Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa imefuatilia taarifa
kwenye vyombo vya habari mbalimbali hapa nchini, kuhusu kushiriki kwa
Mheshimiwa Lu Younqing Balozi wa Jamhuri ya Watu wa China hapa nchini kwenye
mkutano wa hadhara ulioandaliwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) uliofanyika huko
Shinyanga, mwishoni mwa juma lililopita.
Taarifa hizo zimeambatana na picha zinazomuonyesha Mheshimiwa Lu akiwa
amevaa kofia yenye nembo ya CCM. Habari zinaeleza kuwa Balozi alikwenda
Shinyanga kuhudhuria uzinduzi wa mradi wa viwanda vya kuchambulia pamba
vinavyojengwa na mwekezaji wa Kichina anayeitwa Tahong, na viwanda hivyo vita
kuwa na uwezo wa kuchambua tani 120,000 za pamba kwa mwaka, vitakapokamilika
mwakani.
Wizara inatambua mahusiano mazuri yaliyopo kati ya Jamhuri ya watu wa
China na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na vilevile inatambua kazi nzuri
ambayo Balozi Lu Younqing amekuwa akifanya toka alipowasili nchini Tanzania.
Kutokana na tukio hili, Wizara inapenda kuelekeza kwamba kitendo cha Balozi
yeyote kuhudhuria mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa na kuvaa sare zenye
nembo ya vyama vya siasa sio sahihi na kinakiuka Kifungu cha 41(1) cha Mkataba
wa Vienna wa mwaka 1961, unaoongoza uhusiano wa kidiplomasia. Mkataba huo wa
Vienna unazuia wawakilishi wa nchi za nje kujihusisha na masuala ya ndani ya
nchi ikiwemo siasa wanapofanya kazi zao kwenye nchi za uwakilishi. Aidha,
Sheria ya Diplomasia ya Tanzania ya Mwaka 1986 ambayo ni zao la Mkataba wa
Vienna pia hairuhusu Balozi au mfanyakazi wa Ubalozi kujihusisha na masuala ya
ndani ya nchi.
Itakumbukwa kwamba, katika kipindi cha mwaka 2010 hadi 2012 Wizara ilikumbana
na vitendo vinavyofanana na kitendo hiki na ikachukua hatua stahiki. Na kwa
tukio hili pia Wizara imechukua hatua za kidiplomasia zinazostahili ili kuzuia
jambo hili lisitokee tena.
IMETOLEWA NA:
WIZARA YA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA KIMATAIFA
18 Septemba, 2013
Dar Es Salaam.
Chama legelege huzaa Serikali legelege. Mwl. J.K Nyerere
Tumefika hapa tulipo kwa Udhaifu wa Rais Kikwete" J.J Mnyika
No comments:
Post a Comment