Wasiliana nasi : chademadiaspora@gmail.com -Fair and Balanced Platform- Twitter @ChademaDiaspora

Wasiliana nasi : chademadiaspora@gmail.com -Fair and Balanced Platform- Twitter @ChademaDiaspora
----------------------WE THANK AND APPRECIATE YOU FOR VISITING CHADEMA DIASPORA BLOG. AGAIN, THANK YOU!-----------------------

Thursday, September 19, 2013

SABABU ZA KUUNGA MKONO SERIKALI TATU NI HIZI


     Chama Cha Mapinduzi (CCM), kimeamua kufia kwenye hoja yake ya muundo wa Muungano wa serikali mbili. Vikao vya juu vya chama hicho - Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) na Kamati kuu (CC) - vilivyofanyika mwezi uliopita mjini Dodoma, vimesisitiza umuhimu wa kuendelea na Muungano wa serikali mbili kwa madai kuwa hiyo ndiyo sera ya chama hicho. Hata andishi la CCM, lililowasilishwa kwenye Tume ya Mabadiliko ya Katiba, limepinga mapendekezo ya kuwapo kwa serikali tatu ndani ya Jamhuri ya Muungano. Andishi linasema, mwarobaini wa matatizo ya Muungano, siyo kuwapo kwa serikali tatu bali serikali mbili.

       Katika kutetea mfumo wa serikali mbili, chama hicho kimejikita kwenye hoja tatu: Kwanza,muundo wa Muungano wa serikali tatu ni kinyume cha makubaliano yaliyofikiwa Aprili 1964 na waasisi wa Muungano, Mwalimu Julius Nyerere na Abeid Aman Karume. Pili, Muungano wa serikali tatu utaongeza gharama serikalini; utaingiza nchi kwenye umaskini na utasababisha Zanzibar kushindwa kuchangia uendeshaji wa serikali ya pamoja. Hoja inayojengwa ni kwamba mapato ya Zanzibar ni madogo ukilinganisha na Tanganyika. Tatu, mfumo wa Muungano wa serikali tatu, siyo sera ya chama hicho tawala. Kinasema sera ya CCM ni serikali mbili kuelekea serikali moja. Inadai kuwa mfumo wa serikali tatu unahatarisha uhai wa Muungano.

        Ukichunguza hoja hizi za kupinga Muungano wa serikali tatu na utetezi wa serikali mbili,waweza kuona jinsi chama hiki kinavyozeeka kwa kasi; kinashindwa kufikiri,kuchambua na kutafiti. Kwa mfano, kinachoelezwa na CCM kuwa "....umuhimu wa kuendeleza mfumo wa serikali mbili," hakichambui madhara yaliyosababishwa na mfumo huo kwa miaka 49 iliyopita; au madhara yake katika siku zijazo. Hakijielekezi kutafuta njia mbadala ya kutatua matatizo yaliyopo; wala jinsi ya kupata suluhu ya manung'uniko ya washiriki wa Muungano. Hoja zote za chama hiki zinaishia kwenye kauli rejareja za ukubwa wa gharama; taifa kurudi nyuma; hofu ya kuvunjika kwa Muungano na inachoita, "kinyume na makubaliano ya waasisi wa Muungano ya mwaka 1964." Basi!

         Nani amekiambia chama hiki kuwa Muungano ni suala la sera za vyama? Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ulifungwa mwaka 1964. Vyama vya Afro Shirazi Party (ASP) na Tanganyika African National Union (TANU) viliungana mwaka 1977 - miaka 13 baada ya Muungano. Wala Muungano hauwezi kudumu kwa kisingizio cha sera ya chama. Waweza kudumu kwa wananchi kukubaliana kwenye muundo na mfumo. Utadumu kwa kukubaliana kipi kiwe cha Muungano na kipi kiondoke. Muungano hauwezi kuvunjika kwa kubariki mfumo wa serikali tatu. Utaweza kuvunjika ikiwa CCM itawalazimisha wananchi kuwa watumwa wa kubakia kwenye serikali mbili.

       Kabla ya CCM kujitosa katika upinzani wa serikali tatu kwa kusema, "ni kinyume na makubaliano ya mwaka 1964," kingejipa muda wa kupitia, angalau kidogo rasimu ya katiba. Kwa kufanya hivyo kingeweza kugundua kuwa hakuna mahali kwenye rasimu iliyotolewa, kunakoonesha wananchi wanajadili katiba ya mwaka 1964. Kilichoelezwa ni mjadala wa katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano, toleo la mwaka 2014. Hivyo basi, kusingizia muundo wa Muungano wa serikali tatu, ni kinyume na makubaliano ya mwaka 1964; ni kujichosha bure. Aidha, katiba inayojadiliwa haielekezi iwapo wananchi wanataka Muungano au hawataki. Haielekezi mjadala wa kuwapo au kutokuwapo kwa Muungano. Rasimu inajadili namna bora ya kuboresha Muungano. Inajadili ambavyo Muungano utadumu.

       Lakini kuna hili pia: Hata tukikubaliana kuwa Muungano wa mwaka 1964 ulikuwa ni serikali mbili, bado yaliyomo kwenye Muungano wa sasa ni tofauti na yale yaliyokubaliwa wakati huo. Muungano wa mwaka 1964 ulikuwa na mambo 11. Sasa yameongezeka hadi kufikia 22. Nani ameongeza na kwa ruhusa ya nani? Yameongezwa na Nyerere na Karume? Hapana! Yamepachikwa baada ya Karume kufariki dunia. Mfumo wa serikali tatu unaopingwa na viongozi wa CCM kwa kisingizio cha gharama ni nafuu zaidi ukilinganisha na ule wa serikali mbili. Tofauti na mfumo wa serikali mbili, kwenye muundo wa serikali tatu, kumeainishwa  yapi mambo ya Muungano na yapi yasiyokuwa ya Muungano. Kumeoneshwa idadi ya mawaziri,mkatibu wakuu, naibu makatibu wakuu na wengineo.

      Ni tofauti na sasa, ambako mambo ya Tanganyika yamefinyangwa na kuingizwa katika Muungano. Mfumo wa serikali tatu, utazuia rais wa Muungano kumega nchi vipande kwa kisingizio cha kupeleka maendeleo karibu na wananchi. Uhuru bandia wa kuipa Zanzibar mamlaka kamili bila kuwapo serikali ya Tanganyika hauwezi kuwa suluhu. kinachoweza kuitwa Zanzibar yenye mamlaka kamili kitapatikana kwa kuwapo serikali ya Tanganyika na si vinginevyo.

CCM ilikotufikisha panatosha. Huu basi ndio wakati mwafaka wa kusema "Hapana!"

Source: Gazeti la Mawio

No comments: