Wasiliana nasi : chademadiaspora@gmail.com -Fair and Balanced Platform- Twitter @ChademaDiaspora

Wasiliana nasi : chademadiaspora@gmail.com -Fair and Balanced Platform- Twitter @ChademaDiaspora
----------------------WE THANK AND APPRECIATE YOU FOR VISITING CHADEMA DIASPORA BLOG. AGAIN, THANK YOU!-----------------------

Wednesday, September 25, 2013

JK akwama, CCM kitanzini


  
        HATUA ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kupuuza agizo la Rais Jakaya Kikwete la kusitisha tozo la sh 1,000 kwa laini za simu (simu card), limeiweka serikali katika wakati mgumu, huku wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wakishutumiwa kwa kuwadanganya Watanzania. Hali hiyo imetokana na hatua ya TRA kuziagiza kampuni za simu kuhakikisha kuwa zinaanza kutoza kodi ya laini za simu kwa miezi mitatu tangu Julai hadi Septemba, kwa wananchi wote wanaomiliki laini za simu. Barua hiyo iliyosainiwa na Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato, Harry Kitilya, Septemba 12, mwaka huu kwenda kwa wakurugenzi wa Vodacom, Airtel, MIC Tanzania Ltd, Kampuni ya Mawasiliano Tanzania na Dovetel Tanzania inazitaka kampuni hizo zilipe tozo hiyo.

        “Sheria ya fedha ya mwaka 2013 ilianzisha kodi ya laini za simu  na gharama za kutuma na kupokea pesa, tarehe ya utekelezaji ilipaswa kuanza Julai 1, mwaka huu… tumepitia kumbukumbu za makusanyo yetu kupitia sheria  hiyo mpya ya fedha ya mwaka 2013, tunasikitika kuwa malipo haya hayakufanyika, tunahitaji malipo hayo yafanyike ndani ya siku 14,” ilisema barua hiyo. Hata hivyo katika barua yao ya Julai 5, kwenda kwa Kitilya, Umoja wa Kampuni hizo (MOAT),  umeeleza kushangazwa kwao na hatua hiyo ya TRA, huku ukitambua kuwa agizo hilo limesitishwa na linafanyiwa uchambuzi. Aidha, kampuni hizo zimekiri kuwa hatua ya kuwataka kuwakata tozo wateja wao ni mbaya na itaongeza ugumu wa maisha kwa wananchi.


     “Tunaelewa kuwa lengo la tozo hii ni kuongezaza mapato, lakini kampuni za simu zimesajiliwa na zinalipa kodi kupitia TIN ya kila kampuni, njia hii ya kutoza kodi laini za simu itaongeza ugumu katika serikali kufikia malengo yake,” kampuni hizo zilisema. Zilisema hata huduma iliyokuwa inatamkwa na serikali haikupewa ufafanuzi wa kutosha, kwani kampuni za simu ziliweka bayana kuwa huduma ya kuweka pesa ilikuwa haitozwi kodi, hivyo serikali ilipaswa kufafanua wanapotaja huduma za simu walimaanisha huduma zipi, jambo ambalo serikali haikufanya hadi TRA walipodai kuanza malipo hayo. Hatua ya TRA imepokewa kwa hisia tofauti na Watanzania wa kada mbalimbali, huku lawama zikisukumwa kwa wabunge wa CCM kwa kutumia mbinu za ‘funika kombe’ baada ya kuona hoja ya Mbunge wa CHADEMA, Halima Mdee, ingezua balaa bungeni.

         Kuzuka kwa mjadala huo mzito ulimsukuma Rais Jakaya Kikwete kuagiza serikali kukutana na kampuni za simu kuangalia namna ya kushughulikia jambo hilo, huku Katibu wa Itikadi na Uenezi wa chama hicho, Nape Nnauye, akijigamba kuwa serikali ya CCM ni sikivu, na kwamba suala hilo halitatekelezeka. Uamuzi huu mpya wa TRA ni uthibitisho kuwa kauli za Rais Jakaya Kikwete, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda na viongozi wengine wa CCM zinaonekana kama zilizokuwa na lengo la kupunguza jazba za wananchi na wadau mbalimbali waliopaza sauti zao kupinga tozo hiyo muda mfupi baada ya Bunge la mwezi Julai. Wachambuzi wa siasa wanasema  CCM walifahamu mapema tozo hiyo ni mwiba kwao, siku ya kusomwa kwa bajeti kuu ya serikali, Waziri wa Fedha na Uchumi, William Mgimwa, alilazimika kufuta pendekezo la awali katika kifungu (C ) (viii) cha marekebisho ya sheria ya ushuru wa bidhaa, sura 147, akisema kimefanyiwa marekebisho.

            Katika kikao cha Bunge la Bajeti, wabunge wengi walizima hoja binafsi ya Mbunge wa Kawe, Halima Mdee, ambayo pamoja na mambo mengine ilisema: “Jambo la kusikitisha ni kwamba, kipengele kilichokuwa kinapendekeza kodi ya shilingi 1,450 kwa kila laini ya simu, ambacho Waziri wa Fedha alilitangazia Bunge kwamba kimefutwa kilirejeshwa kinyemela (ila kikiwa na pendekezo la shilingi 1,000), na kwa kuwa wabunge walishatangaziwa na waziri wa fedha kuwa kipengele hicho kimefutwa, walipiga kura ya ndiyo kupitisha sheria hiyo bila kujua kwamba kipengele kile kilirudishwa kinyemela. Kwa mujibu wa Mdee, tukio hilo lilidhihirisha kwamba serikali ililihadaa na kulidanganya Bunge, hivyo kufanya maamuzi yasiyo sahihi, na viongozi wa CCM walihadaa wananchi kwa majibu mbalimbali nje ya Bunge. Mbali na tozo hiyo kwenye laini za simu, serikali pia inatoza ushuru wa bidhaa wa asilimia 14.5 kwenye huduma zote za simu za kiganjani badala ya muda wa maongezi.

          Suala ambalo wananchi wengi hawajagundua ni kodi ya zuio ya asilimia 10 ya kamisheni ya usafirishaji wa fedha kwa njia ya simu za mikononi, yaani M-Pesa, Tigo-Pesa, Aitel Money na Easy Pesa. Licha ya Waziri Mgimwa kusema ushuru wa bidhaa kwenye simu hautatozwa kwenye huduma za kutuma na kupokea fedha, tayari makali hayo yameshaanza kuwasulubu  watumiaji wa simu tangu Julai, kwani kampuni hizo zimeongeza tozo kwenye huduma hizo za kutuma na kupokea fedha. Wakati Nape akisema kuwa CCM inataka serikali ifute kodi hiyo kwa madai kuwa ni mzigo kwa walalahoi, Pinda alidai fedha hizo zitakazokusanywa zilipangwa kuingizwa REA ili kusambaza umeme vijijini. Kauli ya Pinda inakinzana na maelezo ya Waziri wa Fedha bungeni, ambapo alisema kuwa fedha zitakazopelekwa REA ni zile za tozo mpya ya mafuta ya petroli (petroleum levy) ya sh 50 kwa lita, ambayo itakusanywa na TRA.

Source:Isango J. (Sept. 2013).JK akwama, CCM kitanzini. Retrieved from Tanzania Daima

No comments: