TAARIFA
KWA VYOMBO VYA HABARI
‘SERIKALI YA KIKWETE IKOMESHE
‘UKABURU’ DHIDI YA WATANZANIA’
KATIBU Mkuu wa Chama cha Demokrasia
na Maendeleo (CHADEMA), Dkt. Willibroad Slaa amehitimisha ziara yake ya siku 22
ya kuimarisha na kukagua uhai wa chama katika majimbo 19 mikoa ya Shinyanga,
Kigoma, Tabora na Singida, akiitaka Serikali ya Rais Jakaya Kikwete kukomesha
manyanyaso na ukatili wanaofanyiwa wananchi.
Amesema kuwa baada ya kuzungumza na
wananchi hususan maeneo ya vijijini ambako alijikita kwa siku hizo 22,
ameendelea kuthibitisha kuwa sehemu kubwa ya kero zinazowakabili Watanzania,
hazihitaji gharama yoyote kuzimaliza ili wananchi waishi kwa amani katika nchi
yao, akitolea mfano wa kero ya manyanyaso mbalimbali, hususan kutoka kwa vyombo
vya dola.
Amesisitiza kuwa kama Serikali ya
Rais Kikwete inataka kupata uhalali mbele ya Watanzania na iwapo Rais mwenyewe
anataka kumaliza muda wake na kuacha kumbukumbu kwa wananchi, inatakiwa
kukomesha mara moja manyanyaso wanayofanyiwa wananchi, kwani kufanya hivyo ni
wajibu wa serikali na hakuna gharama yoyote.
Akitolea mifano ya matukio ya
kikatili na ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu unaofanywa vyombo vya serikali
kupitia matukio mbalimbali zikiwemo operesheni mbili za hivi karibuni, Tokomeza
Ujangili na Kimbunga, Katibu Mkuu amesema kwa namna ambavyo serikali iliyoko
madarakani inawatenda raia wake, Tanzania inavunja rekodi hata ya Afrika Kusini
ya enzi za Makaburu.
“Tunamtaka Rais Kikwete kuacha
kufanya kama afanyavyo baba asiyejali au baba wa kambo anayechukia watoto…JK
ukitaka ubaki na heshima baada ya kuondoka madarakani, fanyia kazi orodha ya manyanyaso
wanayofanyiwa wananchi. Tena mengi yanafanywa na polisi, jeshi na wakuu wa
wilaya, watendaji wa vijiji na watendaji wa kata na madiwani.
“Yapo mengine ya kubambikia kesi
watu, kunyang’anywa ardhi, kunyimwa haki kwa nuguvu tu, kuchangishwa michango
haramu inayoambatana na vipigo na kunyang’anya watu mali zao, huku mapato na
matumizi hayasomwi na kero nyingine kubwa ni migogoro ya ardhi. Kuachia
manyanyaso haya dhidi ya wananchi ni kuonesha udhaifu mkubwa wa kiuongozi.
Labda watuambie kuwa serikali hii ya CCM sasa imeshaamua kuwageuka raia
wake.
“Hauhitaji hata senti moja kuondoa
manyanyaso ya serikali kupitia vyombo vya dola wanayofanyiwa wananchi.
Mnapomtesa Mtanzania namna hii…watu wanateswa sana na kubambikiwa kesi,
wanapigiliwa spoke sehemu za siri, wanawekewa chupa na kubakwa, mnataka aende
kuishi wapi.
“Hayo maendeleo mnayoyazungumza ni
kwa ajili ya nani kama wananchi wanapigwa, kuteswa na kuuwawa bila hatia.
Tumefikia mahali serikali inawatenda raia wake kuliko hata Makaburu
walivyomtesa Mzee wetu Hayati Mandela alipokuwa gerezani.
“Mwalimu Nyerere alisema ukaburu si
rangi. Huu unaofanyika ni ukaburu ambao wakati ule wa ubaguzi wa rangi tuliimba
sana shuleni na majeshini kupinga ukatili wa makaburu wa Afrika Kusini dhidi ya
weusi waliokuwa wengi. Leo Serikali hii inafanyia raia wake matendo zaidi ya
yale. Tunakwenda wapi. Kikwete chukua hatua.”
“Kila nilikopita ni vilio vya
manyanyaso, kuanzia Kakonko kule Wilaya ya Buyungu, kote huko Kasulu Vijijini
viongozi wangu wote wa serikali nzima ya kijiji wamebambikwa kesi ya mauaji,
wote kabisa. Hapo Nzega nimeshuhudia kwa macho yangu mateso wanayoyapata
wachimbaji wadogo wadogo, wengine wamepigwa vibaya na askari polisi, tena
machimbo yao yametekwa na viongozi wa wilaya na kuyageuza mali zao na sasa
wanachuma pesa kwa kupiga raia.”
Katibu Mkuu Dkt. Slaa ambaye
alianza ziara yake Desemba 4, mwaka huu kwa kufanya mkutano wa hadhara na kikao
cha ndani Jimbo la Kahama, mkoani Shinyanga, amehitimisha ziara yake Desemba
23, kwa kuhutubia wananchi wa Vijiji vya Shelui na Nyengege, Jimbo la Iramba
Magharibi.
Amewataka wanaCHADEMA kuuchukulia
mchakato na mjadala wa Katiba Mpya ya Watanzania kuwa agenda ya muhimu, ya
kudumu na lazima katika mikutano yao yote, ikiwemo ya ndani ya chama, hadhara
au ‘vijiweni’, lengo la msingi liwe kuwataarifu wanachama na wananchi kwa
ujumla, tulikotoka, tulipo na tunakokwenda.
Ametumia ziara hiyo kuwasisitiza
viongozi na wanachama wa CHADEMA nchi nzima kuhakikisha wanatekeleza maagizo
mbalimbali ya vikao ya chama, hususan kwa sasa wasimamie kikamilifu maelekezo
ya Waraka Katibu Mkuu Namba 6 wa mwaka 2013.
Waraka huo ambao unahusu mkakati wa
kusukuma ujenzi wa misingi/matawi na uchaguzi wa ndani ya chama 2013/2014,
umeelekeza viongozi nchi nzima namna ya kuendesha programu ya ‘M4C-CHADEMA ni
Msingi’ inayoendelea nchi nzima, ikisimamiwa na kanda 10 za chama ambapo moja
ya malengo mahsusi ni kusimika na kuimarisha chama kwenye vitongoji na mitaa.
“Ni lazima kila mwanaCHADEMA,
wapenzi wa chama hiki, wananchi wenye mapenzi mema na ukombozi wa pili wa taifa
lao, tuungane, tushikamane pamoja kusukuma jitihada hizi za kusimika chama
chenu, ambacho ndiyo tumaini jipya la Watanzania katika ngazi ya chini kabisa
ya uongozi katika nchi yetu.
“Viongozi wote wenye mapenzi mema na
CHADEMA, kuanzia ngazi ya taifa hadi chini kabisa lazima wahakikishe CHADEMA ni
msingi inakamilika kama ilivyokusudiwa,” amesisitiza Katibu Mkuu Dkt. Slaa
katika ziara hiyo.
Katika kuwakumbusha juu ya waraka
huo, Katibu Mkuu Dkt. Slaa amewasisitiza wanachama na viongozi umuhimu wa
kuzingatia;
1. Kupata viongozi imara wa
chama kuanzia ngazi ya chini kabisa ya msingi
2. Ratiba ya utekelezaji wa
mkakati wa CHADEMA ni Msingi.
3. Ratiba ya uchaguzi wa ndani
ya chama ngazi ya jimbo hadi taifa (pamoja na mabaraza ya chama), baada ya
ngazi za chini kumalizika.
4. Kuzingatia taratibu za
kikatiba za uchaguzi, kwani uchaguzi wa ‘mezani’ hautakubalika ndani ya
CHADEMA.
5. Rushwa na kampeni chafu
(katika uchaguzi kwa ngazi yoyote ile) hazitavumiliwa hata kidogo.
6. Maadili ya chama yasimamiwe
kwa kila ngazi ya uchaguzi.
7. Ulinzi wa chama/ viongozi
na wanachama ngazi zote, ambapo Red Brigade na BAVICHA ndiyo
nguzo ya ulinzi.
Ukombozi wa kweli kwa mwananchi
uanzie serikali za mitaa
Katibu Mkuu amewataka Watanzania
kuelewa kuwa ukombozi wa kweli wa mwananchi utapatikana iwapo watu wataweza
kuchagua viongozi imara, makini, waadilifu na wapenda watu kuanzia ngazi ya
kitongoji, mtaa na kijiji na hatimaye madiwani ambao huunda halmashauri ya
wilaya, mji, manispaa au jiji.
“Ikulu ya kwanza ya mwananchi ni
hapa ulipo, hapa kijijini au mtaani kwako. Ikulu ya pili ni halmashauri yenu ya
wilaya. Hizi ni sehemu muhimu sana katika kuhakikisha watu wetu wanapata
matumaini, haki na hatimaye ustawi wa maendeleo ndani ya nchi yao. Hakuna maana
yoyote kuichagua CHADEMA iende Ikulu ya Magogoni, Dar es Salaam halafu huku
mnaweka watu wabovu. Itakuwa sawa na kazi bure,”amesisitiza Katibu Mkuu Dkt.
Slaa.
Amesema kuwa hasa wakati huu ambapo
Taifa linajiandaa kwenda kufanya uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka 2014,
Watanzania wanapaswa kutambua umuhimu wa halmashauri za serikali za mitaa
katika kusukuma maendeleo ya watu katika maeneo yao wanayoishi.
Amesisitiza kuwa katika ngazi hiyo
ya uongozi, si kazi ngumu kumtambua mtu ambaye anaweza kuwa kiongozi mwadilifu,
makini mwenye uwezo na mpenda watu, kwa sababu watu wote wanafahamiana kutokana
na kuishi pamoja.
Pinda kubanwa chaguzi serikali za
mitaa
“Katika ziara yangu hii ya siku 22,
nimebaini kuwa kuna maeneo mengi sana ya vijiji ama hayana serikali kabisa,
sehemu nyingine mwenyekiti hayupo au wajumbe, lakini Serikali ya CCM kupitia
kwa wakurugenzi inaogopa kuitisha uchaguzi, kisa wanaogopa wakiitisha uchaguzi
CHADEMA itashinda.
“Sasa napenda kutumia mkutano wangu
huu wa kuhitimisha ziara hii, kutoa maagizo kwa viongozi wa chama wilaya na
majimbo, kutuandikia taarifa ya kina Makao Makuu, ikieleza maeneo yote ya
serikali za mitaa ambayo yako wazi na wakurugenzi hawajatangaza au hawataki
kutangaza ndani ya muda unaotakiwa kisheria uchaguzi wa kuziba nafasi
kufanyika.
“Tunataka taarifa za kina ambazo
tutazitumia kumbana Mizengo Pinda maana yeye ndiye anahusika kusimamia Wizara
ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa au TAMISEMI. Hatuwezi kukubali kuona
wananchi wanakosa haki yao ya uwakilishi kwa sababu tu CCM wanaogopa ukiitishwa
uchaguzi CHADEMA tutashinda. Katika hili pia tutakufa na Pinda,” amesema Katibu
Mkuu.
Katibu Mkuu Dkt. Slaa ametembelea
jumla ya majimbo 19 ambayo ni; Kahama (Shinyanga), Kakonko, Muhambwe, Kasulu
Vijijini, Kasulu Mjini, Buhigwe, Kigoma Kaskazini, Kigoma Mjini, Kigoma Kusini;
mkoani Kigoma. Mengine ni;
Kaliua, Urambo, Tabora Kaskazini,
Tabora mjini, Sikonge, Igalula, Bukene, Nzega, Igunga (Tabora) na Iramba
Magharibi mkoani Singida.
Katika maeneo yote aliyotembelea,
Katibu Mkuu Dkt. Slaa amepokea kero na ushauri wa wanachama na Watanzania kwa
ujumla, kuhusu masuala mbalimbali ya chama na nchi, ya kitaifa na mengine
yanayohusu maeneo husika (local politics), kwa njia kadhaa ikiwemo taarifa za
viongozi kuhusu utendaji wa chama, kupitia maswali na maoni katika mikutano
pamoja na kufika mwenyewe kujionea hali halisi ya baadhi ya masuala
aliyoambiwa.
Imetolewa leo Desemba 23, 2013 na;
Tumaini Makene
Ofisa Mwandamizi wa Habari-CHADEMA
Hivi ndivyo ilivyokuwa...
Desemba 4, 2013 Kahama
No comments:
Post a Comment