Suala la kutimuliwa kwenye madaraka
ya uongozi aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(Chadema) Zitto Kabwe, na Mwanazuoni kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam,
Kitila Mkumbo, sasa limechukua sura mpya.
Shirikisho la wanachama wanafunzi wa
Chadema kutoka vyuo vya Elimu ya Juu, mkoa wa Dar es Salaam (Chaso), jana
limeibuka na kuunga mkono uamuzi wa Kamati Kuu Chadema kuwavua uongozi
waliodaiwa kufanya uasi ndani ya chama Shirikisho hilo pia limewarushia
shutuma Mtela Mwampamba, Habib Mchange, Juliana Shonza na Greyson Nyakarungu,
waliofukuzwa Baraza la Vijana Chadema (Bavicha), kutengeneza makundi ya kupinga
uamuzi uliofikiwa na Kamati Kuu hiyo.
Akisoma tamko lao kwa niaba ya viongozi
wenzake, Mratibu Mkuu wa shirikisho hilo, Himida Jackson, alisema mapema wiki
hii kikundi cha vijana wanaojiita viongozi wa Chaso, waliibuka na kutoa taarifa
ya kupinga maamuzi yaliyofikiwa na Kamati Kuu Chadema.
Tamko hilo ambalo
limesainiwa na mratibu huyo pamoja na Afisa Habari wa shirikisho hilo, Amandus
Gomba, limetokana na kikao kilichofanyika juzi Chadema na kufikia uamuzi wa
kuliandaa kwa ajili ya umma wa Watanzania.
Alisema taarifa
zilizoripotiwa kwenye vyombo vya habari wiki hii kuwa Chaso limepinga uamuzi wa
kamati kuu siyo za kweli na kwamba waliozitoa hawatambuliki kwenye kumbukumbu
za wanachama wao.
Alifafanua kuwa mapema mwaka huu Bavicha liliwafukuza baadhi
ya vijana kwa usaliti wao ambapo waliotajwa hapo juu walikimbilia chama tawala.
“Kikundi
hicho (waliofukuzwa) kimekuwa kikipita huko mtaani na kukusanya vijana wa CCM
wanaojipachika uanachama wa Chadema na kujipatia vyeo vya Chaso kisha kutoa
matamko ya kupinga maamuzi ya chama,” alisema.
Alisema baadhi yao
wamekuwa wakijitambulisha ni viongozi wa Chadema Chuo Kikuu cha Dar es Salaam
wakati siyo kweli, huku akitaja majina ya viongozi wanaotambulika kuwa ni Marco
Julius ambaye ni mwenyekiti na Daniel Mswelo, katibu.
Aliongeza kuwa,
Januari 19, mwaka huu, uongozi wa Chaso Chuo Kikuu cha Ardhi ulisimamishwa
kutokana na utendaji mbovu.
Alisema kwa misingi hiyo, vijana hao hawana
uhalali wa kufanya shughuli zozote kwa ngazi ya uongozi au chama.
Alisema
Jumapili iliyopita vijana hao walifanya jitihada za kushawishi wanafunzi wa
vyuo vikuu kuungana nao katika kupinga maamuzi yaliyotolewa na kamati kuu
ingawa hawakufanikiwa katika hilo.
Alisema tamko la Jumatano ya wiki hii
walilolitoa watu hao ni mwendelezo wa jitihada hizo walizozikusudia. Kutokana
na hilo, amewataka wanachama watambue kuwa, tamko hilo siyo halali huku
akisisitiza kuwa msimamo wao unaunga mkono maamuzi yaliyochukuliwa na Kamati
Kuu hasa kwa kuhakikisha hakuna mtu yeyote aliye juu ya chama.
“Tunasisitiza
chama kisiruhusu mmoja wetu abomoe nyumba hii hata kama alishiriki kuijenga au
hatuwezi kuruhusu mtu atoboe mtumbwi tunaosafiria,” alisema.
Akizungumzia
kuhusu chama, Jackson alisema ni chenye watu wenye nia ya dhati ya kulikomboa
taifa na watu wake ambao wanakabiliwa na matatizo ya kiuchumi, kijamii na
kisiasa.
“Tunaamini Chadema ndicho chama pekee ambacho ni mbadala Tanzania
kilichobeba matumaini ya Watanzania kwa kuwa kinapigania haki za kila mnyonge,”
alisema.
Aliwataka wanachama na viongozi kuwa makini na kutosita kuchukua
maamuzi dhidi ya mtu yeyote hasa katika kipindi hiki ambacho wamesikia kauli za
viongozi wa CCM wanaojiapiza kuwa Chadema haitafika uchaguzi mkuu.
Mwenyekiti
wa Chadema UDSM, Julius Michael, alisema kuwa yanayoendelea hivi sasa ni
propaganda ya CCM kutaka kukihujumu Chadema na kuonyesha yaliyoamuliwa na
kamati kuu ni uonevu kwa sababu chama tawala hakijawahi kuchukua maamuzi magumu
kama hayo.
Alisema baadhi ya vyombo vya habari (bila kuvitaja), vimenunuliwa
na vimekuwa vikiripoti uamuzi huo wa kamati kuu tofauti.
Mjumbe wa Chaso,
Gwamaka Mbughi alisema baadhi ya magazeti yaliandika bila uhalisia hivyo
kupotosha umma.
Alisema kwa mujibu wa katiba na kanuni za chama chao, Chaso
hakina mamlaka ya kupinga maamuzi yaliyofikiwa. Mwenyekiti wa Chaso kutoka Chuo
cha Usimamizi wa Fedha (IFM), Musa Ndile, alisema maamuzi ya kamati ni halali
hivyo inapotokea mtu ameenda kinyume bila kujali anakubalika kwa kiasi gani,
hatua zitachukuliwa kwa mujibu wa katiba yao.
Source: Mallya R. (Nov. 2013). KUTIMULIWA ZITTO, Dk. Kitila CHASO: Uamuzi wa CC Chadema ni muafaka. Retrieved from Ippmedia/ Nipashe
No comments:
Post a Comment