CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimeibuka
kidedea katika uchaguzi wa Naibu Meya wa Jiji la Arusha, huku kikisisitiza
msimamo wake wa kutomtambua Meya wa jiji hilo, Gaudency Lyimo
(CCM). Ushindi wa CHADEMA ulikuwa wa mteremko baada ya Chama Cha Mapinduzi
(CCM) kuacha kuweka mgombea huku mgombea wa Chama cha Tanzania Labour (TLP),
Michael Kivuyo naye akijitoa siku moja kabla ya uchaguzi. Hata hivyo,
mshindi wa kiti hicho, Diwani wa Kata ya Daraja Mbili, Prosper Msofe, aliibua
mzozo kwa madiwani wa CCM baada ya kutangaza msimamo huo wa CHADEMA kutomtambua
meya. Uchaguzi huo ulifanyika jana wakati wa kikao cha mwisho wa mwaka cha
Baraza la Madiwani ambapo kulitanda ulinzi mkali wa polisi waliovalia kiraia,
Usalama wa Taifa na wale wa kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa
(Takukuru).
Kufanyika kwa uchaguzi huo, kumekata kiu ya wananchi
wengi wa jiji hili, hasa kwa kuzingatia kwamba nafasi hiyo imekuwa wazi tangu
Desemba 2010 baada ya uchaguzi uliofanyika awali kwa kumweka
madarakani Lyimo, kudaiwa kuwa haukukidhi vigezo kisheria. Hatua hiyo, ilimlazimu naibu meya aliyekuwa amechaguliwa
kushika nafasi hiyo, Kivuyo (TLP) kujiuzulu. Katika uchaguzi huo wa jana, Msofe aliibuka mshindi baada
ya kupata kura 25 za ndiyo na mbili za hapana huku moja ikiharibika hali
inayodhihirisha wazi kuwa madiwani wa CCM pamoja na wabunge wao nao
walimchagua. Habari toka ndani ya kikao hicho, zinadai kuwa mara baada
ya Msofe kutangazwa kuwa naibu meya, alimweleza meya kuwa hamtambui kwani
taratibu zilizotumika kumweka kwenye kiti hicho hazikuwa halali.
Akizungumza na Tanzania Daima nje ya kikao, Meya Lyimo
alikiri kutolewa kwa kauli hiyo huku akidai kuwa inashangaza kwani yeye ndiye
aliyesimamia uchaguzi uliomweka naibu meya huyo madarakani sasa inakuwaje
asimtambue. Alisema kuwa hakuna uchaguzi mwingine wa meya kwa sasa
kwani sheria iko wazi kuwa uchaguzi hufanyika kila baada ya miaka mitano
wanapochaguliwa madiwani wengine. Katika uchaguzi wa kamati za kudumu za Mipango Miji,
Mazingira na Ujenzi, Diwani wa Moshono, Paul Matthysen (CCM) aliibuka mshindi
kwa kupata kura 11 dhidi ya moja aliyopata Diwani wa Elerai, Injinia,Jeremiah
Mpinga ambapo kamati hiyo inaundwa na madiwani watano wa CHADEMA na sita wa
CCM.
Uenyekiti wa Kamati ya Uchumi, Elimu na Afya ulichukuliwa
na Diwani wa Ngarenaro, Doita Isaya (CHADEMA) aliyepata kura tisa dhidi ya
mbili alizopata Diwani wa Kata ya Engutoto, Elibariki Marlley (CHADEMA). Wakizungumza na waandishi wa habari, Matthysen aliahidi
kusimamia shughuli za kamati hiyo ipasavyo kwa kuhakikisha watendaji
wanazingatia sheria kwa kuhakikisha hakuna ujenzi holela utakaoendelea
kwenye Jiji la Arusha wala biashara zinazofanyika pembezoni mwa barabara za
waenda kwa miguu na magari. Naye Isaya aliahidi kufanya kazi kwa karibu na wanakamati
wenzake pamoja na wakuu wa shule ili kuhakikisha watoto wanapatiwa elimu bora
sanjari na kuwapunguzia wazazi mzigo wa michango mingi isiyo na tija.
Wakati huohuo, CHADEMA kimedai kuwa CCM haikusimamisha
mgombea kwenye nafasi ya naibu meya kwa kuhofia kushindwa kutokana na kuwa na
idadi ndogo ya madiwani. CHADEMA walikuwa 15 huku wale wa CCM wakiwa 13 kutokana na
mbunge wa viti maalumu, Namelock Sokoine kutohudhuria.
Source: Macha G. (Nov. 2013). CHADEMA
yatwaa Unaibu Meya Arusha. Retrieved from Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment