JIBU LA SWALI LA MBUNGE MPANDA MJINI
MBUNGE wa Mpanda Mjini, Said Arfi (CHADEMA), ameihoji serikali ni kwanini inaendelea kuagiza samaki kutoka nchi za nje kama Yemen na India wakati Tanzania inazalisha samaki wa kutosha. Alitoa hoja yake bungeni jana alipokuwa akiuliza swali la nyongeza kwa kuitaka serikali ieleze ni kwanini inafanya hivyo na kama kwa kufanya hivyo haioni inashusha thamani ya soko la bidhaa za ndani. Awali katika swali la msingi, Mbunge wa Viti Maalumu, Mkiwa Kimwanga (CCM) alitaka serikali ieleze ni kwanini isifikie uamuzi wa kulifufua Shirika la Uvuvi la Taifa (Tafico), ili litoe huduma na kutoa ajira kwa vijana wengi katika sekta ya uvuvi.
Akijibu maswali hayo, Naibu Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Benedict ole Nangoro, alisema pamoja na kuwapo kwa samaki kutoka nje, lakini si kweli kuwa ni kushusha thamani ya bidhaa za ndani. “Najua kuna uagizaji wa samaki kutoka nje, hiyo inatokana na vionjo vya soko huria wala si uhaba wa samaki kutoka katika maziwa yetu, wakati mwingine ni matakwa ya walaji kutokana na utamu wa samaki ambao huwa wamehifadhiwa katika makopo,” alisema Ole Nangoro. Akizungumzia Shirika la Tafico, alisema lengo kubwa la kuanzishwa ni kuendesha shughuli za uvuvi kibiashara hapa nchini.
“Serikali ilitoa tamko la kubinafsisha mashirika ya umma ambapo Tafico ilikuwa chini ya Tume ya Rais ya Kurekebisha Mashirika ya Umma mwaka 1998 hadi Oktoba, mwaka 2005,” alisema. Aidha, alisema shughuli za uvuvi kwa sasa zinafanywa na sekta binafsi ambapo hadi mwaka 2011/2012 wavuvi waliosajiliwa walikuwa 18,816 wakiwamo wavuvi wa kati 75.
Source: Kaijage E. (June 2013). Arfi ahoji serikali kuagiza samaki nje. Dodoma. Retrieved from Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment