Wasiliana nasi : chademadiaspora@gmail.com -Fair and Balanced Platform- Twitter @ChademaDiaspora

Wasiliana nasi : chademadiaspora@gmail.com -Fair and Balanced Platform- Twitter @ChademaDiaspora
----------------------WE THANK AND APPRECIATE YOU FOR VISITING CHADEMA DIASPORA BLOG. AGAIN, THANK YOU!-----------------------

Thursday, September 19, 2013

Katiba mpya majaliwa

Wanaharakati nao wachachamaa Dar

Mchakato wa kupata Katiba mpya umeendelea kupingwa, baada ya wanaharakati kuungana na kutoa tamko la kutaka usiharakishwe huku na Rais Jakaya Kikwete, kutousaini Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Mabadiliko ya Katiba kutokana na kutokuwapo kwa uelewa mpana hususani maeneo ya ukinzani likiwamo suala la Muungano. Kadhalika, wanaharakati hao wamesema uchaguzi wa viongozi wa serikali za mitaa utakaofanyika mwakani pamoja na uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, kisiwe kichocheo cha kuharakisha upatikanaji wa Katiba mpya. Mbali na kutoa tamko hilo, wanaharakati hao walisema wanajiandaa kwenda Ikulu kumshinikiza Rais Kikwete kutosaini muswada huo sambamba na kumpatia tamko hilo litakalokuwa katika maandishi atakaporejea kutoka nje ya nchi kwa shughuli za kikazi.

        Akisoma tamko hilo jana jijini Dar es Salaam kwa niaba ya taasisi nyingine kwenye mjadala wa wazi uliojadili mada kuhusu “Tunajifunza nini kutokana na mchakato wa Katiba nchini Tanzania”, Mkurugenzi Mtendaji wa Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), Usu Mallya, alisema asasi zote nchini zisizo za serikali, zijipange upya kwa kuungana kwa lengo la kuurudisha upya mchakato wa kupata Katiba mpya. Alisema mchakato wa kupata  Katiba mpya usitishwe kwa sasa kwa lengo la kujenga uelewa zaidi wa wananchi juu ya masuala ya Katiba. Asasi zilizozoungana na kutoa tamko hilo ni pamoja na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (Tamwa), Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), TGNP, Hakielimu, Mfuko wa Wanawake Tanzania (WFT), Jukwaa la Katiba Tanzania na Policy Forum. Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba Tanzania, Deus Kibamba, alisema mchakato wa kupata Katiba mpya umeanza kushindikana kutokana na kuwapo kwa migongano kwa baadhi ya wadau.

         Alisema hamasa kwa wananchi juu ya utoaji na uelewa wa masula ya Katiba bado uko chini tangu mchakato huo ulipoanza. Kibamba alidai kuwa misingi mikuu mitano ya kutengeneza Katiba imekiukwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba. Aliyataja mambo hayo ambayo kuwa ni uelewa mdogo wa wananchi juu ya masuala ya Katiba, ushiriki mdogo wa wananchi, umilikishwaji wa Katiba kwa wananchi, uhamasishwaji wa wananchi katika kushiriki mchakato wa kutoa maoni katika Katiba na utekelezaji wa wananchi katika Katiba mpya ulikuwa duni. “Rais asisaini wala usifike kabisa muswada huo Ikulu, ningependa Rais akirudi kutoka safari zake, asiukute muswada huo Ikulu,” alisema Kibamba. Aliongeza kuwa endapo Katiba mpya haitapatikana kwa muda uliopangwa, kuna wasiwasi wa watawala waliopo madarakani kuendelea kutawala hadi pale Katiba mpya itakapopatikana.


     Alisema pia kuna wasiwasi mkubwa Katiba mpya isipopatikana, uwezekano wa kuendelea kutumika Katiba ya mwaka 1977 utakuwa mkubwa. Mkuu wa Dawati la Katiba la LHRC, Anna Henga, alisema uelewa wa wananchi wa masuala ya Katiba ni mdogo kutokana na kuchanganya na kushindwa kutofautisha Katiba na siasa. Alisema mpaka sasa wananchi wengi wanajua siasa ni Katiba na Katiba ndiyo siasa, jambo ambalo siyo kweli na kueleza kuwa siasa ipo ndani ya Katiba, lakini Katiba haipo ndani ya siasa. Alisema katika rasimu yote ya Katiba, wananchi walikuwa wanajadili mambo ya serikali tatu, Rais, Bunge la Katiba litakuwaje, mambo ambayo ni siasa pasipo kuzungumzia makundi ya kijamii. Alisema Bunge la Katiba litakuwa na wanasiasa wengi ambao ni wabunge kuliko wananchi, na kueleza kuwa wanasiasa watakuwa asilimia 72.5 na wananchi asilimia 27.


       Alifafanua kuwa kutokana na hali hiyo, mchakato wa kupata Katiba mpya umeingia dosari, hivyo Rais asiusaini muswada huo.“Tutakwenda kwa Rais kushinikiza mchakato huu usisainiwe, sheria ipo inayoruhusu hayo, tuna uwezo wa kuusimamisha kwa kipindi cha miezi sita,” alisema Henge. Naye Dk. Azaveri Lwaitama, kutoka Kigoda cha Mwalimu Nyerere, alisema shinikizo kutoka nje ya Bunge linaweza kuleta Katiba ambayo siyo makini, na kueleza kuwa rasimu imekuja na mapendekezo ambayo siyo rafiki kwa wananchi. Alisema Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba, aendelee na mchakato huu hadi mwisho pasipo watu wengine kuuendeleza kwa kuwa itasababisha uchakuaji wa Katiba hiyo.


        Aidha, alitaka kujengwa kwa uelewano baina ya Wabunge na wawakilishi wa Bunge Maalum la Katiba ili kuondoa mgangano utakaoweza kutokea. Aliongeza kuwa  asasi za serikali zilizowahi kuwasilisha maombi ya kupatikana kwa Katiba mpya miaka 10 iliyopita, zimshinikize Rais angalie uteuzi wa wajumbe watakaoingia katika Bunge la Katiba.  “Mchakato usiharakishwe, twende taratibu kwanza, Rais asisaini muswada huo, gharama tuliyoingia katika kuandaa mchakato wa kupata Katiba mpya ni kubwa, hivyo isipotee bure,” alisema Dk. Lwaitama. Mbunge wa Ubungo (Chadema), John Mnyika, alisema ni vigumu kupunguza idadi ya Wabunge katika Bunge la Katiba badala yake waongezwe wawakilishi na kuwa inawezekana.


     Alisema sheria ya kura ya maoni inayokwenda kujadiliwa katika Mkutano ujao wa Bunge itakuwa na umuhimu mkubwa kuliko ile ya Muswada wa Mabadiliko ya Katiba mpya. Wanaharakati wameungana kupinga mchakato wa Katiba siku chache baada ya vyama vya NCCR-Mageuzi, CUF na Chadema kuungana kuupinga mchakato huo na kushinikiza Rais Kikwete asiusaini Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Mabadiliko ya Katiba ya mwaka 2013. Wenyeviti wa vyama hivyo James Mbatia (NCCR-Mageuzi), Profesa Ibrahim Lipumba (CUF) na Freeman Mbowe (Chadema), Jumapili iliyopita walikutana na kukubaliana kuungana kuupinga mchakato huo kwa maelezo kuwa umehodhiwa na  Chama Cha Mapinduzi (CCM). Waliazimia kwenda kwa wananchi nchi nzima kuwaelimisha kuupinga mchakato huo na kwa kuanzia, keshokutwa watafanya mkutano wa pamoja katika Viwanja vya Jangwani.


           Juzi, viongozi hao walianza kukutana na wadau kadhaa kwa lengo la kufanya mashauriano kuhusu mchakato wa Katiba. Akizungumza kwa niaba ya wenzake, Profesa Lipumba alisema kuwa uamuzi wao wa kuungana ni kuhakikisha Katiba haitekwi nyara na chama tawala ili Watanzania wapate Katiba mpya na nzuri ambayo imewashirikisha wadau wote. Wabunge wa vyama hivyo walilazimika kutoka nje ya ukumbi wa Bunge  Septemba 4, 5, na 6 wakipinga kuendeshwa kibabe na Sheria na Kanuni za Bunge kwa kuunyima upande wa Zanzibar haki ya kushiriki katika mchakato wa Katiba mpya.


BARAZA LA VYAMA VYA SIASA KUKUTANA 


      Wakati huo huo, Baraza la Vyama vya Siasa nchini, linatarajia kukutana Zanzibar kujadili mvutano uliopo wa Katiba mpya na kutoa tamko kuhusu nini kifanyike ili kuinusuru nchi isitumbukie katika machafuko. Mwenyekiti wa baraza hilo, Peter Kuga Mziray, aliliambia NIPASHE jana kuwa mkutano huo utafanyika Septemba 24, mwaka huu, ambao pamoja na mambo mengine, wajumbe watajadili Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Mabadiliko ya Katiba uliozua vurugu Bungeni. ”Kwenye vikao na Kamati ya Katiba na Sheria, tumeeleza yote haya lakini serikali haikutusikia na sasa imefika mahali mchakato wote wa Katiba umekuwa nuksi,” alisema. Mziray alisema Rais kama atakubali kusaini muswada, ni wazi kuwa ataiingiza nchi kwenye mgogoro wa Katiba, jambo ambalo litaitumbukiza nchi katika machafuko.


       Alisema ajenda ya Katiba mpya siyo ya CCM na kuwa kinachotakiwa kufanywa na serikali ni kuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba itakapomaliza kazi zake na kukabidhiwa ripoti, makabrasha yawekwe kusubiri Rais mwingine atakayekuja aendelee na mchakato wa Katiba mpya. Aliongeza kuwa kama itaonekana kwamba kuna ulazima sana wa kupata Katiba mpya muda wa serikali ya awamu nne ukipita, iundwe serikali ya umoja wa kitaifa ambayo itaandaa Katiba mpya na uchaguzi mkuu.


Source: Ippmedia (Sept. 2013) Katiba mpya majaliwa. Retrieved from Ippmedia/Nipashe


No comments: