Na Bwana Mdogo
KUNA ugaidi na ugaidi; kuna ugaidi unaofanywa na serikali zilizoko madarakani na kuna ugaidi unaofanywa na vikundi vya siasa, kidini na watu binafsi. Ugaidi una historia ndefu. Asili ya neno ugaidi (terrorism) ni neno la Kifaransa “terrorisme”, ambalo hakika asili yake lilikuwa likielezea ugaidi wa serikali (state terrorism) uliokuwa ukifanywa na Serikali ya Ufaransa enzi za utawala wa hofu (reign of terror). Hata neno la Kifaransa ‘terrorisme’ linatokana na neno la Kilatini ‘terre?’ lenye maana ya ‘natisha’. Zamani ugaidi ulimaanisha vitendo vya udhalimu vilivyokuwa vinafanywa na serikali dhidi ya wapinzani kisiasa. Baadaye walibadilisha dhana hiyo, na kama ilivyo leo, kumaanisha mauaji ya watu wasio na hatia yanayofanywa na vikundi fulani.
Serikali zilipata ahueni kubadili dhana ya ugaidi baada ya baadhi ya watu kujitokeza na kujiita kuwa ni magaidi. Hiyo ilikuwa miaka ya 1800 raia mmoja wa Russia, Sergey Nechayev alipojiita kuwa yeye ni ‘gaidi’. Mwaka 1869 aliasisi kikundi cha kigaidi alichokiita People's Retribution. Siasa za Nechayev na People's Retribution ndizo zinafanywa na serikali nyingi duniani ikiwemo Serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), lakini husingizia wengine.
Tafsiri ya UN
Novemba 2004, ripoti ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN) ilieleza ugaidi kuwa ni kitendo chochote “chenye kusudio la kusababisha kifo au maumivu makali ya mwili kwa raia au watu wasio askari kwa lengo la kutishia watu au kuishinikiza serikali au shirika lolote la kimataifa kufanya au kujizuia kufanya jambo lolote. ” Mwanasheria wa Australia aliliambia Bunge kuwa; “Jumuiya ya kimataifa haijafanikiwa kutengeneza na kukubaliana juu ya tafsiri moja kuhusu ugaidi.” Alisema; “Katika miaka ya 1970 na 1980, juhudi za Marekani kupata tafsiri sahihi ziligonga mwamba kutokana hasa na mitazamo tofauti kutoka kwa watu juu ya matumizi ya vurugu katika dhana ya machafuko dhidi ya uhuru wa taifa na ujasiri.”
Utata wa kupima ugaidi
Neno ugaidi limepewa maana kutokana na misingi na mhemko wa kisiasa, na hakika limesababisha ugumu wa kupata tafsiri mwafaka. Wanazuoni wamebaini aina zaidi ya 100 ya tafsiri za ugaidi. Mara zote tafsiri imekuwa ikizua utata kwani hutumiwa zaidi na serikali, na hata baadhi ya watu, kwa msaada wa serikali, kupambana kisheria dhidi ya uhalali wa vikundi au vyama vya siasa pinzani kwa chama tawala (kwa Tanzania ni CCM). Serikali inayolaani vyama vya upinzani na kudai ni vya kigaidi, ndiyo inayohalalisha udhalimu wake kwa kutumia nguvu za vyombo vya dola kupiga, kuua, kujeruhi, kufunga wapinzani. Na ili serikali ifanikiwe kuhalalisha matumizi ya nguvu, itadai vyama vya upinzani vinafanya ugaidi dhidi ya serikali iliyoko madarakani.
Hicho ndicho kinafanywa sasa na Serikali ya CCM dhidi ya makada na viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA). Serikali inawakamata kila uchao na kuwafungulia kesi kwa madai ama ya uchochezi au kutukana au ugaidi. Serikali ya CCM inalenga kuwaumiza kisaikolojia na kuwakosesha muda wa kunadi sera kwa urari sawa na wao. Hata serikali inajua utata wa dhana ya ugaidi. Prudence Rweyongeza, wakili wa serikali katika kesi ya ugaidi iliyokuwa inamkabili Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa CHADEMA, Wilfred Lwakatare, alisema sheria haijaeleza maana ya ugaidi unaomkabili kada huyo. Lwakatare alifutiwa mashtaka. Lakini Jeshi la Polisi pamoja na mwendesha mashtaka mkuu wa serikali, wanahangaika kuweka viraka ili ashitakiwe upya.
Kwa Marekani, mtu yeyote, hata kama ni raia wa taifa hilo kubwa, akijihusisha katika kuhujumu maslahi ya nchi hiyo atawindwa. Mmarekani akiwa nje ya nchi hiyo, sera inasema atauawa kwa ndege zisizo na rubani, lakini akiwa ndani atakamatwa afikishwe kwenye vyombo vya sheria. Hata hivyo, yenyewe haijihesabu kuwa inafanya ugaidi inavyoua watu wasio na hatia katika nchi za Iraq, Afghanistan, Pakistan; ilivyoingia Pakistan na kumuua Osama bin Laden wala ilivyosaidia mauaji ya Rais wa Libya, Muamar Gadaffi. Marekani imejipa uhalali wa kuhujumu.
Tofauti na Marekani, Serikali ya Tanzania inawinda raia wake na kuwabambikia makosa ya ugaidi. Inatumia ugaidi kujinufaisha na kutisha wananchi na katika kipindi hiki cha ziara ya Rais Barack Obama wa Marekani, lugha ya Rais Jakaya Kikwete ni kwamba serikali yake inapambana na magaidi wa ndani na nje. Hizi ni juhudi za kuitangazia dunia kwamba Tanzania kuna ugaidi na kuna magaidi, na magaidi kwa macho ya serikali ni vyama vya upinzani. Kabla ya kulipuliwa kwa ubalozi wa Marekani nchini mwaka 1998, Serikali ya CCM ilikuwa inahangaika na watu iliowaita wahaini.
Baada ya hapo, hasa baada ya kupitisha bungeni Sheria ya Kuzuia Ugaidi mwaka 2002, serikali inatumia sheria hiyo kuwakamata wapinzani wa kisiasa kwa CCM na kuwafungulia kesi za ugaidi. Isitoshe, wachambuzi wa masuala ya sheria, siasa na dini, tangu zamani wameonya uwezekano wa sheria hiyo kuja kutumiwa vibaya na sasa inaonekana. Wote wanaokamatwa ni wafuasi makini wa upinzani. Hii ndiyo sababu CCM inabadili sura za wahaini na magaidi. Mwaka 1995 iliitangazia ubaya NCCR-Mageuzi na ikawa inahangaika kuifuta kisheria; kwa bahati mbaya migogoro ‘ilikifuta’ hadi mwaka 2010 kilipojiunda upya na kuwa na nguvu.
Kipindi hicho hicho CCM ilihangaika na Chama cha Wananchi (CUF), mara ikidai CUF wameweka kinyesi kwenye visima, mara wamepaka kinyesi madarasani, mara hawataki Muungano na hila za kila aina. Magaidi wa leo kwa vigezo vya CCM ni CHADEMA. CCM haina habari na mafisadi kwa vile wao ndio vinara; haina habari na walarushwa kwa sababu wao wamekubuhu; haina habari na umaskini wa watu wala kuzorota kwa elimu kwani inataka kutawala wajinga. Marekani inasumbuka na kukua kwa ugaidi wa kimataifa kama wa vikundi vya Al Qaeda, al Shabaab na Boko Haram vilivyounganisha nguvu, Serikali ya CCM inahangaika na kukua kwa upinzani dhidi yake kutoka kwa CHADEMA, CUF na NCCR na inaomba kila siku vyama hivyo visiungane.
No comments:
Post a Comment