Wasiliana nasi : chademadiaspora@gmail.com -Fair and Balanced Platform- Twitter @ChademaDiaspora

Wasiliana nasi : chademadiaspora@gmail.com -Fair and Balanced Platform- Twitter @ChademaDiaspora
----------------------WE THANK AND APPRECIATE YOU FOR VISITING CHADEMA DIASPORA BLOG. AGAIN, THANK YOU!-----------------------

Wednesday, September 25, 2013

UJAMBAZI WA KIKATIBA: Ubabe, jeuri na vitisho vya CCM


Bakari M. Mohamed

MAKALA

           MEI 30 mwaka jana niliandka mada iliyobeba anuani ya ‘Mchakato wa Katiba: CCM imepora haki ya wananchi,’ ambayo kwa sehemu kubwa ililenga kuonesha jinsi Chama Cha Mapinduzi (CCM) kinavyotumia nguvu ya wenzo (leverage) kufikia utashi wa kutawala na kumiliki mchakato wa upatikanaji wa katiba mpya ya Tanzania. Ukweli umeanza kusadifu kwa jinsi CCM ilivyotumia ubabe, jeuri na vitisho kuelekea kwenye hatua za mwisho za upatikanaji wa katiba mpya kwa misingi ya uporaji wa uhuru, haki, usawa wa wananchi. Wananchi wameporwa uhuru, haki na usawa katika ushirikishwaji wa moja kwa moja katika mchakato wa uundwaji wa katiba. CCM ilijitenga na uandikaji wa katiba mpya, ndiyo maana hata aliyekuwa Waziri wa Sheria, Celina Kombani wakati mmoja alidiriki kusema “hakuna haja ya katiba mpya kwa sasa.”

          CCM haikuwa na nia ya dhati ya kupatikana kwa katiba mpya yenye kuzingatia misingi ya uhuru, haki, usawa, uadilifu na insafu. CCM ilijiweka, na imeendelea kujikita kwenye njia ya kimkakati kulinda nguvu zake kufikia utashi wake wa kutawala siasa na michakato ya kuviza fikra ya uandikaji wa katiba mpya itakayotokana na maoni ya wananchi. CCM imezoea ubabe wa matumizi ya nguvu za kidola, na kuwa mstari wa mbele kuendesha propaganda dhidi ya uhuru, haki, usawa, uadilifu na insafu inayodaiwa na wananchi kupitia kwa wawakilishi wa wananchi, japo kwa uchache wao kwenye Bunge. Wingi wa wabunge wa CCM bungeni ndio unaowapa jeuri viongozi waandamizi kupitisha kwa mambo watakavyo pasipo kuzingatia maoni ya wachache yenye hoja zenye mantiki.

           CCM,  iliyopora haki ya wananchi kwa kutumia kundi la watu wachache wenye umiliki wa chama, imefanya ujambazi wa kutisha kwa kulitumia Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa wabunge wake ambao huchukuliwa kama sehemu ya chama ndani ya Bunge kwa wingi wao kufanya maamuzi kana kwamba wao ndio wenye hakimiliki ya Tanzania. Huu ni ulevi mbaya sana wa matumizi ya nafasi nyeti ya wingi usiozingatia maslahi mapana ya nchi. CCM, kwa jeuri iliyopindukia mipaka, wanafanya vile wanavyotaka kwa vile hakuna nguvu za ndani zilizo tayari kupinga mfumo wa ubabe na jeuri inayotumiwa na baadhi ya viongozi wa CCM ndani na nje ya mduara (msonge) wa uongozi na menejimenti ya chama hicho. Tabia ya baadhi ya viongozi wahafidhina wasiotaka mabadiliko ndani ya CCM umekifanya chama hicho kuwa kama ‘zimwi’ lenye tamaa na uchu wa kula nyama za watu.

         Ni mfano wa simulizi ya hadithi ya ‘Mfalme Binta’ kwenye kitabu cha Lila na Fila. CCM kwa hili, inaonyesha wazi ni kwanini haikutamani Tanzania ipate katiba mpya itakayozingatia uhuru, haki na usawa wa wananchi wote. CCM inatumia mbinu zilezile za mbuni kuficha kichwa mchangani ilhali mwili wote upo nje. Kilichotolewa na Tume ya Jaji Warioba kimewatia kiwewe na kutamani kutumia ubabe, jeuri na vitisho kuzima harakati za upatanaji wa katiba ya wananchi. CCM imejiweka kwenye nafasi ileile ya matumizi ya ubabe, jeuri na vitisho. Ukweli ni kwamba; ubabe ni ushamba, na jeuri ni ushenzi kwa kuwa hakuna mwanzo usiokuwa na mwisho. Na mwisho wa ubabe na jeuri ya CCM ni wananchi kuchukua nafasi yao ya kuwa msingi wa mamlaka ya nchi.

         CCM wameachiwa muda mrefu kupora uhuru, haki na usawa wa wananchi. Muda wa miaka 50 tangu TANU/ASP na baadaye CCM, wananchi wamekuwa wakitungiwa katiba. Wakati huu wananchi wamebadilika na ni wepesi kubadilika wanapopewa elimu na taarifa sahihi juu ya mustakabali wa maisha yao. CCM, kama chama kilichozeeka na chenye fikra za kibabe, kitambue kwamba wananchi wa miaka ile ya baada ya uhuru hawafanani kabisa na wa zama hizi ambazo elimu ya uhuru, haki na usawa imepanuka na inapatikana kwa uwazi zaidi tofauti na propaganda za enzi zile. Inakuwaje chama kinachojinasibu na Matokeo Makubwa Sasa (BRN) kishindwe kutumia ‘akili kubwa’ kutambua na kuona umuhimu wa utashi wa wananchi juu ya katiba mpya itakayozingatia maslahi mapana na makubwa ya wananchi wote kwa sasa na baadaye?

        Binafsi, kama mchambuzi wa masuala ya siasa, jamii na uchumi, nimeshindwa kupata majibu ya moja kwa moja juu ya kwanini CCM hawataki mabadiliko ya katiba. Je, viongozi wa CCM hawataki kwa kuwa hawajui kwamba wananchi wa Tanzania wamechoka na mfumo wa sheria unaoatamizwa na fikra mgando za baadhi ya viongozi waliochoka akili na wasiokuwa na fikra mpya? Au, ndio kusema CCM imekosa watu wenye uoni angavu unaoweza kuona yanayotokea kwenye mazingira ya siasa na mabadiliko yanayotarajiwa kwenye mwendo wa siasa za ndani na za nje? Kama alivyowahi kuandika mwanasaikolojia Al-Naraqi (1997), kwamba ‘mtu anaweza kuwa na upumbavu mchanganyiko na asijijue kwamba ni mpumbavu na anatamani upumbavu wake uwe sawa na watu wengine.’

            Upumbavu wa akili ni ugonjwa mbaya sana hususan pale mpumbavu anavyodhani kwamba anavyodhani yeye ndivyo wanavyodhani watu wengine. Hata ukiichukua akili ya mwendawazimu na kuisoma, kuna asili ya akili kiasi iliyosalimika na ukichaa na ndiyo kusema kila mtu ni kichaa wa jinsi yake (kama alivyowahi kuandika mwanasaikolojia Sigmund Freud). Tunaweza kusema CCM ni chama kinachoendesha siasa zake kwa njia ya unafiki na uzandiki; upande mmoja kinaweka ahadi kana kwamba imekubali katiba mpya, ilhali upande mwingine hawaitaki. Hivi ndiyo kusema kwamba, ‘maneno na matendo ya mtu yasipochimbuka kwenye kiini cha moyo na kwenye moyo mweupe, hayawezi kuwa na thamani yoyote.

         Sayyid Mujtaba Musawi Lari (1992) anaonesha kwamba shakhsia (haiba) ya mtu kisiasa hujengwa na maneno yanayoambatana na matendo yanayoakisi kwenye utekelezaji wa ahadi kwa pamoja na ndiyo maana Waswahili walisema ‘matendo hukidhi haja maridhawa kuliko maneno.’ Kwa jinsi ya sifa za kisiasa, CCM wamepoteza haiba ya kisiasa na wamechukua njia mbaya kuendesha siasa kwa ubabe, jeuri na vitisho vya kisiasa. CCM ambao hata kwa uwiano hawazidi nusu ya raia wote wenye uwezo wa kupiga kura, wanatumia nafasi ya mamlaka yao kutia munda nguvu yao kwenye uamuzi wenye taathira kwa nchi yote. 

        Hata kama CCM imekuwa chama dola kwa muda mrefu, si hakimiliki inayowapa uthubutu wa kuendesha vitendo vinavyoleta songombingo na hamkani ya kisiasa katika mazingira yanayohitaji utumizi mkubwa wa akili, maarifa na hekima ya hali ya juu. Uamuzi wa kipumbavu na au kiwendawazimu utakaofanywa na yeyote kwenye utatu wa serikali; yaani, Bunge, Mahakama na Serikali (Rais) utaliweka taifa njiapanda. Ni matarajio ya wananchi wengi wanaopenda uhuru, haki na usawa kwa misingi ya umoja na amani ya Tanzania, kwamba mchakato wa upatikanaji wa katiba mpya kwa sehemu nyeti na muhimu zilizobaki utakamilishwa kwa njia ya uhuru, haki na usawa pasipokuwa na hamkani na sintofahamu za kisiasa zinazoweza kuleta uvunjifu wa utulivu wa kisiasa.

       Hakuna sababu kwa CCM kung’ang’ania uhafidhina wa ‘wingi’ ilhali kila mwananchi wa Tanzania ana uhuru, haki na usawa katika ujenzi wa siasa, jamii na uchumi. Katiba ni mali ya wananchi wote pasipokuwa na ushawishi wa kundi lolote lenye hakimiliki ya kupora uhuru, haki na usawa wa watu wengine. Ubabe, jeuri na vitisho vya CCM si sehemu ya ustaarabu wa siasa kwa zama hizi; viongozi wa CCM waache uhafidhina, wabadilike.

No comments: