Naibu Katibu Mkuu wa CHADEMA Taifa
Mh. Zitto Kabwe (Mb) amesema Katiba Mpya ni lazima iwajali Wakulima na Wananchi
wanaoishi vijijini hapa nchini maana wametelekezwa kwa muda mrefu, kudhulumiwa
na kufanywa maskini wa kutupwa. Zitto amesema Wananchi wengi wa
vijijini hasa wa Kanda ya Magharibi wanapata shida leo kwa kichagua CCM ambapo
Wabunge wao wamekuwa hawawatetei Bungeni wala hawaulizi maswali na wengine
kutetea maslahi yao binafsi badala ya maslahi ya Wananchi hao. Amesema Waziri Mkuu Mizengo Pinda
tangu achaguliwe hajawahi kuuliza swali Bungeni kwa sababu alipochaguliwa tu
aliteuliwa kuwa Waziri matokeo yake Wananchi wa Jimbo lake wanakosa mtu wa
kuwawasilishia hoja zao Bungeni. “Pinda hata ukimwambia aandike swali kwa taratibu
za kibunge hajui ni kama walivyokuwa wenzie akina Abdallah Kigoda na Mark
Mwandosya ambao tangu walipochaguliwa tu waliteuliwa kuwa Mawaziri, hawawezi
hata kuandika maswali. Kigoda alipata shida kweli kuuliza maswali alipoachwa
kwenye Baraza la kwanza la Mawaziri la Rais Kikwete” Alisema Zitto.
Akizungumza na Wananchi wa Kijiji
cha Mwajalila katika Kata ya Mpanda ndogo Zitto alimshangaa Mbunge wa Jimbo la
Mpanda Magharibi Moshi Selemani Kakoso ambaye badala ya kutetea Wananchi wake
wapate bei nzuri ya Tumbaku, Mbolea kwa wakati na watibiwe kwa mfuko wa Bima ya
afya ambao wamekuwa wakiuchangia Tsh 10,000/= kwa mwaka bila kupata dawa wala
huduma yoyote wanapoumwa; Mbunge huyo kazi yake ni kuzunguka Dar es salaam na
kufanya mikutano na waandishi wa habari kunusuru ulaji wake wa APEX uliofutwa
na Bunge kwenye vyama vya ushirika. (Kakoso alikuwa ni Mwenyekiti wa Shirika
la APEX ambalo kwa muda mrefu lilikuwa likiwalangua wakulima wa Tumbaku nchini
kwa muda mrefu kabla halijafutwa na sheria ya Bunge). Akiwa katika Kijiji cha Karema
kilichokuwa Makao Makuu ya Jimbo la Magharibi enzi za Mkoloni na
kilichogunduliwa na Wamisionari wa Kigiriki toka Kongo Zitto aliwaambia
Wananchi wa eneo hilo “Si mnaona hata mradi wenu wa Bandari hapa Kijiji na
Tarafa ya Karema mmepewa Mkandarasi feki wakati sisi kule Kigoma Bandari
karibia inakamilika ni kwasababu wanajua Kigoma yuko Zitto na hapa yuko mbunge
dhaifu na mwizi mwenzao wa CCM” alisema Zitto
Tunataka Katiba Mpya izuie Wabunge
kuwa Mawaziri na iwape nguvu Wananchi ya kuwawajibisha Wabunge ambao
hawawasilishi maslahi yao kwa kuwaondoa madarakani na kuchagua wengine.
Akizungumzia Pensheni kwa Wakulima
Zitto amesema Taifa hili linaendeshwa na Wakulima ambao wanachangia sehemu
kubwa sana ya pato la taifa, lakini wanapochoka kwa maradhi au uzee wanaishia
kuwa ombaomba na mzigo kwa familia zao kwa kukosa pensheni ya uzeeni hali ya
kuwa nguvu yao iliishia katika kulijenga Taifa. “Si haki mfanyakazi wa ofisini
apate NSSF na pensheni za uzeeni wakati mkulima anayemlisha na kuchangia kwa
kiasi kikubwa pato la Taifa akizeeka ndio mwisho wake wa kujitegemea” alisema
Zitto. Ziara ya Zitto leo ilifanyika
katika Jimbo la Mpanda Magharibi ambapo amezindua vijiwe 20 vya Chama, kupokea
kadi 150 za waliokuwa Wanachama wa CCM katika vijiji vya Mwajalila,
Kasekese,Kapalamsenga, Karema (Bismarkburg enzi za Mjerumani) na Ikola, akiwemo
Kampeni Meneja wa Mbunge Kakoso wakati wa Uchaguzi Mkuu wa 2010. Ziara
itaendelea ya Mh.Zitto kesho katika Jimbo la Mpanda Mjini ambapo jioni
kutafanyika Mkutano Mkubwa sana wa hadhara. Ziara hii ni utekelezaji wa Program
ya CHADEMA NI MSINGI.
Kurugenzi ya Habari CHADEMA
No comments:
Post a Comment