilo linaweza kufanywa na wabunge tu.
Na
kama wabunge wa CCM wanaona serikali yenyewe ndio tatizo wana njia nyingine
mbili za kuiwajibisha; kupiga kura ya kutokuwa na imani na Rais au kutafuta
sababu ya Kikatiba ya kumuondoa Rais Madarakani kupitia Mashtaka ya Kibunge
(Impeachment).
Kufuatia
kutangazwa kwa Baraza Jipya la Mawaziri hoja hizi hapa ni muhimu kuzingalia na
kuzizingatia kwani kama tutaacha huu “mchezo” wa kisiasa ambapo chama cha siasa
kinaingilia majukumu ya Rais hatutakuwa na serikali iliyo thabiti (stable)
madarakani kwani itakuwa serikali ambayo badala ya kufanya kazi kwa ridhaa ya
Rais inafanya kazi kwa ridhaa ya Kamati Kuu ya chama.
Ni
kwa sababu hiyo kwa madaraka yangu ya kipekee niliyojipatia mimi mwenyewe;
nikizingatia dhamira yangu natangaza na kuwataka mawaziri wote wapya na wale
wazamani kukataa mara moja kusimama mbele ya Kamati Kuu ya chama kutoa maelezo
yoyote isipokuwa Bungeni au mbele ya Rais. Hii si kwa ajili ya utukufu wao bali
kwa ajili ya kutenganisha wazi kabisa majukumu ya vyombo mbalimbali nchini ili
kuhakikisha hakuna mwingiliano haramu.
Na
kwa madaraka hayo ninawataka mawaziri wote ambao watajikuta wanalazimishwa
kuweka vyeo vyao mbele ya altare ya chama chao cha siasa kuamua kujiuzulu kazi
zao mara moja kuliko kujidhalilisha kama walivyojidhalilisha baadhi ya mawaziri
wiki chache zilizopita ambao kwa woga wao na kukosa kwao msimamo waliitwa na
kusimama mbele ya Kamati Kuu ya CCM.
Na
wakati umefika kwa Rais Kikwete kuanza kukubali kuwajibika kwa makosa ya
mawaziri wake haiwezekani awe anapata nafasi ya kubadilisha tu na siyo kuwafuatilia
au yeye mwenyewe kuwajibika. Kwani yeye ndiye mamlaka ya juu ya uteuzi na
uwajibishaji na kushindwa kwake kuwawajisha mawaziri wake hadi chama chake
kiamue kumsaidia ni udhaifu mkubwa na wa hatari katika demokrasia yetu. Ni
lazima awe tayari kusimama na mawaziri wake au yeye mwenyewe kuwakingia kifua
kuliko kuwatosa kila wakati mambo yanapokuwa magumu na kusingizia ni
“kuwajibika kisiasa”. Na sisi tungependa kuona nay eye anawajibika kisiasa kama
wengine au yeye mwenyewe awawajibishe bila kulazimishwa na Bunge. Kama hana
muda, nia, uwezo au uthubutu wa kufanya hivyo ni vizuri akaamua nay eye ajipime
mbele ya wananchi kama anastahili kuendelea na majukumu yake au atumie haki
yake chini ya Katiba ili ampishe Makamu wake kufanya kile ambacho yeye ameshindwa.
Vinginevyo,
atajikuta analiachia taifa mojawapo ya mazoea (precedence) mbaya sana ya
kiutawala nchini ambayo ikikubaliwa kama ilivyokubaliwa sasa serikali zetu huko
mbeleni zitapata kazi sana kusimama madarakani.
Na
kwa Mawaziri na Manaibu wao wapya – karibuni kazini na nyinyi mtawajibishwa
pia.
Heri
ya Mwaka Mpya!
Niandikie:
mwanakijiji@jamiiforums.com
Nitafute
Facebook: “Mimi Mwanakijiji”
Nifuate Twitter: “Mwanakijiji”
No comments:
Post a Comment