Waziri Kivuli wa Nishati na Madini ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Ubungo, John Mnyika amemshauri Rais Jakaya Kikwete kumhoji Waziri wa Nishati na Madini, Prof. Sospeter Muhongo akidai amewadanganya Watanzania kuhusiana na gharama za umeme. Kwa mujibu wa taarifa ambayo Mnyika aliitoa kwenye vyombo vya habari jana, Prof. Muhongo amekuwa akidanganya na kuwahakikisha Watanzania kwamba gharama za umeme hazitapanda hata kama Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) litapendekeza kupanda kwa gharama hizo. Alisema kinyume na kauli hiyo, gharama hizo zimepanda na kuongeza mzigo wa maisha kwa wananchi na kuathiri uchumi wa nchi na wizara yake haijasema chochote kuhusiana na suala hilo. “Kufuatia ukimya wa Wizara ya Nishati na Madini na mamlaka nyingine tangu nitoe wito kwao Januari 9 mwaka huu juu ya ongezeko la bei ya umeme, namshauri Rais Jakaya Kikwete katika mchakato wa mabadiliko ya Baraza la Mawaziri kumtaka Waziri Profesa Sospeter Muhongo kujieleza kwake na kwa umma ili kuwezesha hatua stahiki kuchukuliwa,” alisema Mnyika na kuongeza:
“Rais Kikwete akumbuke kwamba Waziri Muhongo alisema uongo kwa nyakati mbalimbali mwaka 2012 na 2013, alipowahakikishia wananchi kwamba bei ya umeme haitapanda hata baada ya Tanesco kuwasilisha mapendekezo ya kupandisha bei ya umeme.” Alisema tayari wananchi wameanza kupata athari mbalimbali kutokana na kupanda kwa gharama za umeme. Aidha, alisema baada ya kupanda kwa gharama hizo alitoa wito kwa wananchi kutoa maoni yao juu ya ongezeko hilo, na kwamba tayari amekwisha pokea maoni mbalimbali ya wananchi kuhusiana na kupanda kwa gharama za umeme ambao wengi wao wamependekeza badala ya mamlaka kukimbilia kupandisha bei ya umeme ni bora kupunguza mzigo wa gharama za uzalishaji, usafirishaji, na usambazaji. Alisema wananchi pia wamependekeza kwamba endapo mamlaka husika haitapunguza gharama hizo, basi yaandaliwe maandamano kushinikiza serikali kuchukua hatua za haraka za kunusuru uchumi wa nchi pamoja na maisha ya wananchi.
Source: Zaya E. (Jan 2014).Mnyika amn'gang'ania Prof. Muhongo. Retrieved from Ippmedia/Nipashe
No comments:
Post a Comment