MBUNGE wa Kigoma
Kaskazini, Zitto Kabwe (CHADEMA), amepata pigo jipya baada ya wabunge wenzake
wa chama hicho kuamua kumuondoa rasmi kwenye nafasi yake ya kuwa Naibu Kiongozi
wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni. Habari kutoka ndani
ya CHADEMA, zinasema kuwa uamuzi wa kumuengua Zitto kwenye nafasi hiyo,
ulifikiwa kabla ya mbunge huyo kuvuliwa nyadhifa nyingine za kichama baada ya
Kamati Kuu (CC) ya chama hicho kumtia hatiani kwa makosa ya usaliti. Kwa mujibu wa
vyanzo vya habari, tayari wabunge wa CHADEMA wameshapitisha azimio la kumvua
nafasi hiyo na chama kinaandaa taarifa rasmi kwa mbunge huyo na ofisi ya spika
kumhafamisha jambo hilo.
Duru za siasa
kutoka ndani ya CHADEMA zilisema kuwa hata kama Zitto asingevuliwa nyadhifa
zake kichama, tayari walishapanga kumvua nafasi ya naibu kiongozi wa kambi
rasmi ya upinzani bungeni kwa madai ya kutokuwa na imani naye. Akizungumza na
Tanzania Daima jana, Mwanasheria Mkuu na Mnadhimu Mkuu wa CHADEMA, Tundu Lissu,
alisema kuwa Kamati Kuu ya chama hicho ilitoa maelekezo kwa Kamati ya Wabunge
kukaa mara moja na kumvua nafasi yake ya Naibu Kiongozi wa Kambi Rasmi ya
Upinzania Bungeni. “Azimo la CC
lilielekeza Kamati ya Wabunge wa CHADEMA kukaa mapema iwezekanavyo kumvua
nafasi hiyo isipokuwa nafasi ya Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya
Hesabu za Serikali (PAC) ambayo amechaguliwa na wabunge wa vyama vyote,”
alisema Lissu.
Hivi karibuni,
mbunge huyo maarufu nchini, amevuliwa nyadhifa zake zote za uongozi ndani ya
CHADEMA na kubaki kuwa mwanachama wa kawaida. Nafasi alizovuliwa
ni Naibu Katibu Mkuu (Bara), Ujumbe wa Kamati Kuu (CC) na Mjumbe wa Baraza Kuu
na Mkutano Mkuu. Mbali ya Zitto
viongozi wengine waliovuliwa nyadhifa zao na kubaki kuwa wanachama wa kawaida,
ni Dk. Kitila Mkumbo aliyekuwa mjumbe wa Kamati Kuu (CC) na Samson Mwigamba
aliyekuwa Mwenyekiti wa CHADEMA Mkoa wa Arusha, ambaye kompyuta yake mpakato
(laptop), ilinaswa kutumika kutuma makala inayodaiwa kukichafua chama kwenye
mtandao wa kijamii wa Jamii Forum. Uamuzi huo mgumu na
mzito ulifikiwa wakati wa kikao cha Kamati Kuu (CC), kilichofanyika katika
ukumbi wa Hoteli ya Blue Pearl jijini Dar es Salaam hivi karibuni. Inadaiwa kuwa
pamoja na mambo mengine, Zitto alikuwa kinara wa mkakati wa kuleta mabadiliko
haramu ndani ya chama hicho, huku waasisi wake wakijipa majina ya MM, M1 na M2.
Source: Tanzania
Daima (Nov. 2013). Zitto apata pigo jingine. Retrieved from Tanzania
Daima
No comments:
Post a Comment