Serikali imeyataka
makundi mbalimbali ya watu yanayopenda majina yao kuteuliwa kuwa Wajumbe wa
Bunge Maalumu la Katiba, kufanya hivyo kabla ya Januari 2, 2014 saa tisa
alasiri. Pia imeyaagiza makundi
hayo kuzingatia sifa zilizotajwa kwenye Sheria ya Marekebisho ya Katiba wakati
wa uteuzi wa majina ya watu watakaowapendekeza. Akizungumza jijini Dar es
Salaam jana, Waziri wa Sheria na Katiba, Mathias Chikawe alisema kuwa makundi
hayo yanatakiwa kuwasilisha kwa Rais orodha ya majina ya watu wasiopungua wanne
na wasiozidi tisa. “Rais Jakaya Kikwete
Desemba 13, 2013 alitoa tangazo kwa mujibu wa kifungu kidogo cha (2A) cha
kifungu cha 22 cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, Sura ya 83 alialika kila
kundi kutoka pande zote za Muungano kuwasilisha kwake majina kwa ajili ya
kuzingatiwa kwenye uteuzi,” alisema Chikawe.
Alibainisha kuwa kila
kundi linatakiwa kuzingatia umri, jinsia, uzoefu, sifa na sehemu ya makazi ya
mtu aliyependekezwa. Jumla ya idadi ya wajumbe kutoka Zanzibar hawatapungua
moja ya tatu ya wajumbe wote. Chikawe alisema iwapo
itabainika kuwa mtu aliyeteuliwa aliwahi kufungwa au kutokuwa na sifa, uteuzi
wake utatenguliwa kwa kuwa atakuwa amepoteza sifa ya kuwa mbunge. “Hatuwezi kuwa na kundi
la watu kutoka katika dini moja au kabila moja,” alisema. Akifafanua, alisema Bunge
Maalumu la Katiba lina makundi matatu, ambapo wabunge wote wa Jamhuri ya
Muungano, wajumbe wote wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar na watu 201 kutoka
kwenye makundi mbalimbali watakuwa wajumbe.
Chikawe alisema pia
zimetengwa nafasi 20 kwa ajili ya wajumbe kutoka makundi mengine yoyote, ambayo
yana malengo yanayofanana. Orodha ya majina hayo itawasilishwa kwa kupelekwa
kwa Katibu Mkuu Kiongozi, Ikulu, Dar es Salaam au Katibu Mkuu Kiongozi, Ofisi
ya Rais, Zanzibar. Pia Chikawe alitangaza kuwa Desemba 30, 2013,
Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba atawasilisha
taarifa kamili ya tume hiyo kwa Rais Jakaya Kikwete na Dk Mohammed Shein.
Source: Eliona G. (Dec. 2013).Serikali yataja rasmi makundi ya kuunda Bunge Maalumu la Katiba. Retrieved from Mwananchi
No comments:
Post a Comment