Maaskofu wa
Makanisa mbalimbali mchini, wamezungumzia kwa nyakati tofauti mustakabali wa
Taifa huku wakitaka watawala kuheshimu maoni yaliyotolewa na wananchi kuhusu
Katiba mpya pamoja kuchukua hatua mapema kwa viongozi waliopewa dhamana za
kuongoza na kushindwa kuwajibika.
Katika mahubiri yake kwenye Kanisa Kuu la
Utatu Mtakatifu, Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Morogoro,
Godfrey Seheba, alitaka watawala kuheshimu mapendekezo yote yalitolewa katika
rasimu ya pili ya Katiba iliyowasilishwa na Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya
Katiba, Jaji mstaafu Joseph Warioba.
Askofu Seheba alisema kuwa mapendekezo
hayo yaliyotolewa na wananchi iwapo yataheshimiwa na kupitishwa katika Bunge la
Katiba, yatasaidia kuleta umoja na mshikamano ili kuifanya nchi kuwa na amani
na utulivu kama ilivyokuwa na sifa yake.
Hata hivyo, Askofu Seheba
alisisitizia umuhimu wa Watanzania kuendelea kuombea rasimu hiyo ili ipatikane
kwa Katiba mpya itakayokidhi mahitaji ya Watanzania kwa maslahi ya nchi na
ustawi wa jamii.
Naye Askofu Mkuu wa Kanisa la Kilutheri la Kiinjili Jimbo la
Morogoro, Jacob Mameo, akizungumza katika mahubiri yake katika Kanisa la Mji
mpya, alisema mwaka 2014, uwe ni mwaka wa serikali kuchukua hatua za haraka kwa
viongozi waliopewa dhamana ya kuongoza na kushindwa kuwajibika badala ya
kusubiri madhara kujitokeza kwa wananchi.
Askofu Mameo alisema mwishoni mwa
mwaka jana, Taifa lilishuhudia madhara makubwa waliyopata wananchi wakati wa
Operesheni Tokemeza kutokana na viongozi hao waliopewa mamlaka kushindwa
kusimamia ipasavyo.
Alisema hali hiyo isipodhibitiwa mapema itazidi kuleta
athari kwa wananchi. Askofu Mameo aliwataka viongozi wanaopewa dhamana kuwa na
hofu ya Mungu katika utendaji wao wa kazi na kuweka maslahi ya taifa mbele ili
kuleta maendeleo na kudumisha amani iliyopo.
Kwa upande wake, Mhashamu Askofu
wa Kanisa Katoliki Jimbo la Morogoro, Telesphori Mkude, alisisitiza umuhimu wa
waumini wa dini zote kuendelea kuliombea Taifa ili kuwa na amani hasa katika
kipindi hiki cha mchakato wa kupata Katiba mpya.
Askofu Mkude aliwataka
Watanzania kuepuka mifarakano na uvunjifu wa amani na badala yake wawe kitu
kimoja hasa katika kipindi hiki cha kuibuka kwa rasilimali mbalimbali za taifa
ikiwamo gesi na mafuta.
Source: Ippmedia (jan. 2014). Maaskofu: Watawala heshimuni maoni ya wananchi Katiba mpya. retrieved from Ippmedia/Nipashe
No comments:
Post a Comment