Wasiliana nasi : chademadiaspora@gmail.com -Fair and Balanced Platform- Twitter @ChademaDiaspora

Wasiliana nasi : chademadiaspora@gmail.com -Fair and Balanced Platform- Twitter @ChademaDiaspora
----------------------WE THANK AND APPRECIATE YOU FOR VISITING CHADEMA DIASPORA BLOG. AGAIN, THANK YOU!-----------------------

Wednesday, July 17, 2013

Wenje amchongea Mwijage kwa wapiga kura Muleba



     MBUNGE wa Nyamagana, Ezekia Wenje (CHADEMA), amewataka wananchi wa Jimbo la Muleba Kaskazini, kumhoji mbunge wao Charles Mwijage (CCM) kuhusu anavyotumia pesa za Mfuko wa Maendeleo ya Jimbo. Wenje aliyasema hayo akiwa katika ziara ya Kanda ya Ziwa Magharibi iliyohusisha wabunge wote wa CHADEMA katika kanda hiyo. Akihutubia wakazi wa Kata ya Muhutwe wilayani Muleba juzi, Wenje alisema ni haki ya wananchi kushirikishwa na mbunge wao katika kupanga jinsi ya kutumia pesa hizo. Wenje alitoa kauli hiyo baada ya kuelezwa na wananchi kwamba tangu ameingia bungeni, Mwijage hajawahi kuitisha mikutano ya kuwaeleza anapewa kiasi gani cha fedha, na kuwashirikisha kupanga jinsi ambavyo wangependa kuzitumia.

     Wananchi hao walisema kuwa mbunge wao amekuwa akizitumia fedha za mfuko huo kufanyia miradi anayopanga yeye bila kuwashirikisha. Wenje ambaye ndiye kiongozi wa msafara wa wabunge wa kanda hiyo kwenye ziara hiyo, alisema jimbo linapata kiasi cha sh milioni 72 kila mwaka kupitia mfuko huo. Kisha akaongeza kuwa CCM ndiyo chanzo cha matatizo mengi yanayowasibu wananchi, na akawataka waige mfano wa wana Arusha kwa kukikataa chama hicho katika uchaguzi. Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa Kanda ya Ziwa Magharibi, Dk. Rodric Kabangila alisema magonjwa mbalimbali yanayosababisha wananchi kupelekwa Bugando yanachangiwa na matumizi ya maji yasiyo salama kutokana na uzembe wa Serikali ya CCM.

     Katika Kata ya Bulyakashaju, Profesa Kulikoyela Kahigi (Bukombe) na Conchesta Rwamulaza (Viti Maalumu), waliwahamasisha wanawake kuwa mstari wa mbele katika harakati za kudai mabadiliko ya kisiasa, kijamii na kiuchumi. Profesa Kahigi aliwaasa wananchi kufuata mfano wa wanaArusha ambao wameonyesha njia ya kupambana na uonevu wa CCM, kwa kuchagua madiwani wa CHADEMA na kukataa wagombea wa chama hicho tawala katika uchaguzi mdogo uliopita. Alisema CCM imeua elimu na kilimo, na kusababisha umaskini kwa wananchi wake. “Serikali imeshindwa hata kusaidia wananchi wa Kagera kuondokana na ugonjwa wa mnyauko unaoshambulia migomba,” alisema. Vile vile, aliwataka wananchi kuachana na siasa chafu zinazosambazwa na CCM, wakati mwingine kwa kutumia baadhi ya wanachama na viongozi wa CHADEMA wasio waadilifu.

     Katika Kata za Nyakatanga, Ngenge na Mushabago mkutano ulihutubiwa na Dk. Anthony Mbasa, Mbunge wa Biharamulo, ambaye alikuwa mgeni rasmi, akiongozana na Renatus Kilongozi, Katibu wa CHADEMA Bukoba Manispaa na viongozi wengine kutoka maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Kagera. Akizungumzia msimamo wa CHADEMA kuhusu Rasimu ya Katiba Mpya, alisema CCM wanahaha kuipinga, kwa sababu tangu awali hawakuwa na hoja ya kuandika Katiba Mpya. Dk. Mbasa alisema CCM wanapinga Rasimu ya Katiba iliyotolewa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba kwa sababu imechukua mawazo mengi mazuri yaliyopendekezwa na CHADEMA na makundi mengine yanayotaka mabadiliko, na kwamba wanang'ang'ania mambo yao yale yale ambayo yamekuwa yanapingwa na wananchi kwa miaka 20 sasa.

Source: Jumapili A. (July 2013).Wenje amchongea Mwijage kwa wapiga kura Muleba. Retrieved from Tanzania Daima

No comments: