WAFUASI WA CHADEMA MAHUTUTI
WAKATI hali za wanachama wawili wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) zikiwa mbaya na kulazimika kulazwa katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando mkoani Mwanza, Jeshi la Polisi mkoani Mtwara linadaiwa kuwakamata na kuwapa kipigo kikali baadhi ya wanachama na viongozi wa chama hicho mkoani humo. Habari zilizothibitishwa kutoka mkoani humo, zinadai kuwa wafuasi wa CHADEMA walikamatwa na wanashikiliwa kwa madai ya kutengeneza vipeperushi vya kuhamasisha watu wasihudhurie mbio za mwenge wa Uhuru. Hata hivyo, habari zinasema kuwa polisi waliwakamata viongozi na wanachama hao baada ya kuitisha mikutano ya ndani, wakawapiga na kuharibu baadhi ya mali za wananchi. Taarifa zinadai kuwa Septemba 11, 2013 viongozi wa wilaya ya Liwale wa CHADEMA walikwenda kwenye kijiji cha Lwelu kilichoko kata ya Jangwani ili kuwatangazia wanachama wao kufanyika kwa mkutano wa ndani Septemba 13, 2013.
Inadaiwa kuwa siku moja baada ya matangazo hayo, majira ya saa 11 alfajiri polisi walifika kijijini hapo na kushusha kipigo, kuwakamata wananchi na kuchukua baadhi ya mali zao kwa madai kwamba kuna vipeperushi vya kuwatisha watu wasihudhurie sherehe za Mwenge kijijini hapo. Waliokamatwa wametambuliwa kuwa ni Hassan Bakari, Bakari Hassan Naembe, Saidi Mohamedi, Antoni Dominick, Albeto Issa na Nyasi Nyota. Wananchi wengine waliambulia kipigo kwa kile kinachotajwa kuwa ni kosa la kutohudhuria mbio za Mwenge wa Uhuru ni Dadi Mohamed Chiputembe (Mwenyekiti wa CHADEMA kata ya Jangwani) ambaye hadi sasa anapata matibabu hospitali ya Lwelu, Asha Ali Nanyonge ambaye ni bibi wa umri unaokadiriwa kufikia miaka 70, Hassani Mkanangwamba, Ismail Hassani Mkanangwamba, Hamis Lada na Sania Abdalah. Aidha wanakijiji hao wamesema kuwa pikipiki yenye nambari za usajiri T367 AXH ya Yusufu Salum imeharibiwa kwa kutiwa chumvi kwenye injini yake. Inadaiwa kuwa baadhi ya askari polisi walioendesha ukamataji huo wanatuhumiwa kuvunja milango ya nyumba na maduka ya wanakijiji hao na kuiba mali na pesa katika kijiji hicho.
- Mmoja wa walioporwa mali zake ni Lwelu Hamisi Nyandindi anayedai kuibiwa sh 1,600,000 alizokuwa amezitunza katika nyumba yake.
Kamanda wa polisi wa mkoa wa Mtwara, Zelote Stephen, alidai kuwa hayo ni mambo ya kipolisi na bado upelelezi unaendelea. “Tunapeleleza. Karibu utaniuliza siku nyingine nikimaliza uchunguzi utanipigia,” alisema na kukata simu.
Watuhumiwa wa ugaidi mahututi
Mmoja wa vijana wawili kati ya wanne wa CHADEMA waliokuwa wamefunguliwa kesi ya ugaidi Igunga mkoani Tabora yuko mahututi kutokana na kipigo alichopewa akiwa mikononi mwa polisi. Kijana huyo, Seif Magesa, aliyekuwa amelazwa katika hospitali ya Nkinga mkoani Tabora amelazimika kuhamishiwa katika hospitali ya Rufaa ya Bugando jijini Mwanza baada ya hali yake kuwa mbaya zaidi. Seif amevimba sehemu kadhaa za mwili kiasi cha kulazimika kuhamishiwa katika hospitali hiyo kubwa. Hata hivyo, kijana mwingine Evodius Justian ambaye ni Mwenyekiti wa BAVICHA Wilaya ya Bukoba hali yake bado ni mbaya kutokana na kufanyiwa upasuaji sehemu zake za siri ambazo zinatoa usaha kutokana na kile kinachodaiwa ni kupigwa shoti ya umeme wakati akihojiwa na polisi na akilazimishwa kuwataja viongozi wakuu wa CHADEMA ili wahusishwe na ugaidi.
Evodius sasa amepangiwa kurudi tena Bugando Septemba 25 mwaka huu kwa matibabu zaidi. Akizungumza na gazeti hili, Evodius alisema ameumizwa vibaya sehemu za siri na kwamba anakojoa damu na usaha. Evodius Justinian alisema kuwa alikamatwa Bukoba: “Nikakaa rumande siku tatu kabla ya kusafirishwa hadi Mwanza. Nikiwa huko niliteswa sana ili nikubali kuwa ninajua ule mkanda wa Wilfred Lwakatare uliokuwa kwenye mitandao. “Nilikataa, niliteswa sana nikahojiwa kama nilimmwagia Musa Tesha tindikali nilikataa. Nilisafirishwa kwa ndege kuja Dar es Salaam ambako nilipokelewa na polisi. “Nikiwa uwanja wa ndege niliomba ruhusa kwenda chooni, askari walinifuata huko wakanitesa sana.
“Nilifanyiwa mahojiano na Advocate Nyombi na afande Pasua. Walinilazimisha nikubali kuwa viongozi wetu huwa wanafanya vitendo vya kigaidi,” alisema. Alisema kuwa akiwa makao makuu ya jeshi la polisi, aliteswa sana kwa maelekezo ya Afande Pasua na Nyombi katika ghorofa ya nane, jengo la makao makuu ya polisi. “Niliambiwa nieleze siri za Dk. Slaa, Mbowe, Mnyika na Lissu na niseme kuwa walihusika na vitendo vya utekaji na utesaji, nilipokataa nilipigwa shoti za umeme ili nikubali kusema. “Walikuwa wametafuta hata waandishi wa habari wakisubiri nikubali ili wanirekodi. Nilitoa maelezo kwa kulazimishwa huku nikiteswa. Nilipata nafuu baada ya wakili wangu, Nyaronyo Kicheere, kuja ndipo nikaeleza nilivyofanyiwa ukatili,” alisema.
Alisema kuwa alisafirishwa toka Dar es Salaam hadi Igunga na kwamba kila walikopita alitambulishwa kwa makamanda wa polisi kuwa ni mtu hatari sana. Naye Magesa aliliambia Tanzania Daima Jumatano kuwa hali yake sio njema, mwili unavimba sehemu tofauti tofauti na madaktari wameshauri apelekwe Bugando.
Kwa upande wake Seif Magesa alisema alikamatwa Mwanza na mabaunsa wa Meya wa Manispaa ya Ilemela, Henry Matata, aliyefukuzwa CHADEMA, wakiambatana na Adam Chagulani ambaye pia alifukuzwa pamoja na baadhi ya maafisa wa Usalama wa Taifa. “Nilipelekwa ofisi za Usalama wa Taifa. Nilihojiwa nikiulizwa mimi ni nani katika CHADEMA na kwa nini huwa nawasiliana na Mbowe, Dk. Slaa, Lissu au Mnyika,” alisema. Alisema kuwa aliuzwa kama viongozi hao wanahusika na utekaji wa watu mbalimbali unaotokea nchini na alipokataa aliteswa sana kuanzia saa 3 hadi 7 usiku.
“Nilipigwa shoti za umeme kwa maelekezo ya afande Pasua. Yeye alikuwa anakuja kuniaga kuwa anaenda kunywa pombe, vijana watafanya kazi yao. Waliniambia kuwa Lwakatare alikuwa amenitaja kuwa mimi nafanya vitendo vya kigaidi. Nilikataa kata kata,” alisema. Aliongeza kuwa Aprili 23, mwaka huu, waliwaleta mama yake mzazi, mama mkwe na mkewe huku wakimdhalilisha mbele yao lakini alikataa kubadili maelezo yake. “Siku moja nikiwa nahojiwa simu ya afande aliyekuwa ananihoji ilikuwa karibu; kiongozi mmoja wa CCM (anamtaja) alipiga simu akisema kama nimekataa kusema lolote nipelekwe Igunga ambako nilipelekwa nikasomewa shtaka la kummwagia tindikali Musa Tesha,”
Source: Tanznia Daima (Sept. 2013). Mtwara kwanuka tena. Retrieved from Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment