Wasiliana nasi : chademadiaspora@gmail.com -Fair and Balanced Platform- Twitter @ChademaDiaspora

Wasiliana nasi : chademadiaspora@gmail.com -Fair and Balanced Platform- Twitter @ChademaDiaspora
----------------------WE THANK AND APPRECIATE YOU FOR VISITING CHADEMA DIASPORA BLOG. AGAIN, THANK YOU!-----------------------

Wednesday, July 3, 2013

Mwigulu chali kortini

AKWEPA KUTOKEA, VIGOGO CHADEMA WAACHIWA



     MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi mjini Singida imetupilia mbali kesi iliyokuwa ikiwakabili viongozi wawili wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), baada ya shahidi muhimu, Mwigulu Nchemba, kushindwa kutokea mahakamani kuthibitisha matusi aliyodai kutukanwa. Viongozi hao walioachiwa huru juzi ni Mkurugenzi wa Sera na Utafiti makao makuu, Mwita Waitara na mshauri wa chama hicho, Dk. Kitila Mkumbo. Katika hukumu yake aliyoisoma mbele ya wakili wa washtakiwa hao, Tundu Lissu, Hakimu wa mahakama hiyo, Ruth Massam, alisema kuwa washtakiwa hawana kesi ya kujibu, kwa kuwa mashahidi wa serikali walishindwa kuthibitisha aina ya matusi yaliyodaiwa kutolewa na washtakiwa.

     Alisema kwamba upande wa serikali walishindwa kumleta shahidi muhimu katika kesi hiyo, Mwigulu, ambaye ni Naibu Katibu Mkuu wa CCM (Bara), aliyedaiwa kutukanwa ili athibitishe kama alitukanwa na namna ambavyo matusi hayo yamemuathiri. ”Kushindwa kwa Mwigulu kufika mahakamani ni kuonesha kwamba ama hajui kama alitukanwa au hakuona kosa lolote alilotendewa na mahakama haiwezi kutoa uamuzi kwa mambo ya kuhisiwa au ya kutungwa na kubambikiza,” alisema hakimu huyo.  Waitara na Mkumbo walidaiwa kutenda kosa hilo Julai 14, mwaka jana katika mkutano wa hadhara wa CHADEMA uliofanyika katika Kijiji cha Ndago wilayani Iramba. Kesi hiyo imekuwa ikisuasua mara nyingi kutokana na hatua ya upande wa serikali kushindwa kuleta mashahidi mahakamani na kusababisha kesi hiyo kuahirishwa mara kwa mara, jambo ambalo lilikuwa likimkera hakimu.

    Akizungumza na Tanzania Daima kuhusu uamuzi wa mahakama, Dk. Mkumbo aliishukuru mahakama kwa kuendelea kutenda haki dhidi ya wanachama na viongozi wa CHADEMA wanaofunguliwa kesi za ajabu ajabu kila kukicha.Mkumbo alifafanua kuwa mahakama imeendelea kujijengea heshima kwa kukataa kutumika kisiasa. Alisema kuwa kesi hiyo kama zilivyo kesi nyingine dhidi ya viongozi wa CHADEMA ilifunguliwa kwa mashinikizo ya kisiasa ndiyo maana upande wa serikali ulishindwa kuleta mashahidi walioorodhesha wenyewe katika hati ya mashtaka. Dk. Mkumbo alieleza kushangazwa na kitendo cha upande wa mashtaka kushindwa kumleta mtu aliyedaiwa kutukanwa na kuhoji huyo Mwigulu ni nani ambaye anaonekana yupo juu ya sheria za nchi.

      Dk. Mkumbo ambaye pia ni mhadhiri wa Chuo Kuu Kishiriki cha Ualimu (DUCE) cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, alilisihi Jeshi la Polisi lijirudi na lianze kufanya kazi zake kitaalamu kwa mujibu wa taratibu na sheria. Alisisitiza kuwa huko tuendako mapambano ya kisiasa yatakuwa makali, kwamba Jeshi la Polisi lisipojirudi likaanza kufanya kazi kitaaluma na kwa mujibu wa sheria, matatizo yatakuwa makubwa.

Source: Tanzania Daima (July 2013). Mwigulu chali kortini. Retrieved from  Tanzania Daima

No comments: