MKAKATI wa Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM),
Mwigulu Nchemba, kuwanunua madiwani watatu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(CHADEMA), wilayani Igunga mkoani Tabora umegonga mwamba. Mwigulu anadaiwa kuwashawishi madiwani hao wakubali sh
milioni 45 ili wajivue uanachama wa CHADEMA. Tanzania Daima imedokezwa kuwa baada ya mpango huo
kukamilika, wajumbe wa kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya hiyo walipousikia
waliugomea kwa madai utasababisha machafuko zaidi katika maeneo yao.
Katika Wilaya ya Igunga, CHADEMA wana madiwani watatu kati
yao mmoja ni wa viti maalumu ambapo Mwigulu anadaiwa katika mkakati wake huo,
aliwashirikisha wajumbe wa kamati ya ulinzi na usalama ambao walivujisha siri
hiyo kwa uongozi wa CHADEMA. “Tulimueleza wazi kuwa tutakuwa tunaiingiza serikali
katika gharama za matumizi ya fedha kwa sababu zisizo na msingi wowote kwa
ajili ya kutaka sifa za kisiasa, tulikataa na tukawaambia madiwani kama
watathubutu kuwasaliti wananchi tutawafikisha mahakamani kwa kuwa mkakati huo tunauelewa,”
alisema mmoja wa wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama mjini Igunga.
Kwa mujibu wa sheria, kamati ya ulinzi na usalama ya
wilaya inaundwa na mkuu wa wilaya na wawakilishi wa vyombo vyote vya usalama
katika wilaya husika. Mkakati huo unaelezwa kupata upinzani kutoka kwa wajumbe
wa kamati ya ulinzi na usalama wilayani Igunga, kwa kile walichoeleza kuwa
wamechoka kushuhudia vifo na matukio ya uvunjifu wa amani yanayoweza
kujitokeza. Wapinzani wa mpango huo walieleza kuwa sababu ya
kumkatalia Mwigulu ni pamoja na kurejea matukio yaliyojitokeza wakati wa
uchaguzi mdogo wa ubunge uliomuingiza Dk. Dalaly Kafumu madarakani baada ya
Rostam Aziz kujiuzulu nafasi hiyo akihusishwa na tuhuma za ufisadi.
Katika uchaguzi mdogo wa Igunga uliofanyika mwaka 2011,
baadhi ya watu waliuawa na wengine kujeruhiwa katika mchakato mzima wa
kuhitimisha uchaguzi huo. Ofisa habari wa CHADEMA, Tumaini Makene, alipoulizwa juu
ya kuufahamu mpango huo wa Mwigulu, alikiri kupata taarifa hiyo, lakini
haukufanikiwa kwakuwa walidhibiti kila mwanya wa hujuma hiyo. Akijibu tuhuma hizo, Mwigulu alisema hazina ukweli na
hajui kama katika Wilaya ya Igunga kuna madiwani wa CHADEMA. “Havina ukweli na sijui kama Igunga ina madiwani wa
CHADEMA, kwani wana msaada gani kwa chama changu na wana tatizo gani wakiwa
CHADEMA?” alisema.
Source; Abdalah H. ( Dec. 2013).
Mwigulu akwama Igunga. Retrieved from Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment