Dr. Slaa akifanya mkutano Kasulu leo
JITIHADA za Chama Cha Mapinduzi (CCM) kutumia mzozo kati
ya Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe, na Chama cha Demokrasia na
Maendeleo (CHADEMA) zinaelekea kugonga mwamba. Tanzania Daima Jumapili limedokezwa kuwa CCM imewekeza vya
kutosha katika hujuma dhidi ya CHADEMA ikitumia baadhi ya wanachama wa zamani
wa chama hicho kuunda mgogoro na kukipasua. Hata hivyo, licha ya misukosuko na kelele kutoka kwa
baadhi ya wanachama na wanaodhaniwa kuwa ‘mapandikizi’, CHADEMA kimeweza
kupuuza hujuma hizo na kujikita katika harakati za ujenzi wa ngazi za chini za
chama katika vijiji na vitongoji.
Kwa sasa viongozi kadhaa wa CHADEMA wamesambaa katika
majimbo 103 nchi nzima kujenga chama kwa kufuata maagizo ya Baraza Kuu
lililoketi mwishoni mwa mwaka jana, kama mwendelezo wa vuguvugu la mabadiliko,
na ujenzi wa chama kuelekea uchaguzi unaokuja. Baadhi ya wanachama walioondolewa kwa tuhuma mbalimbali
wamekuwa wanashirikiana na wana CCM waziwazi kusambaza maneno machafu dhidi ya
CHADEMA mtandaoni na mitaani. Baadhi yao wameshiriki kutengeneza mabango na
kuyapeperusha katika mikutano inayohutubiwa na Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk.
Willibrod Slaa, katika mikoa ya Shinyanga na Kigoma.
Wanapinga uamuzi wa Kamati Kuu kuwavua nyadhifa Zitto, Dk.
Kitila Mkumbo na Samson Mwigamba. Zitto amevuliwa wadhifa wa Naibu Katibu Mkuu,
Dk. Kitila amevuliwa wadhifa wa Mjumbe wa Kamati Kuu, na Mwigamba amevuliwa
wadhifa wa Mwenyekiti wa Mkoa wa Arusha kwa tuhuma za ‘usaliti’. Katika kumtetea Zitto na wenzake, baadhi ya wanachama
wamekuwa wakitoa matamko, huku wawili wakitangaza kujiuzulu nafasi zao katika
mikoa ya Lindi na Singida. Huku wakitoa shinikizo kwa chama Zitto asichukuliwe hatua
zaidi, baadhi yao mkoani Kigoma walikwenda mbali wakitaka chama kiahirishe
ziara ya Dk. Slaa mkoani humo hadi baadaye, kwa kisingizio cha usalama.
Hata hivyo, Dk. Slaa alisisitiza kuwa masuala ya usalama
yamezingatiwa barabara, na kwamba ziara ziko pale pale, kwani hakuna mkoa au
wilaya ya mtu. Tanzania Daima limedokezwa kuwa uongozi wa CCM mkoani
Kigoma, chini ya Dk. Aman Walid Kabourou, umekuwa ukiratibu vitisho na fujo
katika mikutano au maeneo anayotembelea Dk. Slaa kwa lengo la kutisha wananchi. Dk. Kabourou aliwahi kuwa Mbunge wa Kigoma Mjini kwa
tiketi ya CHADEMA kabla ya kukimbilia CCM miaka kadhaa iliyopita. Alipohamia
CCM akapewa ubunge wa Afrika Mashariki. Sasa ndiye Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa
Kigoma. Makundi ya vijana wa CCM na wana CHADEMA wenye matatizo na
chama, wamekuwa wakisambazwa kuelekea maeneo kadhaa kwa lengo la kuhujumu
mikutano ya Dk. Slaa.
Lengo ni kutumia fursa hii kujaribu kudhoofisha uwezo wa
chama kinachohatarisha utawala wa CCM. Miongoni mwa mikakati ya kuivuruga CHADEMA inayofadhiliwa
kwa gharama kubwa ni kuwapandikiza vijana kufanya fujo katika mikutano ya Dk.
Slaa. Katika mikutano hiyo vijana mbalimbali wamekuwa
wakijitokeza na mabango ya kupinga uamuzi wa kuondolewa kwa Zitto, kuzomea na
kufanya vituko vyenye lengo la kuharibu mikutano hiyo. Miongoni mwa matukio hayo ni lile lililotokea juzi katika
Kijiji cha Mabamba wilayani Kibondo, ambako zaidi ya vijana saba
walikamatwa na kufikishwa kwenye kituo cha polisi.
Hata hivyo, baadhi ya watu waliokuwapo eneo la tukio
waliwatambua kuwa wengi wao ni vijana wa CCM ambao wamekuwa wakizunguka katika
mikutano yote anayofanya Dk. Slaa. Katika mikutano yake mkoani Shinyanga na Kigoma, Dk Slaa,
alisema propaganda za udini, ukabila na ugaidi zinazopandikizwa na CCM zimezidi
kuimarisha chama chake katika safari ya kuelekea Ikulu mwaka 2015. Dk. Slaa alisema wanaosema CHADEMA itakufa hawajui
kinachoendelea, kwa sababu ya uamuzi wa kuwachukulia hatua au kuwaondolea
nyadhifa watu wasiotaka kufuata maadili, katiba na miongozo ni njia ya kukipa
uhai chama hicho.
“Mimi nilidhani CCM wangeshangilia chama chetu kufa,
lakini hiki ninachokiona kinanistaajabisha; yaani eti wanatuonea huruma sisi
tusife? Huu ni muujiza,” alisema. Tanzania Daima Jumapili, limekuwa likidokezwa kuwa
viongozi wa CCM wamekuwa wakifadhili harakati za kuidhoofisha CHADEMA ili
wasipate upinzani mkali katika uchaguzi ujao. Wiki iliyopita kupitia ukurasa wake wa facebook, Naibu
Katibu Mkuu wa CCM (bara), Mwigulu Nchemba aliandika kuwaMkurugenzi
wa Oganaizesheni na Mafunzo wa CHADEMA, Benson Kigaila aliyekuwa Kigoma
alipigwa na wafuasi wa Zitto hadi kushindwa kusimama hadi aliposaidiwa na
polisi. Wakati Mwigulu akituma maneno hayo kupitia ukurasa wake,
Kigaila amesema kuwa yeye yupo katika ziara ya kujenga chama mkoani Mbeya, na
aliondoka Tukuyu kwenda Njombe kwa kazi hiyo hiyo.
Wakati wana CCM wakishangilia kile kinachoitwa mpasuko ndani
ya CHADEMA, Dk. Slaa anasema wanazidi kuimarika na watafanya vizuri zaidi
katika chaguzi zijazo. Katika mazungumzo yake na Tanzania Daima, wiki iliyopita,
Dk. Slaa aliwataka Watanzania wawe makini, kwani hao wanaotoa matamko ya
kulaani Kamati Kuu wanafanya kazi ya CCM, hata kama baadhi yao wana kadi za
CHADEMA. “Wanaojitokeza kutoa matamko kulaani Kamati Kuu ya CHADEMA
hawazungumzi bei ya umeme kupanda, hawazungumzi hali mbaya ya elimu na afya
nchini, hawazungumzii suala la mishahara ya wafanyakazi, wamejikita kumjadili
Mbowe na Slaa.
“Niwahakikishie wanachama na Watanzania wanaotaka
mabadiliko kuwa tuna usalama uliokomaa tunajua hujuma zote, ndio maana jana
Naibu Katibu Mkuu wa CCM, Mwigulu Nchemba, aliwatangazia Watanzania kuwa
Mkurugenzi wetu wa Oganaizesheni na Mafunzo Benson Kigaila amepigwa na wafuasi
wa Zitto na amesaidiwa na polisi wala hajiwezi hata kusimama.” Dk. Slaa alisema wakurugenzi na viongozi mbalimbali wa
chama hicho wapo kwenye majimbo 103 nchi nzima kwa ajili ya ujenzi wa chama
ngazi ya msingi, kutekeleza uamuzi wa Baraza Kuu. Alisisitiza kuwa ziara hizo
hazina uhusiano na propaganda zinazosambazwa sasa kuhusu hatua ya chama hicho
kumvua vyeo Zitto.
Source: Tanzania Daima ( Dec. 2013).
CHADEMA yadinda. Retrieved from Tanzania Daima

No comments:
Post a Comment