MSAJILI wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji Francis Mutungi ameunga mkono hatua iliyochukuliwa na serikali kupitia Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa kukemea kitendo cha Chama Cha Mapinduzi (CCM) kumtumia Balozi wa China nchini kwenye shughuli za kisiasa. Onyo hilo la msajili linakuja siku chache tangu Wizara ya Mambo ya Nje ikiri kuwa balozi huyo, Lu Youqing alivunja mkataba wa kimataifa wa Vienna unaoongoza uhusiano wa kidiplomasia na kuahidi kuchukua hatua. Wakati CCM ikizidi kukemewa, Katibu wake wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye amekuwa akifanya jitihada za kujitetea bila mafanikio kwa kukishambulia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kilichoibua sakata hilo, akidai kwamba kinaona wivu.
Katika taarifa ya msajili iliyotolewa kwa vyombo vya habari jana, Jaji Mutungi alisema kuwa kama mlezi wa vyama vya siasa anakemea kitendo cha CCM kumshirikisha balozi huyo katika shughuli za kisiasa. “Katika tukio hilo ambalo CCM iliruhusu raia wa kigeni kutumia jukwaa lake, ni dhahiri limezua hali ya taharuki kwa wananchi. Sheria ya vyama vya siasa kwa upande wake iko kimya katika suala hilo,” alisema. Aliviasa vyama vya siasa kwa ujumla wake kuzingatia na kufuata sheria na utaratibu stahiki katika utekelezaji wa shughuli zao za kisiasa. “Aidha, napenda kuujulisha umma kwamba ofisi yangu kwa sasa ipo kwenye mchakato wa marekebisho ya sheria husika ya vyama vya siasa, ambayo imebainika kuwa na upungufu, na lengo ni kukabiliana na changamoto zilizopo ikiwamo suala hili lililojitokeza,” alisema.
Wakati huo huo, CHADEMA imeitaka CCM kufuta kauli yake kwa umma ya utetezi wa kumtumia Balozi wa China, vinginevyo wananchi wataamini kwamba serikali imefanya hivyo ili kupunguza makali ya hasira. Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Mawasiliano na Uenezi wa CHADEMA, John Mnyika, pia balozi huyo naye anapaswa kujitokeza kuomba radhi kwa umma. Jumatatu wiki hii, CHADEMA kupitia kwa Mkurugenzi wake wa Mambo ya Nje, Ezekiel Wenje ilisema kuwa Balozi Youqing, alikiuka mkataba wa kimataifa wa Vienna kwa kuanza kushiriki kazi ya uenezi wa siasa za CCM mkoani Shinyanga. Kwamba Septemba 12 mwaka huu, balozi huyo alihudhuria mkutano wa hadhara wa CCM uliofanyika Uwanja wa Shycom mkoani humo na baadaye katika eneo la mnada wa Mhunze jimboni Kishapu.
Balozi Youqing alitambulishwa kwa wananchi na Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, na kisha kuwahutubia akisema China imevutiwa na sera za CCM, na hivyo itawekeza katika soko la pamba katika mkoa huo. Ni katika mkutano huo, balozi huyo alicheza nyimbo za CCM za kubeza vyama vya upinzani huku akiwa amevalia kofia ya chama hicho. Wenje alisema balozi huyo alikiuka kifungu cha 41 (i) cha mkataba Vienna kuhusu mambo ya kidiplomasia ambacho kinakataza mabalozi wa nchi kujiingiza katika masuala ya ndani ya nchi nyingine. Katika utetezi wake, CCM kupitia kwa Nape ilisema kuwa ziara ya balozi huyo mkoani humo haikuwa ya kisiasa bali ilitokana na mazungumzo kati ya chama hicho na Chama cha Kikomunisti cha China.
Alisema kuwa lengo lilikuwa ni China kuweza kuwekeza katika kilimo cha pamba na mifugo kuongeza ajira. “Katika suala hilo CCM ilikuwa nyuma ya kuhamasisha wawekezaji. Katibu wetu alipokwenda China aliomba wawekezaji na watawekeza katika viwanda kumi, na sasa wameanza na vitatu, ndiyo sababu Balozi wa China alienda kumwonyesha Kinana,” alisema. Nape aliongeza kuwa balozi huyo alipita katika mkutano wa hadhara na kuomba kusalimia wananchi kuelezea uwekezaji utakaofanywa na China.
Source: Bani A. ( Sept. 2013). Jaji Mutungi aanza na CCM. Retrieved from Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment