HATUA ya vyama vya upinzani kuungana dhidi ya chama tawala cha CCM, kupinga kupitishwa kwa sheria ya mabadiliko ya Katiba imekuwa moto kwa mwenyekiti wake, Rais Jakaya Kikwete, Tanzania Daima Jumatano limebaini. Habari za kuaminika kutoka ndani ya CCM zimesema kuwa hatua ya muungano wa vyama hivyo vilivyoonekana kuwa hasimu: CUF, CHADEMA na NCCR-Mageuzi, imeushtua uongozi wa juu wa CCM na kwamba ukimya wa Rais Kikwete umezidisha hofu kwa chama hicho. Mwenyekiti wa CUF, ambaye pia ni mwenyekiti wa Kamati ya Maridhiano ya vyama hivyo vitatu, Ibrahim Lipumba, alisema jana mara baada ya kumaliza kikao na Jukwaa la Katiba Tanzania kilichodumu kwa takriban saa tatu, kwamba hawana sababu ya kukutana na Rais Kikwete badala yake wamemtaka asitishe utiaji saini muswada wa sheria uliopitishwa na wabunge wa CCM mjini Dodoma hivi karibuni.
“Leo (jana) tumeanza na Jukwaa la Katiba, kesho (leo) tutakutana na taasisi inayowaunganisha walemavu, Alhamisi tutakutana na Ashura ya Maimamu, kisha Ijumaa tutakutana na BAKWATA pia na viongozi wa madhehebu ya Kikristo, asasi zisio za kiserikali, taasisi za wanafunzi, vyama vya wakulima kwa kuwa suala hili ni la Watanzania wote,” alisema Profesa Lipumba.
Kwa upande wake mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba Tanzania Deus Kibamba alisema kuwa walishatoa angalizo kuwa mchakato huo uko njia panda. Kibamba alisema kama kiongozi wa upinzani bungeni ambaye ni Mwenyekiti wa CHADEMA Freeman Mbowe angeruhusiwa kutoa hoja yake bungeni, suala hilo lingeupeleka mchakato huo vizuri zaidi. “Tutaendelea kutoa elimu ya uraia, tutaunga mkono jitihada zinazofanywa kuhusu mchakato huu,” alisea Kibamba.
Source: Ngowi L. (Sept. 2013). Moto wa katiba kumtesa JK. Retrieved from Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment