Wasiliana nasi : chademadiaspora@gmail.com -Fair and Balanced Platform- Twitter @ChademaDiaspora

Wasiliana nasi : chademadiaspora@gmail.com -Fair and Balanced Platform- Twitter @ChademaDiaspora
----------------------WE THANK AND APPRECIATE YOU FOR VISITING CHADEMA DIASPORA BLOG. AGAIN, THANK YOU!-----------------------

Wednesday, July 3, 2013

Tangazeni hali ya hatari Mtwara


       
       BARAZA la Vyama vya Siasa nchini, limeishauri serikali kuwa endapo inaamini Mkoa wa Mtwara si sehemu salama, itangaze hali ya hatari badala ya kuruhusu wawepo wanajeshi wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) wakiwa na zana za kivita na kutisha wananchi. Ushauri huo ni moja ya mapendekezo tisa yaliyopelekwa kwa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, baada ya wajumbe wa baraza hilo linaloundwa na vyama 20 vya siasa walipokutana jijini Dar es Salaam hivi karibuni kujadili mambo mbalimbali yanayoendelea nchini zikiwamo vurugu za Mtwara. Mwenyekiti wa baraza hilo, Peter Mziray, akizungumza na gazeti hili jana alisema kutokana na wanajeshi kuendelea kuzunguka katika mji wa Mtwara baraza limeamua kutoa mapendekezo na ushauri kwa serikali kwa sababu kifungu cha 21C (1) cha sheria ya Vyama vya Siasa namba 5 ya mwaka 1992 kimetoa mamlaka kwa baraza kuishauri serikali.

      Alisema katika mapendekezo hayo wameeleza kuwa kitendo cha wanajeshi kuendelea kuzunguka Mtwara na vifaa vya kijeshi ni cha kutisha wananchi pia ni kinyume cha Katiba ya nchi, haki za kiraia na haki za binadamu. “Baraza la Vyama vya Siasa linaona ikiwa serikali inaona kuwa Mtwara pamekuwa mahali hatari kiasi hicho, rais atangaze hali ya hatari kwa mujibu wa Katiba ya mwaka 1977 ibara ya 32 ili wananchi wote watambue kuwa Mtwara si salama tena,” imeeleza sehemu ya barua ya mapendekezo hayo kwa waziri mkuu. Mziray alisema mapendekezo mengine yaliyotolewa ni kuitaka serikali ifanye tathmini ya uharibifu wa mali za wananchi uliotokana na vurugu hizo na iwatambue waliofanyiwa uharibifu na izisaidie taasisi na vyama vya raia wote walioathirika kwa kuwafidia.


     “Serikali ianzishe uchunguzi huru wa mauaji yaliyofanywa na polisi kwa sababu ya kutumia nguvu kupita kiasi ili wananchi wasio na hatia waliouawa haki yao isipotee bure,” alisema. Mziray aliongeza kuwa mapendekezo mengine waliyoyawasilisha kwa waziri mkuu ni kutaka serikali iunde tume huru ya maridhiano itakayoshirikisha viongozi wa vyama vya siasa, dini, kijamii na wazee wa jadi zikiwamo mamlaka za serikali ili kutengeneza mkakati wa kutatua mgogoro Mtwara. Mapendekezo mengine ni kuitaka serikali itumie njia za kidemokrasia kuwasiliana na wananchi wa Mtwara kuliko kutumia nguvu kubwa za kijeshi na kimatamko kwani zinajenga usugu kwa wananchi.

       Pia serikali iweke wazi mikataba ya gesi na iujulishe umma inalinufaishaje taifa, badala ya kuifanya mikataba kuwa ya siri, jambo ambalo ni hatari kwa ustawi wa uwazi, uwajibikaji na maendeleo ya nchi. “Serikali ianze kujenga uchumi kwa mikoa ya kusini ili kuleta usawa katika maendeleo ya nchi kwa mikoa hiyo. Kwa kuanzia na Mtwara, serikali ijenge kiwanda kikubwa cha mbolea, viwanda vya chuma na viwanda vya malighafi zinazotokana na gesi inayozalishwa Mtwara kwa ajili ya kuzalisha ajira za kutosha na kuvutia wawekezaji,” alisema Mziray.

      Mwezi Mei mwaka huu kulitokea machafuko katika Manispaa ya Mtwara mkoani Mtwara baada ya wananchi wa mji huo kuchoma moto ofisi za serikali na nyumba za viongozi wa serikali takriban sita ikiwamo ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Hawa Ghasia. Hatua ya wananchi hao kufanya uasi huo na uharibifu mkubwa wa mali wanapinga  hatua ya serikali kusafirisha gesi kutoka Mtwara kwenda Dar es Salaam kabla ya kujua mikoa ya kusini watanufaika vipi.

Source: Tanzania Daima (July 2013). Tangazeni hali ya hatari Mtwara. Retrieved from Tanzania Daimna

No comments: