UKATILI kwa watoto wadogo nchini unazidi kushika kasi
ambapo askari polisi wanne wa Kituo cha Turiani Mvomero, wanatuhumiwa kuwavunja
miguu na mbavu watoto wanne kwa kuwapiga kwa madai ya kuiba vyuma chakavu. Malalamiko hayo yalito lewa jana na wazazi wa watoto hao,
Stephania John (75), Kudura Rajabu (33), wakidai watoto wao Elias Michael (11)
na Dickson Kudura (15) wamelazwa katika Hospitali ya Misheni ya Bwagala wakiwa
wamefungwa bandeji ngumu (POP).
Rajabu ambaye ni mzazi wa Dickson na Stephania mama mzazi
wa Elias, walisema kuwa waliambiwa kuna mtu alikwenda polisi akidai watoto hao,
Elias, Dickson, Ismail Seif na Victor Elias, waliiba vyuma chakavu na vipuri
vya gari, rim mbili, jeki, betri, vioo, simu tano na sh 150,000.
“Hatutetei watoto hao, kama wamefanya makosa wangestahili
wakumbane na mkono wa sheria, lakini si kama polisi walivyojichukulia hatua
mkononi ya kuwafanyia unyama wa kuwapiga, kuwavunja miguu na kuwapa ulemavu wa
kudumu,” alisema Stephania. Waliwataja askari wanaodaiwa kuhusika kuwatesa watoto wao
kuwa ni Afande Muddy (Traffic), Robert, Romano’s na askari mgambo aitwaye Gogo. Walipoulizwa wanachukua hatua gani, walisema wao ni
watu duni, hawana uwezo wa kifedha.
“Kila njia tumefanya tangu Novemba 17 mwaka huu, tumeishia
kupigwa ‘changa la macho’, tumesikia askari wamewekwa ndani, lakini
tunanong’onezwa usiku wanalala makwao, labda taasisi za haki za binadamu
zitusaidie,” alisema Stephania. Mkuu wa Kituo cha Polisi Turiani, Fineous Majura
alipohojiwa hakuonyesha ushirikiano akidai kuwa si msemaji bali atafutwe
Kamanda wa Mkoa, Faustine Shilogile. Wazazi hao wamegoma kuwachukua watoto wao hospitalini
wakiitaka polisi walipe gharama za kuwatoa kama walivyolipa gharama za
kiingilio cha matibabu na kisha wawapeleke mahakamani ili wakawawekee dhamana
huko.
Source: Mathius B. (Dec. 2013).Polisi
wadaiwa kuwavunja miguu watoto. Retrieved from Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment