TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imeahirisha tena uchaguzi katika kata nne za Jiji la Arusha, kwa sababu hali si shwari kuruhusu uchaguzi huru na wa haki. Kata ambazo zilipaswa kufanya uchaguzi Juni 30 ni Kimandolu, Elerai, Themi na Kaloleni ambazo uchaguzi wake uliahirishwa baada ya bomu kulipuka na kusababisha mauaji ya watu wanne na wengine kadhaa kujeruhiwa katika mkutano wa mwisho wa kampeni wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA). Akizungumza na gazeti hili kwa njia ya simu, Mkurugenzi wa Uchaguzi, Julius Malaba alisema: “Ni kweli tumeahirisha uchaguzi mdogo katika kata nne za Manispaa ya Arusha kwa kuwa hali bado si shwari kuruhusu uchaguzi huru na wa haki.”
Alipoulizwa kuhusu siku zilizoongezwa kama ndio kigezo cha kuwapo kwa hali ya utulivu na amani itakayoruhusu uchaguzi huru na wa haki kwa wananchi wa Arusha alisema: “Tunatumaini kuwa siku tulizoziongeza hadi tarehe 14 Julai hali ya Arusha itakuwa imetulia.” Aidha, katika kipindi chote hadi kufikia Juni 14, Tume ya Taifa imesema kampeni hazitaruhusiwa. Tume ya Uchaguzi (NEC) ilitangaza kurudiwa kwa uchaguzi mdogo katika kata nne za Arusha ambazo ni Kimandolu, Elerai, Themi na Kaloleni, ambazo zilisimamishwa kufanyika kwa uchaguzi mdogo wa madiwani kutokana na vurugu zilizojitokeza katika kampeni za mwisho. Akizungumzia uamuzi huo, Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa, Freeman Mbowe, alisema: “Uamuzi huu ni mzito na wa majonzi, hata chama hakikufurahi kuufanya, ila kwa kuwa tunasimamia utashi wa chama, ikifikia hatua kama hii hatuna budi kuchukua hatua.”
Source: Isango J. (June 2013). Uchaguzi wa madiwani Arusha mgumu. Retrieved from Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment