BAADHI ya vigogo wa serikali akiwemo mbunge mmoja wa CCM wanaodaiwa kumiliki vituo vya mafuta, kando kando ya Bahari ya Hindi wametajwa kuwa vinara wa hujuma na wizi wa mafuta kwenye bomba kubwa la TPA, imefahamika. Akizungumza na Tanzania Daima Jumatano jana kwa sharti la kutotajwa jina lake, mmoja wa wafanyakazi wa kituo cha mafuta kilichoko kandokando ya Bahari ya Hindi alikiri kuwepo kwa hujuma hiyo hasa kwa vituo vya mafuta. Alisema kuwa baadhi ya vigogo hao wamekuwa wakifanya hujuma hiyo kwa kuunganisha mabomba yao pale TPA inapokuwa ikipakua mafuta hayo. “Yaani Dk. Mwakyembe kama amechelewa ninavyokwambia hapa kuna kile kituo cha mafuta ninachofanyia kazi (jina linahifadhiwa) ambacho kinamilikiwa na mbunge mmoja wa Chama cha Mapinduzi (CCM) kinacheza huo mchezo sana tu huu karibia mwaka wa tatu,” alisema.
Alisema kuwa mbali na kuunganisha mabomba vituo hivyo vimekuwa vikipakua mafuta hayo na kuyajaza katika magari na kisha kusafirisha katika vituo vingine vikiwemo vya mkoani. Chanzo cha habari kimesema kuwa kwa utaratibu, mafuta yakishapakiwa katika magari hayo yasisafirishwe siku hiyo lakini vituo hivyo vimekuwa vikisafirisha kuhofia kukamatwa. “Niwaombe mjipange na kama mtakuwa na muda mje majira ya saa 12:30 au saa 1:30 usiku wakati kumetulia siku za Ijumaa na Jumamosi ambapo hujuma hiyo ndiyo hufanyika,” alisema. Hata hivyo gazeti hili lilimtafuta kigogo aliyetajwa katika hujuma hiyo ambaye hakuwa tayari kupokea simu wala kujibu ujumbe mfupi wa mkononi aliotumiwa na gazeti hili. Mwishoni mwa wiki Dk. Mwakyembe alisema anaamini kuwa watu hao wanafahamika kwa kuwa si rahisi hujuma kama hiyo kufanywa na mtu asiyekuwa mtaalamu wa sekta hiyo.
Dk. Mwakyembe alisema wezi hao bila hofu wamejaribu kulitoboa bomba hilo kubwa ambalo limeigharimu serikali mamilioni ya shilingi na kuunganisha mabomba yao chini kwa chini kisha kunyonya mafuta hayo hadi kwenye stesheni zao za kuhifadhia mafuta. Alisema kuwa wezi hao wamekuwa wakiibia serikali lita 35,000 hadi 40,000 katika kipindi kisichojulikana kitendo ambacho ni sawa na uhujumu uchumi. “Tiper ndio vinara wa wizi huo hivyo naagiza kuvunja mkataba, pia muwalete ili waje wawataje waliohusika na wizi huo, kwani umefanywa kitaalamu pia nasikia kuna Mzungu ambaye amezoea kutoa rushwa lakini kwa hili naamini watarudi kwao Ulaya,” alisema na kuongeza: “Baada ya wizi kupungua kwenye Mamlaka hiyo Bandari nawapongeza sana lakini wapo watu ambao si waaminifu, wamebuni mbinu mpya za kuihujumu serikali kwa kutumia mbinu nyingine,” alisema Dk. Mwakyembe. Alisema kuwa alimfahamisha Waziri wa Nishati na Madini Sospeter Muhongo juu ya hujuma hiyo inayofanywa na kampuni hiyo ya Tiper, kitendo ambacho kilimsononesha.
Source: Kangonga B. ( Sept. 2013).Vigogo, mbunge watuhumiwa kuiba mafuta. Retrieved from Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment