SIKU chache baada ya Waziri wa zamani na Mbunge wa Urambo
Magharibi, Profesa Juma Kapuya (CCM) kutuhumiwa kumbaka na kutishia kumuua
binti mdogo wa miaka 16, kiongozi huyo ameibuka na kutoa utetezi wa
kujikanganya. Akizungumza kupitia kwa wakili wake, Yasin Memba, mbunge huyo
alitishia kuliburuza gazeti hili mahakamani endapo halitamwomba msamaha ndani
ya siku saba. Pamoja na kukataa kwake kumfahamu binti huyo, Kapuya amekiri
kumiliki simu namba 0784993930 ambayo imekuwa ikitumiwa kuwasiliana naye
ikiwemo kumtumia ujumbe mfupi wa maneno (sms) wa vitisho.
Hata hivyo, katika namna ya kushangaza, Kapuya alidai kwamba
simu hiyo aliishaigawa miezi sita iliyopita, na hivyo hausiki kwa namna moja
ama nyingine na tuhuma alizopewa. Lakini wakati Kapuya akikwepa mtego huo, Novemba 9, mwaka huu,
gazeti hili liliwasiliana naye kupitia namba hiyo hiyo anayodai kwamba
alishaigawa miezi sita iliyopita. Tarehe hiyo, gazeti hili liliwasiliana na mbunge huyo ili
kuthibitisha tuhuma zilizokuwa zikimkabili wilayani Kaliua za kumpiga makofi
kiongozi mmoja wa CCM. Kapuya kupitia namba hiyo, alitoa utetezi wake ambapo gazeti
hili lina sauti yake. Utetezi wake pia unaongeza utata kwani hakufafanua ilikuwaje
akagawa namba ya simu iliyosajiliwa kwa jina lake kwa mtu mwingine, huku
ikiendelea kutuma fedha na vitisho kwa binti huyo.
Katika utetezi wake jana, Kapuya alikana kutomjua binti huyo
wala dada yake, na kwamba yeye si mwathirika wa ugonjwa wa ukimwi. Alilishutumu gazeti hili kuwa lilijifanya hakimu kwa kuchapisha
tuhuma zake bila kumpa nafasi ya kujitetea kama ilivyo kawaida kwenye tasnia ya
habari. Hata hiyo, ukweli ni kwamba nafasi hiyo aliipata, lakini
hakuitumia kwani alipopigiwa, simu yake ilipokelewa na mtu aliyejitambulisha
kuwa ni dereva wake na kutaka aelezwe sababu za kutafutwa bosi wake. Hata alipoelezwa kuwa anayehitajika ni bosi wake, alisita kisha
alitoa namba nyingine ya simu akitaka atafutwe kupitia namba hiyo.
Lakini muda wote namba hiyo haikupokelewa na hata alipopigwa
tena namba ya awali, nayo iliita bila kupokelewa. Wakili Memba alidai kuwa mteja wake, alimweleza kuwa habari ile
imemletea madhara na usumbufu mkubwa katika familia yake, jamii na kumvunjia
heshima yake. “Kwa sababu hiyo, amenielekeza niwapatie siku saba gazeti la
Tanzania Daima, mitandao ya kijamii ukiwemo wa Jamii Forum, Justina John na
Vituko Mtaani ambao walichapisha habari hiyo, waombe radhi kwa uzito ule
ule la sivyo atavishitaki mahakamani. “Kama hawataomba radhi, basi atafungua kesi mbili, moja ni kwa
ajili ya gazeti la Tanzania Daima na hiyo mitandao ya kijamii, na kesi ya pili
ni ya kuhusu huyo mtoto anayedaiwa kubakwa na kuambukizwa ukimwi,” alisema.
Aliongeza kuwa wanataka mtoto huyo aje mahakamani athibitishe
aliambukizwaje ukimwi na alete ushahidi unaoonyesha Kapuya ana ukimwi. Memba aliuomba umma kuelewa kuwa habari hiyo iliyochapishwa na
Tanzania Daima haiusiani na chama chake wala serikali. Kwa siku mbili mfululizo gazeti hili lilifichua tuhuma za Kapuya
kudaiwa kumbaka mtoto huyo, na hata baada ya kubaini siri hiyo imevuja,
alimpigia simu mtoto huyo, na baadaye kutuma meseji kadhaa za vitisho. Tanzania Daima ilishuhudia baadhi ya meseji za simu zilizotumwa
na Prof. Kapuya kwenda kwa mtoto huyo. Juzi alfajiri saa 11:21 kupitia simu yake alituma ujumbe kwa
mtoto huyo: “Chagueni kunisubiri tuje tuongee au mnataka kufa?”
Baadaye saa 1:07 asubuhi, alituma ujumbe mwingine kutoka simu
hiyo hiyo kwenda kwa mtoto huyo, ukisema: “Mkiuawa, itakuwa nzuri,
itawapunguzia gharama za kuishi. Usitake kugombana na serikali, mtoto mdogo
kama wewe. Sisi ndo wenye nchi yetu.” Baadhi ya mashirika yanayotetea makundi kadhaa yakiwamo Kituo
cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) na Mtandao wa Kijinsia Tanzania (TGNP)
yalijitokeza kuwasaidia watoto hao, ambao ni yatima. Mtoto huyo na dada yake, wakizungumza na gazeti hili kwa hofu
mafichoni, walisema kwa sasa hawana imani tena kama kuna serikali nchini
Tanzania kwa kuwa wamedhalilishwa, wametembezwa hadi bungeni na wabunge bila
hatua kuchukuliwa, licha ya kutoa taarifa katika Kituo Cha polisi Oysterbay
tangu mwaka jana.
Hata hivyo, kabla ya tukio la watoto hao kuripotiwa ofisi za
gazeti hili, juzi usiku kulikuwa na watu waliokuja wakiwatafuta watoto hao,
huku wakiwatisha kwa simu na kuwatolea maneno ya kejeli, wakidai watawamwagia
tindikali. Juzi gazeti hili lilichapisha habari kuhusu mwanafunzi
huyo aliyesema kuwa waziri huyo alimbaka kwenye hoteli moja ya kitalii
iliyoko jijini Dar es Salaam mwaka 2011, na kurudia tena kitendo hicho katika
Jengo la Biashara Complex lililoko Mwananyamala Juni 3, 2012 alipoitwa kwenda
kuchukua ada kwa mara ya pili.
Source: Tanzania Daima (Nov. 2013). Kapuya ajikoroga. Retrieved from Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment