Wasiliana nasi : chademadiaspora@gmail.com -Fair and Balanced Platform- Twitter @ChademaDiaspora

Wasiliana nasi : chademadiaspora@gmail.com -Fair and Balanced Platform- Twitter @ChademaDiaspora
----------------------WE THANK AND APPRECIATE YOU FOR VISITING CHADEMA DIASPORA BLOG. AGAIN, THANK YOU!-----------------------

Friday, July 19, 2013

Chadema:Rasimu ya katiba kwa chopa


        Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimepanga kuzunguka nchi nzima kwa kutumia usafiri wa anga, majini na nchi kavu, kufanya mikutano ya hadhara, ambayo itakuwa ni mabaraza yake ya katiba. Katika mikutano hiyo, wananchi watajadili Rasimu ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kutoa maoni yao hadharani. Chadema imesema tangu ilipoanzisha ajenda ya katiba mpya, imekuwa na dhamira ya kuona Watanzania wakijipatia katiba inayotokana na matakwa yao ili kusimamia na kulinda maslahi yao. Imesema haitafanya mikutano ya ndani au ya siri kama inavyofanya Chama Cha Mapinduzi (CCM). Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, alisema hayo alipokuwa akihutubia mkutano wa hadhara uliofanyika katika viwanja vya Stendi ya Malori, eneo la Majengo, mjini Songea, mkoani Ruvuma juzi.


       Alisema utaratibu wote wa namna mabaraza ya katiba ya Chadema yatakavyoendeshwa kwa nia ya wananchi kutoa maoni yao na namna ya kuboresha rasimu hiyo, utatolewa hivi karibuni. Mbowe, ambaye pia ni Mbunge wa Hai na Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, alisema Chadema inataka katiba mpya inayotokana na mwafaka wa Watanzania wote. “Ndugu zangu, Watanzania wenzangu wa Songea, mtakumbuka kuwa ajenda hii ya katiba ilikuwa ni ya Chadema. Na tuliisimamia kwa miguu yote. Mnajua hilo. Haikuwa ajenda wala haijawahi kuwa ajenda ya CCM. Ndiyo maana sasa chama hicho kinafanya juhudi za kupingana na maoni ya Watanzania katika masuala ya msingi yaliyomo ndani ya rasimu,” alisema Mbowe na kuongeza:




     “Tunavyozungumza hapa, tayari mabaraza ya katiba yameanza kukutana. Lakini kama mnavyojua pia asilimia kubwa yametawaliwa na CCM...lakini sisi pia na Watanzania wengine wote wanaoipenda nchi yao, tunayo fursa ya kuunda baraza letu. Tutakuwa na mabaraza ya katiba nchi nzima, ambayo tutayafanya kwenye mikutano ya wazi ya hadhara. Hatutajifungia ndani kama wanavyofanya wao.” Alisema katika rasimu ya katiba mpya, pamoja na kuwapo kwa masuala mengi, kuna mambo manne, ambayo Mtanzania yeyote makini na anayeipenda nchi yake atalazimika kukubaliana na mapendekezo ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba inayoongozwa na Waziri Mkuu mstaafu, Jaji Joseph Warioba. “Bahati mbaya sana, mambo yote haya manne ambayo kwa kweli ni muhimu ssana yakawamo kwenye katiba mpya ya Watanzania, CCM wanayapinga. Tunaomba sana Watanzania mambo haya ni muhimu...kwanza kuna suala la maadili na miiko ya viongozi, pili kuna suala la tunu za taifa, tatu haki za binadamu na nne ni serikali tatu,” alisema Mbowe na kuongeza:



        “Haya ni kati ya mambo ya muhimu sana, ambayo sisi Chadema tunaona ni vyema yakatajwa na kuzingatiwa kwenye katiba npya, lakini jamaa mengine hawayataki au mengine eti wanataka yasitajwe kwenye katiba mpya, bali yaundiwe sheria. Yaani jamaa hawa wanahofu, hawataki mambo ya tunu za taifa kama vile uwazi, ili mikataba hii mibovu iliyoko kila mahali iwe mwisho. Wanapinga hata haki za binadamu. Serikali tatu ndiyo balaa kabisa. Wanajua wameondoka.” “Sasa jiandaeni kwa mabaraza ya katiba ya Chadema. Tutazunguka nchi hii ikibidi kwa ndege. Yatakuwa yakifanyika kwenye sehemu za wazi, ambayo siku nzima wananchi wa eneo husika watajadili rasimu ya katiba mpya wakitoa maoni yao. Kisha tutayachukua pamoja na saini zao...nchi nzima tutafanya, viongozi wote, wabunge wote watasambaa nchi nzima,” alisema Mbowe.



        Mbowe ambaye juzi alikuwa akihutubia mkutano wa hadhara kwa mara ya kwanza tangu yeye na viongozi wenzake waliponusurika kufa katika shambulio la bomu la kijeshi, alisema kuna propaganda, ambazo ama zinafanywa kwa makusudi au kwa kutokujua, zikipotosha maana nzima ya amani, ambayo kila Mtanzania hana budi kuipigania. Akimnukuu Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere kwenye moja ya hotuba yake aliyowahi kuitoa mwaka 1986, Ukumbi wa Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM), jijini Dar es Salaam, Mbowe alisema kama jamii haina wala haioni matumaini kwa viongozi wao, huku haki zikiminywa, amani haiwezi kudumu. “Suala la amani linafanyiwa upotoshaji mkubwa siku hizi. Ukisikiliza baadhi ya redio siku hizi unasikia wamerekodi sauti sijui ya kiongozi au mtu mashuhuri katika nchi, wanazungumzia amani, amani, amani, utafikiri amani inapatikana kwa kuimbwa kama ngonjera. Amani ina misingi yake. Misingi hiyo ikiwekwa au kutekelezwa amani itadumu tu,” alisema Mbowe na kuongeza:



      “Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere, aliwahi kuhutubia akisema kuwa wakati anang’atuka madarakani, aliacha nchi ikiwa na amani, si kwa sababu watu hawakuwa maskini, umaskini ulikuwapo, lakini kulikuwa na amani.” “Alisema ni kwa sababu watu...wananchi walikuwa na mani na serikali yao. Walikuwa na matumaini na viongozi wao, walikuwa wanaamini katika Azimio la Arusha. Walikuwa wana matumaini ya haki katika nchi yao.” Alisema wananchi wanahitaji kuona matumaini katika elimu yao, elimu ya watoto wao, wananchi wanasumbuliwa na gharama za maisha zinazopanda kila kukicha, tofauti za kipato zinazidi kuwa kubwa na wanataka wakienda mahakamani watendewe haki, waone haki inatendeka, vinginevyo amani inayohubiriwa kwa maneno tu bila miundombinu ya matumaini na haki, itakuwa ni amani ya muda mfupi.



       Alimshambulia Msajili wa Vyama vya Siasa, John Tendwa, kuwa ni mtu aliyelewa madaraka na kudai kwamba kama angekuwa chini ya uongozi makini, alipaswa kufukuzwa kazi mara moja kwa kauli zake zinazohatarisha demokrasia na amani ya nchi. Mbowe huku akiwahoji wananchi kama wanakubaliana na maamuzi ya Kamati Kuu ya Chadema ya kuimarish kitengo cha ulinzi na usalama (Red Brigade) kwa kuwapa mafunzo ya ukakamavu, alisema mtu yeyote mwenye nia mbaya na nchi yake, hawezi kutangaza hadharani.  “Kauli za Tendwa zinazidi kuiponza serikali. Hazitawasaidia hata kidogo. Kwa kauli zake tu hizo alipaswa kuwa amefukuzwa kazi mara moja. Sasa kauli ya Mbowe ambayo naomba imfikie Tendwa ni hii, ajaribu kuifuta Chadema aone moto wake, hana mamlaka wala ubavu wa kuifuta Chadema. Binadamu anapodai haki yake, mnaweza kutumia mabomu kuua watu, kutesa, kuteka, na vitisho, lakini hatimaye itashinda kama ilivyokuwa Arusha,” alisema na kuongeza:



       “Unajua anaposema atafuta Chadema maana yake ni kwamba, anafuta Kambi ya Upinzani Bungeni, anafuta wabunge wote, hivyo uitishwe uchaguzi, anafuta madiwani 600 na kitu nchi nzima, hivyo uchaguzi urudiwe, anafuta wenyeviti wa vijiji, mitaa, vitongoji na wajumbe wao...huyu mtu amelewa madaraka...anatafuta fadhila kwa waliomweka hapo...hana busara hata kidogo, ajaribu aone moto.” Alisema vitisho, ambavyo Chadema na yeye binafsi wanakabiliana navyo kwa sasa, ikiwamo hivi karibuni kunusurika kwenye mlipuko wa bomu na risasi kwenye tukio la Arusha, havitawatia hofu na badala yake inawaongeza nguvu, kwa sababu wanajua wanasimamia haki, ukweli na matumaini ya Watanzania wote. Akisimulia tukio la bomu Arusha na namna waombolezaji walivyopigwa mabomu na risasi wakati wakitaka kuaga mwili wa marehemu, Mbowe alidai Chadema imeshinda kata 10 katika uchaguzi wa marudio wa kata 26, kwa damu za wanachama wake kumwagika.



       “Wananchi wa Songea, huu ni mkutano wangu wa kwanza kuhutubia hadharani tangu nilipokoswa koswa kuuawa kwa bomu, risasi za SMG na risasi za bastola kwenye tukio la Soweto, Arusha siku ya kuhitimisha kampeni. Lakini napenda niwaambie kitu kimoja, miye kama kamanda wenu mkuu, sitaingia hofu. Sasa tuna usongo zaidi na wametuongeza charge (nguvu) ya kuing'oa CCM chaguzi zijazo,” alisema na kuongeza: “Kama kuna mtu alifikiri kuwa kumuua au kutaka kumuua Mbowe atamtia hofu...huyo mtu ameshindwa. Kwa kweli siku ile mimi na wengine tuliokuwa walengwa kabisa wa lile tukio, tulinusurika kwa mipango ya Mungu tu. Ni kwa sababu tunaongozwa na Mwenyezi Mungu, tutaendelea kupigania haki hadi kieleweke.”



      “Sitamuogopa Rais, lakini nitamheshimu, sitaogopa polisi lakini nitawaheshimu, sitaogopa jeshi lakini nitaheshimu jeshi...sitamheshimu mtu yeyote asiye heshimu ubinadamu wa mtu mwingine. Uchaguzi wa juzi wa kata tumeshinda kwa mapambano ya damu. Watu wetu wamepigwa kila mahali, wamekatwa mapanga na mashoka na vijana wa CCM, Green Guard.” alidai. Alidai kuwa, katika kata ya Machila, wafuasi wa Chadema walitekwa nyara, wakapelekwa na kufichwa kwenye nyumba ya CCM, wengine wamebakwa, wengine wamewekewa chupa sehemu za siri. “Kwa sababu tu wanapenda Chadema, katika hali kama hiyo siwezi kucheka na polisi, ndiyo maana juzi tumetangaza kuwapatia vijana wetu mafunzo ya ukakamavu ili tujilinde na vitendo hivi” alisema kuongeza:


      “Hatuwezi wala hatuna mpango wa kuanzisha jeshi kama ambavyo polisi wanataka kupotosha kwa kusoma habari zinazoandikwa na magazeti ya CCM na kutangazwa na TBC. Nani hajui kuwa CCM wana kikundi kinaitwa Green Guard ambacho kiko nchi nzima, kinapiga wananchi, kinaumiza wapinzani na ushahidi tunao wa kutosha, kinapewa mafunzo ya kijeshi na ushahidi tunao.” Wakati huo huo, Chadema imetangaza kuwa imeandaa vitabu viwili, ambavyo vitazinduliwa hivi karibuni. Kitabu kimoja kinaonesha picha na kuelezea matukio mbalimbali ya namna ambavyo wafuasi na viongozi wake wamekuwa wakifanyiwa ukatili wa kinaowatuhumu kuwa ni vijana wa CCM. Kitabu kingine kinaelezea kwa muhtasari msimamo wa Chadema katika Rasimu ya Katiba Mpya.


      Naye Mwandishi Wetu kutoka Musoma anaripoti kuwa  Mbunge wa Musoma Mjini (Chadema), Vincent Nyerere, amemtaka Rais Jakaya Kikwete kuwataja na kuwachukulia hatua watu aliowahi kusema kwamba wanajishughulisha na biashara haramu ya dawa za kulevya. Alisema kama Rais Kikwete atashindwa kufanya hivyo basi akubali kubeba shutuma kwamba serikali yake ndio mratibu wa biashara ya dawa za kulenya kwa kinachodaiwa kutochukuliwa kwa hatua madhubuti.


Source: Ippmedia (July 2013).Chadema:Rasimu ya katiba kwa chopa. Retrieved from Ippmedia/Nipashe

1 comment:

Anonymous said...

CHADEMA SONGA MBELE MABADILIKO HAYAJI HIVIHIVI ILA KWA KUWA NA NIA MOJA KAMA WATU WENYE UCHUNGU NA NCHI YETU INAYOTEKETEZWA NA MAFISADI