Wasiliana nasi : chademadiaspora@gmail.com -Fair and Balanced Platform- Twitter @ChademaDiaspora

Wasiliana nasi : chademadiaspora@gmail.com -Fair and Balanced Platform- Twitter @ChademaDiaspora
----------------------WE THANK AND APPRECIATE YOU FOR VISITING CHADEMA DIASPORA BLOG. AGAIN, THANK YOU!-----------------------

Friday, June 28, 2013

Serikali inamjua mlipuaji Arusha

MDEE ASEMA CHADEMA WATAKUWA WENDAWAZIMU KUJILIPUA



       MBUNGE wa Kawe, Halima Mdee (CHADEMA), ameitolea uvivu serikali akisema kuwa ilitumia nafasi ya kutokuwapo kwa wabunge wa chama hicho kutoa kauli zenye utata na zenye upotofu mkubwa bungeni kuhusu tukio la mlipuko wa bomu jijini Arusha. Tukio hilo la bomu lilitokea Juni 15 katika mkutano wa kufunga kampeni za udiwani ambapo watu wanne walipoteza maisha huku wengine 70 wakijeruhiwa. Katika kauli yake jana, Mdee licha ya kutomtaja kwa jina lakini alikuwa akimlenga Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi, aliyetoa kauli hiyo bungeni kwa niaba ya serikali, akisema wafuasi wa CHADEMA waliwazuia polisi kumkamata mlipuaji.

      Lukuvi katika taarifa hiyo alisema kuwa polisi walimwona mlipuaji wa bomu hilo lililosababisha vifo vya watu wanne na wengine sabini kujeruhiwa lakini kutokana na uchochezi wa wanasiasa, wakati wakimfukuza kumkamata wananchi wa CHADEMA walianza kuwashambulia kwa mawe. Mbali na Lukuvi, pia Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mwigulu Nchemba na mawaziri, Hawa Ghasia na Mary Nagu nao walikitwisha lawama CHADEMA wakidai kuwa kilihusika na mlipuko huo. Katika kujibu mapigo ya serikali na CCM, Mdee wakati akichangia mjadala wa Muswada wa Fedha jana bungeni, alitumia dakika chache za mwanzo kugusia tukio hilo la Arusha.

     “Mheshimiwa Spika, kwa kuwa ni mara yangu ya kwanza kuzungumza humu bungeni baada ya tukio la mlipuko wa bomu jijini Arusha, naomba nichukue nafasi hii kuwapa pole Wana Arusha. “Lakini vile vile nichukue nafasi hii kulaani vikali kauli zenye utata na zenye upotofu mkubwa zilizotolewa na serikali hapa bungeni. Serikali inajua nini kilichotokea Arusha, ilitumia kutokuwapo kwetu kupotosha lakini nashukuru kwamba ukweli utadhihiri,” alisema. Huku akipigiwa makofi na wabunge wenzake wa CHADEMA, Mdee alisema kuwa watakuwa ni wendawazimu kama chama wakijilipua mabomu wenyewe ili wapate umaarufu. “Hiki chama mnajua kasi yake na mnajua muziki wetu 2015 utakuwaje,” alisema Mdee huku wabunge wa CCM na mawaziri wakiwamo Lukuvi na Nagu wakibakia wamemkodolea macho.

      Katika kauli hiyo ya serikali kuhusu mlipuko wa bomu kwenye mkutano wa CHADEMA jijini Arusha, Lukuvi alisema imetenga sh milioni 100 kama zawadi kwa mtu yeyote atakayetoa taarifa zitakazofanikisha kunaswa kwa mhalifu wa matukio hayo. Lukuvi alisema mkutano wa CHADEMA ulikuwa na ulinzi wa polisi wenye magari mawili waliosimama upande wa kaskazini ya uwanja na mrushaji wa mlipuko huo akiwa upande wa mashariki ya uwanja huo na kurusha kuelekea magharibi. “Jaribio la askari kutaka kumfuata aliyerusha mlipuko huo lilizuiliwa na makundi ya wananchi ambao walianza kuwashambulia askari kwa mawe na kuwazomea, hivyo polisi kulazimika kuanza kujiokoa badala ya kumsaka mhalifu huyo,” alisema.

       “Hivi karibuni zimekuwapo jitihada za makusudi za baadhi ya vyama vya siasa, makundi ya kijamii na watu binafsi kupandikiza chuki ya raia dhidi ya vijana wetu wa polisi, kuwafanya raia wawachukie, wasiwaamini, wasiwape ushirikiano na kuifanya nchi isitawalike,” alisema. Alisema kuwa kufanikiwa kutoroka kwa mhalifu wa Soweto ni matokeo ya uchochezi unaofanywa kwa makusudi na baadhi ya wanasiasa dhidi ya serikali na polisi, hivyo kuwafanya wananchi wajenge chuki dhidi ya polisi. Lukuvi alisema kuwa tukio hilo la kanisani limehama kutoka kanisani kwenda kwenye mikutano ya kisiasa. Kwamba nia ni ile ile ya kuwafanya Watanzania wachukiane, wapigane na taifa hili liparaganyike.

Lissu alipuka

          Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu amesema kuwa manyanyaso na mateso wanayoyapata Watanzania kutoka kwa serikali ni mapito kwenye bonde la mauti ya kifo kuelekea kilele cha uhuru. Lissu alitoa kauli hiyo jana wakati akichangia muswada wa sheria ya fedha mwaka 2013 iliyowasilishwa bungeni na Waziri wa Fedha na Uchumi, William Mgimwa. Lissu ambaye pia ni Mnadhimu wa Kambi rasmi ya upinzani bungeni alinukuu kauli ya Rais wa zamani wa Afrika Kusini, Nelson Mandela aliyoitoa Septemba 21, mwaka 1953. “Mtoto wa Afrika wa pili ninayemzungumzia yuko kitandani anaweza kufa wakati wowote. Mwaka huo alisema maneno hayo baada ya kuwa amepigwa marufuku yeye na viongozi wenzake wa ANC kukutana.

       “Alisema kwa kuandika, hakwenda kwenye mkutano kwamba: ‘Barabara ya kwenda kwenye Uhuru si rahisi mahali kokote na wengi wetu watapita mara kwa mara katika bonde la mauti la kifo kabla ya kufika kwenye kilele cha matazamio yetu’,” alisema. Lissu aliongeza kuwa Tanzania hivi sasa imefika mahali serikali inapiga watu mabomu kwenye mikutano ya hadhara, inapiga wabunge, inakamata watu na kuwatesa bila sababu za maana. Alibainisha kuwa mkoani Mtwara watu wanakamatwa usiku, wanapigwa viboko na kumwagiwa maji ya chumvi. “Watanzania wanateswa, tunapita kwenye bonde la mauti ya kifo…mtasema sana. Watu wamekufa, watu wameuawa, Bunge linaendelea na vikao kama kawaida.

      “Kwa hiyo Mheshimiwa Spika, maneno ya Mzee Mandela ya hakuna njia rahisi kuelekea kwenye kilele cha Uhuru, na wengi wetu lazima tutapita kwenye bonde la mauti kabla ya kufika kwenye Uhuru…ni maneno muhimu na tutayakumbuka siku kama ya leo ambapo mzee Mandela yupo kitandani,” alisisitiza. Hata hivyo, baada ya kutoa kauli hiyo Spika wa Bunge, Anne Makinda alisimama akipinga kuwa Bunge halikuacha kufanya vikao vyake kwasababu alizozisema Lissu. ‘‘Mheshimiwa Tundu Lissu yote uliyoyasema ni sawa, lakini hilo la kwamba Bunge hatukuacha kwa sababu uliyoisema si sahihi,” alisema. Awali Lissu alianza hoja yake akisema atawanukuu watoto wawili wa Kiafrika ambapo alianza na hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere kwa kauli yake ya mwaka 1995 katika mkutano wake na waandishi wa habari kwamba serikali ya wala rushwa haiwezi kukusanya kodi.

     Lissu alionesha takwimu mbalimbali za jinsi kampuni za madini zinavyochimba madini Tanzania na zinavyolipa kodi kidogo wakati wafanyakazi walioajiriwa wanalipa kodi kubwa zaidi. Alisema kuwa kati ya mwaka 1999 hadi 2004 kampuni za madini zililipa kodi sh sifuri kama kodi ya mapato wakati wafanyakazi wake walilipa sh bilioni 51.82. Lissu aliongeza kuwa katika kipindi hicho hicho 1999 hadi 2012, kampuni hizo zililipa kodi ya mapato ya sh bilioni 467.98 na wafanyakazi walilipa kodi za sh bilioni 505.4. “Mwaka 2001 hadi 2012, kampuni za madini zililipata mapato ya dola za Marekani bilioni 11.9 sawa na sh trilioni 19.635 na kipindi hicho zililipa kodi sh trilioni 1.216 au asilimia sita ya mapato yao,” alisema.

Source: Kamkara E. (Jne 2013). Serikali inamjua mlipuaji Arusha. Dodoma. Retrieved from Tanzania Daima

No comments: