Meya wa Jiji la Arusha, Gaudance Lyimo (CCM), ametamba kuwa wanaofikiria kumng’oa kwenye kiti chake wanaota ndoto za alinacha kwa sababu lazima wazingatie kanuni za uendeshaji wa Mabaraza ya Madiwani. Baada ya kushinda kata nne za Arusha kwenye uchaguzi mdogo juzi, Chadema ilitamba kuwa kazi inayofuata ni kumng’oa Meya kutokana na kuwa na viti vingi kwenye Baraza la Madiwani. Lyimo aliliambia Mwananchi kuwa pamoja na Chadema kuwa wajumbe wengi kwenye Baraza la Madiwani, bado hawana ubavu wa kumtoa. Alisema ili kumtoa katika nafasi hiyo wanahitaji kuwa na theluthi mbili ya wajumbe . Lyimo alisema maana yake ni kuwa ili ang’oke lazima Chadema waungane na madiwani wa CCM ndiyo watafanikisha azma hiyo.
“Sharti la kumng’oa madarakani Meya au Mwenyekiti wa halmashauri ni kupata theluthi mbili ya kura za wajumbe wote. Najiuliza wenzetu watafikiaje kiwango hicho hadi waanze kutamba kuning’oa madarakani,” alisema Lyimo. Jiji la Arusha lina jumla ya wajumbe 32 kwenye Baraza la Madiwani ambapo ukimtoa Meya, wajumbe wanaostahili kupiga kura wanasalia 31 hivyo kufanya wenye nia ya kumng’oa kiongozi huyo kuhitaji zaidi ya kura 24 kutimiza lengo lao. Baada ya kunyakua viti vyote vinne kwenye uchaguzi mdogo uliofanyika Jumapili iliyopita, Chadema imefikisha wajumbe 15 kwenye baraza ikiwa ni madiwani 12 pamoja na wabunge watatu, wawili wa viti maalumu na mmoja wa jimbo.
Meya huyo aliwataka madiwani kutoka Chadema kuacha kupoteza muda na nguvu nyingi kuweka mikakati ya kumng’oa madarakani, badala yake watumie muda na nguvu hizo kuwatumikia wananchi waliowaamini na kuwapigia kura kwenye uchaguzi. Alisema kwa nafasi yake ya Umeya, atashirikiana na madiwani wote kutatua kero na kutafutia ufumbuzi matatizo ya wananchi bila kujali tofauti zao kiitikadi kwa sababu suala la maendeleo halina itikadi, dini wala ukabila. Akizungumzia kiti cha Umeya, Katibu wa Chadema Kanda ya Kaskazini, Amani Golugwa alisema ajenda kuu ya Chadema ni kupata wingi wa kura na hivyo kuwa na uamuzi katika Baraza la Madiwani limefanikiwa baada ya kurejesha kata zake zote nne.
“Hata kama wenzetu wataendelea kubaki na Meya wao wa ‘kuchonga’, bado uamuzi wote unayohitaji kura kwenye baraza la halmashauri yatasimamiwa na kuongozwa na Chadema. Hilo ni faraja na ishara njema ya kunyakua uongozi wa halmashauri na nchi katika uchaguzi mkuu ujao,” alisema Golugwa. Tangu achaguliwe kushika wadhifa huo mwaka 2010, Meya Lyimo amekuwa akipingwa na Chadema kwa madai kuwa hakuchaguliwa kihalali ambapo Januari 5, 2011, chama hicho kikuu cha upinzani kiliitisha maandamano makubwa kumpinga ambayo yaliishia kwa watu kujeruhiwa na kuuawa baada ya polisi kuyasambaratisha.
Source: Lymo G. (July 2013)Meya Arusha awavimbia Chadema. Arusha. Retrieved from Mwananchi
No comments:
Post a Comment