Wasiliana nasi : chademadiaspora@gmail.com -Fair and Balanced Platform- Twitter @ChademaDiaspora

Wasiliana nasi : chademadiaspora@gmail.com -Fair and Balanced Platform- Twitter @ChademaDiaspora
----------------------WE THANK AND APPRECIATE YOU FOR VISITING CHADEMA DIASPORA BLOG. AGAIN, THANK YOU!-----------------------

Wednesday, September 25, 2013

Malaysia na Tanzania: kuelekea Maisha bora dhidi ya kuelekea Ufukarishwaji kupitia Kilimo


Zitto Kabwe
Wakati Jamhuri ya Tanganyika inapata Uhuru mwaka 1961, Nchi ya Malaya ilikuwa tayari ina uhuru miaka mine kabla. 1957. Malaya ilijiunga na Singapore, Sabah na Sarawak tarehe 16 Septemba mwaka 1963 kuunda Malaysia. Tanganyika ilijiunga na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar kuunda Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwaka miezi saba baadaye. Hata hivyo Singapore ilifukuzwa kutoka katika Muungano wa Malaysia mwezi Agosti mwaka 1965 kutokana na kutofautiana kwa sera kuhusu watu wa asili na namna ya kuwalinda kiuchumi. Viongozi wa Kuala Lumper walitaka kuweka sera za kusaidia wazawa kwa kuwapa upendeleo maalumu wakati viongozi wa Singapore chini ya Lee Kuan Yew walitaka kuwepo na Malaysia moja kwa wote bila upendeleo maalumu kwa Bumiputera (son of the soil). Singapore ina wakazi wengi zaidi wahamiaji kutoka China. Tanzania imeendelea kudumu na Muungano licha ya changamoto kadha wa kadha zinazoukabili muungano huo. Tanzania na Malaysia zote zilitaliwa na mkoloni Mwingereza.
Wakati Tanzania inapata inaundwa mwaka 1964 pato la wastani la mtu mmoja lilikuwa dola za Marekani 63 wakati Malaysia ilikuwa na pato la dola za Marekani 113 Kimsingi nchi hizi zilikuwa sawa kimaendeleo ingawa Tanzania ni kubwa kwa zaidi ya mara tatu ya Malaysia. Hivi sasa Malaysia kipato cha wastani cha mwananchi ni dola za Marekani 10,000 na Tanzania ni dola za Marekani 600. Kwa Tanzania pato la wastani limeongezeka mara kumi takribani na kwa Malaysia limeongezeka mara elfu moja. Nini tofauti ya mikakati ya maendeleo ya nchi hizi mbili?
Leo tutaangalia eneo moja tu la Kilimo na namna Kilimo kilivyoweza kuivusha nchi ya Malaysia na Kilimo hicho hicho bado hakijaweza kuivusha Tanzania. Malaysia iliunda Shirika la Umma linaloitwa Federal Land Development Authority (FELDA) likiwa na wajibu mmoja mkubwa wa kuhakikisha wananchi masikini wanapata ardhi, wanalima kisasa na kuongeza uzlishaji kasha kufuta umasikini. Kila mwananchi masikini aligawiwa ardhi hekta 4.1, ardhi ikasafishwa na kuwekwa miundombinu yote muhimu, ikapandwa michikichi na Mwananchi akapata huduma za ugani ili kukuza michikichi hiyo. Shughuli zote hizi zilifanywa kwa gharama za Serikali na wananchi wale wakapewa kama mkopo ambao walikuwa wanaulipa kidogo kidogo kila wanapovuna na kuuza ngazi/mawese kwa Shirika hili la Serikali. Hivi sasa Shirika hili ni kubwa sana, lina thamani ya dola za kimarekani bilioni 3.5 na kupitia Ushirika wao wananchi hawa waliopewa ardhi ya kulipa michikichi sasa wanamiliki asilimia 20 ya Shirika hili. 
Malaysia iliweza kuondoa umasikini kutoka asilimia 57  ya wananchi wanaoishi kwenye dimbwi la umasikini mwaka 1965 mpaka chini ya asilimia 3 mwaka 2012.  FELDA sasa ni Shirika la kimataifa maana linaanza kuwekeza duniani kote. FELDA ilipouza hisa zake kwenye masoko ya mitaji, IPO  yake ilikuwa ni ya tatu kwa ukubwa baada ya Facebook na Japanese Airlines. Shirika la Umma linalomilikiwa na Serikali, Wakulima na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (EPF) na linaloendeshwa kwa misingi ya utawala bora wa makampuni limeweza kufuta umasikini kwa zao moja tu la Michikichi. Malaysia leo inaongoza kwa kuuza Mawese duniani. Michikichi hiyo ilitoka Kigoma, Tanzania na kupelekwa Malaya na Waingereza miaka ya hamsini.
Tanzania nasi tulikuwa na Shirika la Umma kwa ajili ya Kilimo. Leo tuchukulie Shirika la NARCO. Kama FELDA, NARCO walichukua ardhi kubwa maeneo kadhaa nchini. Tofauti na FELDA wao walilima wenyewe mashamba haya na kuweka miundombinu ya kilimo. Tuchukulie mfano wa Mashamba ya mpunga kule Kapunga, wilaya ya Mbarali mkoa wa Mbeya. Mwaka 1985 NARCO walikwenda kijijini Kapunga kuwaomba wananchi wawape ardhi ya kulima mpunga. Wananchi wakawapa hekta 3000 hivi kwa mujibu wa muhtasari wa mkutano mkuu wa Kijiji nilionyeshwa mwaka 2009 nilipoenda kutembelea mashamba haya kufuatia mgogoro wa ubinafsishaji. NARCO wakapata msaada kutoka Serikali ya Japani na uwekezaji mkubwa ukafanyika ikiwemo kuweka kinu cha kukoboa mpunga cha kisasa kabisa. Hata hivyo NARCO ilijiendesha kwa hasara na ilipofika kati kati ya miaka ya 90 ikaamuriwa kubinafsishwa. NARCO ikauza mashamba yale kupitia Mpango wa ubinafsishaji kwa kampuni binafsi. Katika uuzaji huo NARCO waliuza hekta 3500 badala ya 3000 walizopewa na wananchi. Kwa maana hiyo Kijiji cha Kapunga nacho kiliuzwa!
Mifano hii miwili inaonyesha tofauti kubwa za kifikra kimaendeleo kati ya nchi zetu hizi mbili. Moja iliwezesha wananchi kumiliki ardhi na imefanikiwa. Nyingine iliamua kufanya kupitia Shirika la Umma na baada ya kushindwa, badala ya kurejesha ardhi kwa wananchi na kuwawezesha kulima, ardhi ile ikauzwa kwa kampuni ya mtu mmoja. Mfano wa Kapunga upo pia huko Wilayani Hanang kwenye mashamba ya Ngano ya Basotu nk. Hata kwenye mpango wa SACGOTT bado fikra ni za wakulima wakubwa wenye mashamba makubwa badala ya kuwezesha wananchi kumiliki ardhi na kulima kwa mfumo ambao huduma zitatolewa kwa pamoja. Ujamaa wa Malaysia ulikuwa ni wa kumilikisha wananchi wao ardhi na kuwawezesha kuzalisha. Ujamaa wetu ulikuwa ni wa kumiliki kwa pamoja na hivyo kukosa uwajibikakaji. Badala ya kuboresha tunaona bora kwenda kwa wakulima wakubwa na kugawa ardhi hovyo bila mpango.
Hatuwezi kujifunza kwa wenzetu kweli? Lini tutaacha umazwazwa?

No comments: