Polisi mkoani Pwani
inachunguza kundi la watu linalodaiwa kuweka magogo barabarani kuzuia msafara
wa Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) taifa, Sadifa Juma Khamis (MB)
katika eneo la Tondoroni, wilayani Kisarawe, mkoani humo.
Kamanda wa Polisi
mkoa wa Pwani, Ulrich Matei, alisema atazungumzia suala hilo baada ya
kupata taarifa kamili.
Kwa mujibu wa watu walioshuhudia tukio
hilo, kundi hilo liliweka magogo hayo jana usiku katika barabara ya kati ya
eneo la Mpuyani katika njia panda ya barabara iendayo vijijini kuingia barabara
kuu ya Morogoro.
Mashuhuda wa tukio hilo walisema katika nyakati tofauti kundi
hilo lilianza kuzuia msafara huo kwa kutaka kushinikiza dai la mgogoro wa
mipaka kati ya eneo la Jeshi la Wananchi wa Ulinzi Tanzania (JWTZ) na makazi ya
watu katika eneo la Tondoroni, wilayani humo.
Watu hao ambao idadi yao
haikuweza kufahamika walidaiwa kutishia kuchoma moto magari ya msafara huo wa
mwenyekiti wakati alipotaka kushuka na kuzungumza nao na kuamua kujisalimisha
kwa kuingia ndani ya gari na kurudi Kisarawe.
Mwenyekiti huyo
ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Donge, Tanzania Visiwani mapema akiwahutubia
wananchi wa Kisarawe aliwataka kudumisha amani kwa kukiweka Chama Cha
Mapinduzi madarakani. “Amani ikivurugika hakuna atakayekuwa salama, hata
askari nao hawatokuwa salama”.
Akiongea na viongozi wa CCM na
UVCCM katika jengo la ofisi za CCM wilaya, aliwataka wanachama hao
kuvunja makundi ya kampeni kwa kuwa hayana tija kwa sasa, isipokuwa wakati wa
kampeni za uchaguzi.
Alisema kuwa Muungano wa Tanzania ni muhimu hivyo
changamoto zilizomo ndani yake zitafutiwe muafaka kwa njia ya amani.
Alisema
kuna baadhi ya watu wakorofi ambao wanadai muungano uvunjwe hasa kutoka
Pemba wakidai kuwa kisiwa hicho ni chao wakati visiwa hivyo vya Pemba na
Zanzibar havina wenyewe na watu walioko huko wametokana na biashara
ya utumwa na wengi wao walitoka upande wa Tanzania Bara wa makabila mbalimbali.
Wakati
huo huo, mwenyekiti huyo alimsimika mwandishi wa siku nyingi, Abubakar Mlawa
kuwa kamanda wa UVCCM wilayani humo na wengine 15 wakiwamo madiwani
kuwa makamanda wa UVCCM wa kata zao.
Source: Lugungulo A. ( Nov. 2013). Msafara wa Mwenyekiti UVCCM wawekewa magogo. Retrieved from Ippmedia/ Nipashe
No comments:
Post a Comment