Shahidi katika kesi
ya kusafirisha wanyama hai na ndege kwenda Qatar, Indonesia, Maulid
Hamis, ameieleza mahakama kuwa twiga watatu walikufa wakiwa chini ya uangalizi
wa mwajiri wake ambaye ni mshitakiwa namba moja, Kamran Mohamed.
Akitoa
ushahidi wake mbele ya hakimu mkazi wa mahakama hiyo, Simon Kobelo.
Alidai
kuwa kwa kipindi hicho yeye alikuwa ni mfanyakazi katika kampuni ya ukamataji
wanyama inayomilikiwa na mshitakiwa wa kwanza na alikuwa akikamata wanyama hao
na kuwahifadhi katika zizi la wanyama.
Alidai mahakamani hapo kuwa kuanzia
mwaka 2009 kazi yake ya kwanza aliyoifanya akiwa na Kamran ni ya kwenda
kukamata twiga na walifanikiwa kukamata twiga wanne waliokuwa wakiwawinda kwa
kuwatega na kamba na kuwafunga katika maboksi na kuwapeleka katika zizi.
“Siku
ya kwanza tukiwa na kibali pamoja na Kamrani, tulikamata twiga watatu na
tulitumia siku mbili katika kuwakamata huku siku iliyofuata tukafanikiwa
kumkamata twiga mmoja na kwa bahati mbaya alikufa twiga mmoja na baada ya siku
kadhaa wa pili na watatu nao pia walikufa…
daktari alipompasua twiga mmoja
alisema kuwa wamekufa kwa sababu ya hofu…tuliendelea na kazi ya kukamata
wanyama wengine wakiwamo tompson na grant gazer ambao nao walikuwa wakifa kwa
wingi wakiwa zizini,” alidai mahakamani hapo.
Mbele ya Mwendesha mashitaka wa
serikali, Evetha Mushi na Stela Majaliwa, ilidaiwa mahakamani hapo kuwa kila
twiga alipokuwa akifa walikuwa wakiambiwa wachimbe shimo refu na kumfukia huku
wakipewa amri ya kwenda kuwakamata wengine na kufanikiwa kukamata twiga watatu
na kufikisha jumla ya twiga wanne ambao walisafirishwa Novemba 25, 2010.
Aidha
ilidaiwa mahakamani hapo kuwa mara baada ya wiki tatu walipewa amri nyingine na
mshitakiwa wa kwanza ya kwenda kutafuta wanyama wengine na kuwarudisha zizini
ambapo walifanikiwa kukamata nyati, tompson na twiga mmoja lakini hawakuweza
kupata nyumbu na pofu.
Shahidi huyo pia alidai kuwa kutokana na twiga huyo
kukimbia sana, alikufa mara tu baada ya kufikishwa zizini ambapo madaktari
kutoka maliasili walisema amekufa kutokana na kukimbia kwa muda mrefu na kwamba
walisafirishwa pofu watatu, nyumbu sita, tompson 32, grant 12 na twiga wanne.
Washitakiwa
hao wanakabiliwa na kosa la kusafirisha wanyama hai na ndege kwenda nchini Doha
kwa kutumia ndege aina ya C.17 yenye nambari AMA/MAB mali ya shirika la Qatar
Airways ambapo waliwapitisha wanyama na ndege hao kwenye geti namba 5A na 5B
katika kiwanja cha ndege cha KIA.
Washitakiwa hao ni Kamran Mohamed Raia wa
Pakistani, Hawa Hassan, Martin Methew na Michael Disha, wote wapo nje kwa
dhamana isipokuwa mshitakiwa wa kwanza. Kesi hiyo imeahirishwa hadi Januari
21, mwakani.
Source: Lymo C. (Nov. 2013).Shahidi aeleza Twiga walivyokuwa wanakamatwa. Retrieved from Ippmedia/ Nipashe

No comments:
Post a Comment