VITUO vya afya 170 mkoani Dodoma havina huduma ya maji hali inayotishia afya za wagonjwa. Katibu Tawala Mkoa wa Dodoma, Rehema Madenge, alieleza hayo jana katika uzinduzi wa mradi wa maji kwa afya ya jamii. Alisema kati ya vituo vya afya 432 vilivyopo, 171 havina huduma ya maji kabisa huku vingine vikikabiliwa na uhaba wa mara kwa mara. Alisema hali ni mbaya zaidi kwa wajawazito pindi wanapokwenda kujifungua, kwani hulazimika kwenda na ndoo za maji zaidi ya tano kutokana na huduma wanayopatiwa kuhitaji maji mengi, hali inayosababisha usumbufu mkubwa kwa mgonjwa, waganga, wauguzi na watu wanaowasindikiza. Katibu huyo alisema mradi huo uliozinduliwa utakuwa mkombozi mkubwa katika vituo vya afya mkoani hapa kutokana na maeneo mengi kukabiliwa na ukame wa muda mrefu.
Wakizungumzia mradi huo uliopo chini ya ufadhili wa Mfuko wa Maendeleo wa Serikali ya Uswisi, washirika wa maendeleo kutoka wilaya saba za mkoa walisema tatizo la maji katika vituo vya afya linaleta adha kubwa kwa wagonjwa. Mganga Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa, Dk. Sigfid Ishengoma alisema hali ya upatikanaji wa maji katika vituo vya afya hasa vilivyoko maeneo ya vijijini wilayani humo ni mbaya hali inayosababisha wakati mwingine madaktari kushindwa kuwahudumia wagonjwa. Ofisa Mkuu wa mradi huo, Ewout Van Galen, alisema mradi huo uliogharimu dola milioni 5 za Marekani (sh bilioni 8) utakaotekelezwa kwa miaka minne ukikamilika utaondoa kero ya maji katika vituo vyote vya afya mkoani hapa.
Source: Mtweve H. (Sept. 2013). Vituo vya afya vyakosa maji. Retrieved from Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment