Wasiliana nasi : chademadiaspora@gmail.com -Fair and Balanced Platform- Twitter @ChademaDiaspora

Wasiliana nasi : chademadiaspora@gmail.com -Fair and Balanced Platform- Twitter @ChademaDiaspora
----------------------WE THANK AND APPRECIATE YOU FOR VISITING CHADEMA DIASPORA BLOG. AGAIN, THANK YOU!-----------------------

Wednesday, July 17, 2013

Lipumba achochea tena udini

WAUMINI WALISHWA KIAPO


      KASHFA zaidi za Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba kuendesha kampeni za kidini kwa ajili ya uchaguzi mkuu ujao zimezidi kuanikwa. Wakati kashfa nyingine iliyomtuhumu kutoboa siri ya namna alivyofanya kampeni za kuwashawishi watu wa dini yake kumchagua aliyekuwa mgombea wa urais kupitia CCM kwa misingi ya kidini, ikiwa bado inarindima, Lipumba anatuhumiwa kutoa maagizo kwa waumini wa Kiislamu kuchagua mgombea wa dini hiyo mwaka 2015. Mkanda wa video ulionaswa na Tanzania Daima unamuonyesha kiongozi huyo wa ngazi ya juu kabisa wa CUF akiwahamasisha Waislamu kuungana na kushikamana kupigania haki zao za kiraia. Katika mkanda huo uliorekodiwa katika Msikiti wa Mtambani jijini Dar es Salaam, mara baada ya swala ya Ijumaa unamwonyesha Profesa Lipumba akiwataka waumini kupigania haki zao ambazo alisema kwa sasa hawazipati.

       Lipumba aliwaambia waumini hao kuwa serikali imewatupa na kuwafanya waishi kama raia wa daraja la nne ndani ya nchi yao. Kwenye mkanda huo wa video, Profesa Lipumba anasikika akiwataka Waislamu kujipanga kikamilifu kisiasa ili kuzuia kile alichokiita uuzwaji wa nchi na rasilimali zake. Alisema kuna mafisadi wamejipanga kuchukua nchi na kuiuza jumla huku wakiungwa mkono na watu ambao hakuwataja. Alifafanua kuwa mafisadi hao wanaendesha biashara ya madisko inayoambatana na uchafu wa kila aina, biashara ya vileo na dawa za kulevya. “Kwahiyo ndugu zangu Waislamu tupo njiapanda katika nchi yetu. Tuna rasilimali kubwa zinazidi kugunduliwa, lakini siasa zetu zinazidi kuwa na matatizo na sisi Waislam tupo chini. Utajiri huu unatolewa macho, wanahitajika watu ambao ni mafisadi waweze kushika nchi, na hao ndio wanaoungwa mkono washike nchi halafu waweze kuiuza nchi yote kwa ujumla.

      “Kwahiyo, huu ni wakati wa kuwa macho kwamba tupo njiapanda. Hii neema, utajiri unaogunduliwa ikiwa hatutajipanga vizuri, neema hii itabadilika kuwa balaa, neema hii badala ya kumsaidia kila Mtanzania aweze kuneemeka na neema hii, itageuka kuwa balaa dhidi yetu,” alibainisha Profesa Lipumba. Aliwaeleza waumini hao kuwa kwa sasa Waislamu wanapaswa kushiriki kikamilifu katika harakati za siasa za nchi kama walivyoshiriki wazee wao wakati wa kudai uhuru. “Kwamba kila mwananchi, kila Mtanzania awe raia wa daraja la kwanza. Apate fursa ya uhuru wa dini yake, apate fursa ya kuelimishwa kwa kadiri ya uwezo ambao Mwenyezi Mungu amempa bila kubaguliwa, apate fursa ya kupata huduma bora za afya, apate fursa ya kushiriki kikamilifu katika uendeshaji wa serikali, apate fursa ya uendeshaji wa uchumi wa nchi yetu.

     “Kazi ipo kwetu, na ndugu zangu sisi tunapozungumza hapa tumejitoa mhanga. Kwamba hii ni nchi yetu sote, tunamuogopa Mwenyezi Mungu Tunamuogopa Mwenyezi Mungu na huu mwezi wa Ramadhan,” aliweka mkazo Profesa Lipumba. Katika kusherehesha kauli ya Profesa Lipumba, mhadhiri wa Kiislamu, Ustaadhi Said Ricco alisema kuwa waendesha madisko aliowakusudia Profesa Lipumba ni Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe, maelezo ambayo hayakukanushwa na kiongozi huyo wa CUF. Katika hatua ya kushangaza, waumini waliohudhuria ibada hiyo walilishwa kiapo na Ustaadhi Ricco cha kuahidi kumpigia kura Profesa Lipumba katika uchaguzi mkuu wa 2015 ili awe Rais wa Tanzania, huku mwenyewe akishuhudia kitendo hicho bila kusema chochote.

      Gazeti hili lilifanya juhudi za kumpata Profesa Lipumba ili atoe ufafanuzi wa kauli zake, lakini ilishindikana kutokana na simu yake ya kiganjani kutokuwa hewani. Hata alipotumiwa ujumbe mfupi wa maandishi, hakuweza kujibu chochote. Naibu Katibu Mkuu wa CUF Tanzania Bara, Julius Mtatiro alipoulizwa kuhusu kauli za mwenyekiti wake, alisema hajui chochote kwani huwa haambatani naye anapokwenda kusali misikitini. “Mimi sijui chochote kwa sababu huwa siambatani naye misikitini, nakushauri umtafute yeye mwenyewe azungumze maana yeye ndiye aliyerekodiwa akitoa kauli hizo, siyo mimi Mtatiro,” alisema.

       Lakini Mtatiro alipokumbushwa jinsi alivyosimama kidete kumtetea Lipumba katika tuhuma za awali kuhusiana na suala hilo la kampeni za kidini, na vipi sasa ashindwe kutoa kauli, kiongozi huyo alisisitiza kutoongea lolote, na kudai hayo ni masuala binafsi ya mwenyekiti wake na sio msimamo wa chama chao. Hivi karibuni Profesa Lipumba alikaririwa akikiri kwamba alihamasisha kuunganisha nguvu kati ya CCM na CUF ili kumwezesha Rais Kikwete kushinda uchaguzi mkuu wa mwaka 2010 kwa kigezo cha udini. Kashfa hiyo ambayo haijakanushwa na Lipumba iliibua mjadala mkubwa, huku CUF wakijitahidi kumtetea bila mafanikio. Aidha, licha ya video hiyo kusambazwa katika mitandao ya kijamii, ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini haijawahi kusema lolote kuhusiana na suala hilo.


Source: Maziku G. (July 2013).Lipumba achochea tena udini. Retrieved from Tanzania Daima

No comments: