Wasiliana nasi : chademadiaspora@gmail.com -Fair and Balanced Platform- Twitter @ChademaDiaspora

Wasiliana nasi : chademadiaspora@gmail.com -Fair and Balanced Platform- Twitter @ChademaDiaspora
----------------------WE THANK AND APPRECIATE YOU FOR VISITING CHADEMA DIASPORA BLOG. AGAIN, THANK YOU!-----------------------

Tuesday, July 2, 2013

Obama azindua mitambo tata

APONDA VIONGOZI, WAZIRI MUHONGO AJITETEA



      RAIS wa Marekani, Barack Obama jana alizindua mitambo ya kufua umeme ambayo ilizua mtafaruku mkubwa na kusababisha mtikisiko mkubwa serikalini na bungeni. Mitambo aliyozindua Rais Obama ni ile iliyodaiwa kuwa mibovu na isiyofaa, mali ya Kampuni ya Dowans iliyorithi mkataba tete kutoka kampuni iliyozua sakata zito lililosababisha kujiuzulu kwa aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa. Dowans Tanzania Limited ilirithi mkataba tata wa kampuni ya kufua umeme wa dharura ambao kampuni ‘hewa’ ya Richmond Development Corporation iliingia na TANESCO Juni 23, mwaka 2006, kufua umeme wa dharura wa megawati 100 kwa kutumia gesi asilia. Hata hivyo, Richmond ilishindwa kuleta mitambo hiyo, na ikaonekana baada ya uchunguzi wa Kamati ya Bunge iliyoundwa Novemba 2008 kuwa haikuwa imesajiliwa huko Marekani kama kampuni inayofua umeme.

     Lowassa alilazimika kujiuzulu pamoja na mawaziri wawili, Nazir Karamagi na Ibrahim Msabaha kutokana na kashifa hiyo, kabla ya kampuni ya Dowans kuuziwa mkataba wa kufua umeme na Richmond katika hatua nyingine iliyozua sintofahamu serikalini. Utata huo uliongezeka zaidi baada ya kubainika kuwa hadi Kampuni ya Richmond Development, ikijitoa na kuirithisha mkataba wake Dowans, kinyume cha maelezo yaliyowahi kutolewa bungeni na baadhi ya viongozi wakuu wa serikali, kwamba haikuwahi kupewa fedha za serikali, kampuni hiyo ilikuwa imechotewa zaidi ya sh bil. 30 (Dola 30,696,598 za Marekani). Kiasi hicho ni sawa na asilimia 35 ya gharama ya kodi ambayo msingi wake ulikuwa kufanikisha mchakato wa ufunguaji wa hati ya muamana (letter of credit) kati ya kampuni hiyo na Benki ya Biashara.

    Malipo hayo ya asilimia 35 ni utekelezaji wa makubalino yaliyofikiwa awali, kati ya serikali na wawakilishi wa Richmond Development. Baada ya kupewa kitita hicho cha zaidi ya sh bil. 30, Richmond ilipewa masharti ya kurejesha fedha hizo serikalini katika malipo ambayo yangefanyika kwa dola 1,279,044 za Marekani (zaidi ya sh bil. 1.3) kila mwezi, lakini katika awamu tatu. Malipo ya awali yalipaswa kuanza kufanyika Novemba 2007. Hata hivyo, kutokana na utata wa Richmond, hasa kwa upande wa uwezo wake kiteknolojia na utendaji, kampuni hiyo iliuza shughuli zake kwa Dowans. Imebainika kuwa wakati mchakato wa uuzaji wa shughuli za kampuni hiyo kwa Dowans unafanyika, Richmond ilikuwa haijarejesha fedha ilizopewa na serikali na kwa kuwa Dowans ndiyo iliyobeba mikoba, ilipaswa kuendeleza urejeshaji huo.

   Kutokana na hali hiyo ya fedha za serikali kubaki kwa 'wawekezaji' hao waliopasiana mpira wa uwajibikaji, Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), kupitia timu ya wataalamu wa sheria, ilichunguza mkataba kati yake na Richmond ambao ulirithiwa na Dowans. Taarifa ya timu ya wanasheria wa TANESCO ilibaini kuwa mkataba huo hauna nguvu za kisheria na kuamuru uvunjwe. Ukavunjwa rasmi Agosti Mosi, 2008. Imebainika kuwa fedha zilizorejeshwa hadi mkataba unavunjwa ni jumla ya dola 7,674,186 za Marekani (zaidi ya sh bil. 7.7), huku dola za Marekani 23,022,412 (zaidi ya sh bil. 23) zikibakia kwa Richmond na mrithi wake Dowans. Dowans waliweza kuingiza nchini mitambo ya kufua umeme na kuanza kazi, lakini ilizuka vuta nikuvute kati ya wawekezaji hao na wabunge, baada ya kudaiwa kwamba mitambo hiyo ilikuwa mibovu na haikufaa kwa lolote.

      Mbali na tuhuma za ubovu wa mitambo hiyo, bado kwa mujibu wa mkataba serikali ililazimika kuilipa kampuni hiyo kiasi kikubwa cha fedha kwa mujibu wa mkataba, ingawa haikuzalisha umeme wowote. Kutokana na hali hiyo, na baada ya mvutano mkubwa, serikali iliamua kuvunja mkataba huo jambo lililoifanya Dowans kwenda mahakamani kudai fidia. Dowans ilifungua kesi dhidi ya TANESCO katika Mahakama ya Usuluhishi wa Migogoro ya Biashara (ICC) ambayo hukumu yake iliiamuru TANESCO kulipa faini ya sh bil. 94 kwa kukatisha mkataba huo. Taarifa zinaeleza kuwa hukumu hiyo yenye kurasa 211 ilionesha kuwa mmiliki wake pia anatuhumiwa kuwa ndiye aliyeileta Kampuni ya Richmond ambayo mkataba wa Richmond kwenda Dowans ulifanyika nje ya TANESCO kinyume cha sheria ya manunuzi ya umma. Ni katika kipindi hicho, Dowans iliamua kuuza mitambo hiyo kwa Kampuni Symbion Tanzania, ambayo imesifiwa na kuchukua sura ya kuwa mitambo bora na ya kisasa ya kufua umeme hapa nchini.

Obama awashukia viongozi, Waziri Muhongo ajitetea

    Katika hatua nyingine Rais Obama amewatupia shutuma viongozi wa serikali za Bara la Afrika kwa tabia yao ya ubabaishaji na kushindwa kutekeleza miradi wanayofadhiliwa na ile ya ndani kwa wakati muafaka. Rais Obama ameyasema hayo jana wakati akizungumza na wanahabari jana, kwenye mtambo wa kufua umeme wa Symbion, ulioko Ubungo jijini Dar es Salaam mbele ya mwenyeji wake, Rais Jakaya Kikwete. Bila kutaja majina ya viongozi hao, Rais Obama alidai kuwa baadhi ya viongozi wa serikali wamekuwa hodari sana wa kupanga mipango ya maendeleo, lakini wasiweze kuisimamia na hata kuitekeleza. 

   Kauli hiyo ilipokelewa kwa hisia tofauti miongoni mwa watendaji wa serikali walioyokuwepo kiasi cha kumlazimu Waziri wa Nishati na Madini, Prof. Sospeter Muhongo kuitolea maelezo. Muhongo akizungumza na waandishi wa habari, mara baada ya Rais Obama kuondoka, alikiri kuwepo kwa tatizo katika wizara yake kabla ya yeye kuongoza wizara hiyo. “Wakati naingia madarakani nilikuta tatizo la kiwanda cha saruji cha Mtwara kikizungushwa kupewa kibali cha kuanza kazi kwa zaidi ya miaka miwili, lakini katika uongozi wangu nimetumia muda wa saa mbili kuhakikisha wanapata kibali hicho,” alisema. Muhongo aliwahakikishia Watanzania kwamba mradi wa umeme wa nchi za Afrika (Power Africa Initiative) watautekeleza kwa wakati kwa kufikisha kila mkoa umeme wa uhakika ili tatizo hilo libaki kuwa historia.

   Alibainisha kuwa ili kuhakikisha umeme wa uhakika unapatikana wamepanga kuongeza mara mbili ya umeme wa sasa ambao ni megawatt 1438.24 na kufikia megawatt 2780 hadi kufikia mwaka 2015. Lakini pia nchi inakusudia kufikia megawatt 3000. Akizungumzia faida nyingine ya Obama kwa kuja Tanzania alisema baada ya kufanya mazungumzo wamefanikiwa kuongeza megawatt 600 za uzalishaji wa umeme katika mradi wa Symbion na GE. Katika hotuba yake Rais Obama alisema kuwa mradi huo utakaofaidisha Watanzania katika awamu ya kwanza utagharimu kiasi cha dola bilioni 7 na pia nchi nyingine zitakazonufaika nao ni Ethiopia, Kenya, Liberia, Nigeria, Uganda na Msumbiji.

    Alisema kuwa sababu kubwa ya kuchagua nchi hizo imechagizwa na kuwa na  malengo kabambe ya kufanya mageuzi katika sekta ya nishati kwa ajili ya kuboresha uwekezaji na ukuaji wa uchumi. Akizindua rasmi mpango huo Maalum wa Maendeleo ya Nishati alisema kuwa msaada huo umetoka katika sekta binafsi na serikali ya Marekani. Alisema kuwa sababu nyingine ni kuhakikisha wakazi wengi hasa wa maneo yasiyokuwa na umeme ambao ni asilimia kubwa kupata huduma hiyo. Katika ziara yake hiyo Obama pia alizindua mpira wa miguu ambao waliucheza na Rais Kikwete ukiwa maalumu kwa kuchaji simu na kuwasha taa ambao umetengezwa na Kampuni ya Unchartered play.inc.

Source: Tanzania Daima (July 2013). Obama azindua mitambo tata. Retrieved from Tanzania Daima

No comments: